Wabunge kumbukeni hakuna amani kwenye dhuluma ya haki!

chibidula

Member
Jan 3, 2011
63
39
Miongoni mwa kauli nyingi za wanasiasa wetu zilizosisimua sana tokea mwaka huu uanze, ni ile iliyotamkwa ndani ya Bunge letu tukufu la Tanzania na mmoja wa waheshimiwa wawakilishi wetu bungeni ya ‘Tufunge milango tupigane ngumi!'. Kauli hii, ambayo katika hali yoyote ile inasisimua na ni ngeni, ilitolewa wakati wa kikao cha Bunge hilo pale wabunge wetu walipotunishiana misuli, kimaneno zaidi kuliko kivitendo, wakibishana kuhusu matumizi ya kanuni mojawapo ya Bunge.
Tumezoea kusoma kwenye vyombo vya habari na mitandao na kuona (na kuchekelea!) picha za wabunge wa nchi kadhaa duniani wakitoleana kauli za kifedhuli na kufikia hatua ya kushikana mashati na kusukumana wakiwa ndani ya kumbi zinazopaswa kuheshimiwa za Bunge za nchi zao. Mfano, Mei mwaka huu, Spika wa Bunge la Kuwait, Mheshimiwa Jassim Al-Kharafi alilazimika kusitisha kikao cha Bunge kwa siku kadhaa hadi mwishoni mwa mwezi huo baada ya wabunge kadhaa kutiana makofi wakati wa kikao cha Bunge kufuatia mjadala mkali uliohusu kurejeshwa ama kutorejeshwa nchini humo raia wawili wa Kuwait wanaoshikiliwa kwenye kizuizi cha Wamarekani kwenye rasi ya Quantanamo.
Pia mwishoni mwa mwaka jana tulishuhudia kupitia mitandao na luninga zetu, na kuchekelea, ngumi na matusi vikivurumishwa ndani ya ukumbi wa Bunge la Korea ya Kusini kati ya wabunge wa chama cha upinzani cha Democratic Party na kile tawala cha Grand National Party GNP cha Raisi Lee Myung-bak. Chanzo cha purukushani hiyo iliyofikia hata Spika kutaka kunyanyuliwa kwenye kiti chake na wabunge wanawake kuwa mstari wa mbele kujaribu kukikalia, ilitokana na chama kinachoongoza Serikali cha raisi huyo kukataa kupitisha muswada unaotaka serikali kutoa chakula cha bure kwa wanafunzi wa shule za chekechea hadi za kati ambazo huku kwetu ni za sekondari.
Kadhalika, Bunge la nchini Nigeria baada ya kusomwa kwa tangazo la kuwafungia Wawakilishi saba ambao walidaiwa kumtuhumu Spika wa Bunge hilo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma. Katika tafrani hiyo, mbunge Solomon Ahwinahwi kutoka kundi linalojiita Progressives ndani ya chama cha People's Democratic Party linalotaka spika wa bunge hilo mheshimiwa Oladimeji Bankole kung'oka kwenye kiti chake alivunjika mkono na kulazimika kupata matibabu.
Zipo taarifa nyingi tu za wabunge wa nchi za Japan, India, Nigeria, Ukraine na kwingineko za waheshimiwa wabunge wa mabunge hayo kuamua kushikana mashati pale wanapoamini kuwa mambo bungeni na nchini mwao yanaendeshwa ndivyo sivyo na waliowapa madaraka. Sishabikii magomvi miongoni mwa wanasiasa wetu, lakini inapofikia mahali maswali na majibu yanayoulizwa na kujibiwa ndani ya ukumbi wa Bunge ni mizaha tu ambayo mwisho wa siku haimsaidii chochote mkulima na mfugaji wa kijijini Sitimbi, Mgwashi, Kimbiji na Mahezangulu na kwingineko, pengine tunalazimika sasa kuangalia taratibu mpya za kupata majibu muafaka ya matatizo yetu kutoka kwa walio madarakani!
Hoja yangu hapa ni kuwa wabunge walioamua kutupiana ngumi kwenye mabunge yao sio kwamba wanapenda sana ugomvi ama ni wakorofi, la hasha. Inawezekana kabisa kuwa pengine nchi zao zina ‘amani, uvumilivu na mshikamano' mkubwa zaidi kuliko ule tunaojidai nao sisi. Lakini inafika mahali wabunge wanashindwa kuvumilia majibu ya juu juu na ya kebehi kutoka kwa watawala ambayo hayatoi suluhisho la kueleweka kwa matatizo ya wananchi wanaowawakilisha, ndipo wanaamua kushikana mashati hadi kieleweke.
Ninachojaribu kuonyesha hapa ni kuwa mwisho wa siku kila binadamu ana kipimo chake cha uvumilivu. Inafika mahali anaamua kuwa liwalo na liwe na kufanya chochote ili mradi kupata kile anachoamini kuwa ni haki yake. Wapo wabunge wenye uchungu wa kweli na wapiga kura wao. Wanapouliza swali linalohusu matatizo ya wananchi wa jimbo lake halafu mhusika akajibu swali hilo kwa mizaha na kebehi kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge, wa pili na tatu swali lile lile na majibu yale yale, tusishangae mbunge huyo kuishia kumkwida mhusika akimtaka aache mizaha linapokuja suala linalohusu maisha ya wapiga kura wake!
Kwa hakika, kama inafika mahali tukaulizwa kibunge kuwa wanaotaka waheshimiwa wafunge milango wachapane makofi ndio tutapata umeme bila mgawo, shule zetu za kata ziwe na madawati na maabara, zahanati zetu vijijini ziwe na dawa za kutosha, mabomba yetu ya maji yatoe maji badala ya tando za buibui na kadhalika waseme ndioo, kidole changu kitakuwa cha kwanza kwenda juu na kujibu ‘ndiyooo'! Naam, na kugonga dawati kwa msisitizo zaidi. Nisingependa wabunge wetu wafikie hatua ya kushikana mashati na kutiana vibao, lakini nisingependa pia Bunge letu kuishia kuwa malighafi ya vichekesho vya msanii wetu Masanja aliyepata kusema kuwa kila mheshimiwa anayesimama ni; "kwa kuwaa…na kwa kuwaa…na kwa kuwaaa…!" kama vile hakuna maneno mengine ya Kiswahili!
Source: www.kwanzajamii.com
 
Back
Top Bottom