Waalimu 16,000 wa Sekondari wakosa ajira

Vumbi

Senior Member
Nov 7, 2010
191
27
WAKATI Shule za Sekondari za Serikali zikikabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu, imebainika kuwa walimu 16,000 waliohitimu shahada ya kwanza na stashahada kati ya Mei na Julai mwaka huu, hawajapangiwa vituo vya kazi.Katika hali ya kawaida, walimu wanapohitimu mafunzo, serikali inawapangia vituo vya kazi ndani ya miezi miwili, lakini mwaka huu, walimu hao wamesubiri kwa zaidi ya miezi tisa bila kuelezwa lolote kuhusu ajira.

Hatua hiyo imewafanya baadhi ya walimu hao, kusota katia ofisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wakitaka kujua hatima yao huku wengine wakilazimika kutafuta ajira za muda mitaani, ili kukabiliana na ugumu wa maisha.

Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), zilisema walimu hao wako mitaani baada ya kukosa ajira.

Kwa mujibu wa habari hizo, moja ya sababu za walimu hao kuchelewa kupangiwa vituo vya kazi, ni uhaba wa fedha serikalini.

"Ukweli ni kwamba serikali haina hela, lakini kibaya inachofanya ni kutosema ukweli. Ni Bora wakawaambia walimu hao ukweli ili nao wajue watasubiri kwa muda gani," kilisema chanzo chetu ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Baadhi ya walimu hao, waliliambia gazeti hili kuwa hali hiyo ni ya kusikitisha na kwamba wanashindwa kuelewa sababu za serikali kutokuwa wazi kuhusu hatuma yao.

"Jambo la kushangaza ni kuona walimu wa shule za msingi wanapata ajira mara tu baada ya kumaliza vyuo, lakini walimu wa sekondari tunatelekezwa na kuachwa tukitangatanga mitaani," alisema mmoja wa walimu aliyekutwa kwenye Ofisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Mwalimu huyo ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alipofuatilia ajiri yake kwa mara ya mwisho, alielezwa kuwa angepangiwa kituo cha kazi Oktoba mwaka huu lakini, hadi sasa hajaambiwa chochote.

Mwalimu mwingine ambaye amehitimu shahada ya ualimu alisema anashindwa sababu za kutowapangia vituo vya kazi walimu hao wakati imeshatumia fedha nyingi kuwasomesha.

Alisema shule nyingi za sekondari, zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu lakini, serikali inashindwa kuwapatia kazi.

"Ukweli ni kwamba walikuwa wengi lakini baada ya kuona ubabaishaji umekuwa mwingi, wengine wameamua kufanya kazi zingine. Watu wamechoka kusubiri bila maelezo ya lini subiri hiyo itafikia mwisho," alisema

Kwa upande wake, Rais wa Chama Cha walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema kitendo hicho kinawavunja moyo walimu ambao bado hawajaariwa.

Kwa mujibu wa Mukoba , baadhi ya walimu hao sasa wamelazimika kutafuta kazi katika kampuni binafsi, zikiwemo za simu, ili kujikwamua kimaisha.

"Bajeti ya kuajiri walimu ilitolewa tangu Juni mwaka huu sasa kinachoonekana hapa fedha hizo zimetumika kwenye kampeni ama zimetumika kwenye mambo mengine ambayo si ya muhimu," alisema Mukoba.

Rais huyo wa CWT alipuuza maelezo kwamba kilichokwamisha ajira za walimu hao ni uchambuzi wa majina ya walioenda kujiendeleza.

"Suala la walimu kujiendeleza, vibali vinatolewa na serikali yenyewe sasa iweje waseme wanafanya uchambuzi wa majina wakati utaratibu huo wanaufahamu,"alisema.

Alielezea wasiwasi wake juu ya uwezekano mkubwa serikali kuajiri idadi ndogo ya walimu wakati itakapoajiri kwa sababu wengi watakuwa wameingia katika ajira nyingine.

Awali Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, (Menejimenti na Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, aliwataka walimu hao kuvuta subiri hadi Januari mwakani serikali itakapotangaza ajira zao.

Waziri Ghasia alisema walimu hao wanapaswa kuwa na subira kwa sasabu kwa sasa serikali inafanya uchambuzi wa majina yao kabla ya kuwapangia vituo vya kazi.

"Unajua kuna walimu waliokwenda kusoma wengine kujiendeleza wakiwa kazini na kuna wale ambao wanatoka moja kwa moja vyuoni. Kwa hiyo lazima tufanye uchambuzi wa majina yao. Kazi hii itafanyika hadi Januari mwakani," alisema waziri Ghasia.

Alisema utaratibu wa kupitia majina kabla kupanga vituo vya kazi, unalenga katika kuepuka uwezekano wa mwalimu kupangiwa kituo zaidi ya kimoja.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alisema, alilitaka gazeti hili liwasiliane na afisa habari wake kwa sababu yeye yuko mkutanoni.
"Naomba umuulize msemaji wa wizara ambaye ni ofisa habari mkuu wa wizara, atakupa ufafanuzi wa suala hilo maana nimebanwa na shughuli za kikao,"alisema Dk Kawambwa.

Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margreth Kishiwa alisema wizara hiyo haihusiki na kuwapangia walimu vituo vya kazi na kwamba jukumu lake ni kutoa mafunzo tu.

Source:
Mwananchi Monday, 27 December 2010 08:52
 
Back
Top Bottom