Waathirika wa mafuriko waanza kuhamishwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,293
33,078
Hatma ya wapangaji kitendawili



Kumekuchamabwe(1).jpg

Baadhi ya wathirika wa mafuriko katika kambi ya Azania wakipandisha mizigo yao katika gari la jeshi la ulinzi tayari kuhamia katika kambi nyingine ya Ubungo Maziwa kupisha wanafunzi kuanza masomo.


Malori aina ya Fuso jana yalifanya zoezi la kuwahamisha waathirika wa mafuriko waliokuwa wakiishi katika makambi mbalimbali waliotengewa jijini Dar es Salaam kulekea kwenye makazi mapya ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo kesho.

Hata hivyo, wapangaji ambao pia waliathirika na mafuriko hayo ambao walihifadhiwa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuondolewa kambi hiyo bila kupangiwa mahali pengine pa kuishi na kulazimika kujipa hifadhi nje ya ukuta wa shule hiyo.

Zoezi hilo ambalo lilisimamiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mgambo na askari wa ulinzi, liliendeshwa kwa utulivu huku kila muathirika akiitwa jina na kuingia kwenye lori akiwa na mizigo yake kwenda kwenye makazi mapya waliyotengewa ya Ubungo Maziwa na JKT Mgulani.

Baadhi yao walikuwa wanaishi katika makambi ya Shule ya Sekondari ya Azania, Shule ya Msingi Rutihinda na Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko.

Muda wa mwisho uliotengwa kwa ajili ya kuhama kwenye makambi hayo ilikuwa Ijumaa (juzi) lakini hata hivyo, magari yaliyopangwa kuwahamisha yalichelewa kufika makambini na kulazimika kuwahamisha jana.

Mmoja wa wapangaji walioathirika na mafuriko hayo, John Fredirick, alimwambia mwandishi wa NIPASHE Jumapili kuwa anasikitishwa na kitendo cha serikali kuwaacha katika mazingira magumu ambayo hawajui hatma yao.

Alisema tangu jana asubuhi wamekosa huduma muhimu kama ya chakula, mahali pa kujisaidia na pa kujihifadhi. Aliiomba serikali iwasaidie fedha kidogo itakayowasaidia kutafuta nyumba za kupanga ili waweze kujisitiri na familia zao.

Muathirika mwingine, Charles Yolam, alisema kwamba walioathirika kwa kiasi kikubwa kwenye mafuriko hayo ni wapangaji lakini wanashindwa kuelewa kwanini serikali inashindwa kuwapatia haki yao.

Alisema wenye nyumba wengi wanajenga nyumba zao na kuwaacha wapangaji wakae wakati wenyewe wanakwenda kuishi sehemu nyingine.

Alisema serikali ilipowatoa mabondeni na kuwapeleka kwenye makambi, iliwaahidi kuwa itawatafutia sehemu za kuishi lakini wanashangaa kuwatelekeza. "Tutakaa kwenye hizi kuta mpaka kieleweke,", alisema Yolam huku akisisitiza kuwa serikali ina jukumu la kuwaangalia kama binadamu wengine waliopatwa na maafa.

Sakina Mohamed, alidai Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipowatembelea kwenye kambi yao alisema wapangaji ndio waanze kutafutiwa maeneo kwa kuwa wao ndio waathirika wakubwa.

"Tumeshangaa jana askari wanakuja kutuondoa na kutuambia tukatafute sehemu za kuishi hapa hatutakiwi," alisema.
Alisema anashangaa serikali kutoa kipaumbele kwa wenye nyumba peke yao wakati viongozi wake walipokuwa wakitafuta kura katika uchaguzi, walikuwa wanaomba kwa wote (wapangaji na wenye nyumba).

HATMA YA WAPANGAJI


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Yordan Rugimbana, alipoulizwa na NIPASHE Jumapili juu ya hatma ya wapangaji walioachwa alisema msimamo wa serikali uko palepale haitawasidia kwa lolote wanachotakiwa ni kutafuta maeneo waondoke.

Alisema kuwa atakwenda kwenye kambi hizo kukagua kama bado kuna wanaendelea kuishi kwenye kambi hizo na kuahidi kutoa taarifa kwa hatua inayofuatia.

UGAWAJI VIWANJA BAADA YA WIKI MBILI


Awamu ya kwanza ya ugawaji wa makazi mapya kwa waathirika wa mabondeni wilayani Kinondoni yaliyotengwa na serikali eneo la Mabwe Pande jijini Dar es Salaam utaanza wiki mbili zijazo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, ameliambia NIPASHE Jumapili jana kuwa, zoezi la ugawaji wa maeneo hayo umegawanyika sehemu mbili.

Rugimbana alisema awamu ya kwanza itahusisha viwanja 630 ambavyo hadi kufikia jana vyote vilikuwa vimeshapimwa na kwamba zoezi linaloendelea ni ujenzi wa mahema na huduma nyingine.

"Wiki mbili zitakapokamilika tunatarajia ujenzi wa mahema utakuwa umekamilika na mara moja awamu ya ugawaji wa maeneo kwa waathirika nao utaanza, " alisema.

Alisema kuwa, awamu ya pili ya upimaji wa viwanja vingine pamoja na ujenzi wa mahema hayo nao utafanyika kwa wiki mbili ili kuweza kufikia lengo la viwanja 1,000 ambavyo ndivyo vilivyokusudiwa.

"Tumefanya kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ndio inaendelea na ile ya pili itachukuwa wiki mbili kama hii ya kwanza, tunawaomba wananchi wawe na subira na uvumilivu." alisema.

Gazeti hili lilishuhudia jana mchana zoezi la ujenzi wa mahema na huduma nyingine za kijamii ukiendelea kwenye eneo hilo la Mabwe Pande.
Ujenzi huo ulikuwa ukifanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na kikosi cha maafa na uokoaji Tanzania Red Cross ambapo hata

hivyo ulionekana kutoenda kwa kasi. Aidha, huduma nyingine ambazo zimewekwa ni pamoja na maji, uchongaji wa barabara.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, aliliambia gazeti hili kuwa, tayari wameshawahamisha waathirika kutoka

kwenye kambi za awali kwenda zile walizozitenga ambazo ni Ubungo Maziwa, Jeshi la Kujenga Taifa, Mbweni na ile ya Mgulani.
Sadiki amewaomba wananchi kuwa na moyo wa subira wakati serikali ilifanya juhudi za kutayarisha makazi mapya.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Back
Top Bottom