Vitambulisho Z`bar vyawasha moto Bara

JuaKali

JF-Expert Member
Nov 14, 2007
776
118
Sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi inayolenga kuwaengua wananchi kutoka Tanzania Bara kuajiriwa Zanzibar, imezua mjadala mkali miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa na serikali, baada ya baadhi yao kuiunga mkono na wengine kuipinga wakisema kwamba itasababisha chuki na mapigano miongoni mwa Watanzania iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaipitisha.

Kati ya wanaoiunga mkono sera hiyo iliyowekwa bayana juzi na SMZ ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Saleh Ramadhani Ferouz.

Wanaopinga uanzishwaji wa sera hiyo kwa misingi ya ubaguzi wa ajira kwa wananchi kutoka Tanzania Bara, ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.

Baregu aonya
Profesa Baregu alisema kutatokea chuki na mapigano ikiwa serikali ya SMZ itapitisha sera ya vitambulisho vya mkaazi vinavyolenga kumzuia mwananchi kutoka Tanzania Bara kupata ajira huko.Alitoa kauli hiyo wakati akitoa maoni yake juu ya uamuzi wa SMZ kutunga sera hiyo.

Alisema sera hiyo haifai kwa kuwa itasababisha kuwepo kwa chuki kati ya pande hizo mbili.

Kauli ya SMZ kutaka kupeleka sera hiyo ya vitambulisho vya mkaazi katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea visiwani humo ilitolewa juzi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Suleiman Othuman Nyanga.

Aidha, Profesa Baregu alisema, kasoro hizo zinajitokeza kutokana na katiba mbovu ya Muungano iliyopo sasa.
Alishauri kama SMZ inataka kufanya hivyo kwanza kuwepo kwa majadiliano ya pande mbili za Muungano badala ya kukurupuka.

Alisema kama sera hiyo itawaathiri Wabara kuna uwezekano mkubwa wa kulipiza visasi kwa Wazanzibari wanaoishi na kufanya kazi upande wa Bara.

Alifafanua kuwa matatizo mengi ya Muungano yakiwemo ya pasi za kusafiria kuja Bara yaliondolewa mwaka 1995, lakini anashangaa tena vitu kama hivyo kuibuliwa.

Aliongeza kuwa Zanzibar imeshindwa kuwa na siasa za tahadhari jambo ambalo ni hatari kwa hali ya sasa.
Profesa Baregu alisema, hiyo ni dalili kubwa ya kuwepo haja ya kuifanyia marekebisho ya Katiba ya Muungano ili kuondoa vitu kama hivyo.

Lipumba: visitumike kwa ajira

Akizungumza na Nipashe jana, Profesa Lipumba alisema anaunga mkono sera ya kuwapo vitambulisho kwa Wazanzibari kwa madai kwamba suala hilo si la Muungano.

Lakini akasema anapinga utekelezaji wa sera hiyo kwa misingi ya ubaguzi kwa vile suala hilo litavunja umoja wa kitaifa na kufuta mjadala unaoendelea wa uanzishwaji wa soko la ajira ya pamoja katika nchi za Afrika Mashariki.

``Ni vizuri tukawa na vitambulisho vya kitaifa, kwa Wazanzibari kuwa na vitambulisho, lakini kama kuwapo kwa vitambulisho kutakuwa ni kwa ubaguzi, kunaweza kuharibu majadiliano ya kuanzishwa soko la ajira ya pamoja katika Afrika Mashariki, pia badala ya kutuweka karibu, litazusha mtafaruku miongoni mwa Watanzania,`` alisema Profesa Lipumba.

Hata hivyo, alitahadharisha vitambulisho vinavyokusudiwa kutolewa kwa Wazanzibari kutumika kupiga kura katika uchaguzi, badala ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) akisema kwamba, kitendo hicho kinaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani nchini.

Mrema: Huu ni mgogoro mpya
Naye Mwenyekiti wa TLP, Mrema alisema sera ya vitambulisho kwa Wazanzibari, imedhihirisha kwamba kuna tatizo kubwa katika Muungano kuliko serikali inavyofikiria na akaonya kuwa kama hatua hazitachukuliwa haraka, hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika siku za usoni.

``Nashauri Muungano uwe negotiated (ujadiliwe), kwani hatuwezi kuishi kwa vitisho kila kukicha tutakuwa tunamtawala nani?`` alihoji Mrema.

Mbatia: Ni kero mpya

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Mbatia alisema utekelezaji wa sera hiyo kwa misingi ya ubaguzi, unazidi kuongeza kero za Muungano ambao hadi kufikia sasa una umri wa miaka 44, badala ya kuzipunguza.

``Wazanzibari tujijue sisi ni taifa moja kwani hawawezi kuingia kwenye global system (mfumo wa dunia). Umoja wa Mataifa hakuna taifa la Zanzibar, hivyo waangalie kwa mapana dunia ya leo. Kwani ustawi wa taifa lao utadidimia, utasababisha Watanganyika nao wataanza kuzungumzia Utanganyika,`` alionya Mbatia.

Ferouz: Ni jambo jema

Wakati Profesa Lipumba, Mrema na Mbatia wakisema hayo, Ferouz alisema anaunga mkono sera hiyo kwa vile ni jambo jema kwa Wazanzibari kupewa kipaumbele na kuongeza kuwa Zanzibar ina mamlaka ya kufanya mambo yake na kwamba, hakuna Wazanzibari wanaofanya kazi Tanzania Bara hasa kwenye mahoteli kama ilivyo Visiwani huko.

``Kwanza hiyo sera ilichelewa, walikuwa wameshaanza ku-emplement (kutekeleza), lakini sera ilikuwa haipo,`` alisema Ferouz.

Hata hivyo, alisema haungi mkono maoni ya kuwataka wananchi kutoka Tanzania Bara kuingia Zanzibar kwa kutumia paspoti.

Khatib: Udogo wa Zanzibar umechangia

Naye Waziri Khatib alisema haujui mjadala wa sera hiyo kwa sababu hakushiriki pia hajui hatima yake kwenye Mkutano wa Baraza la Wawakilishi unoendelea visiwani humo, lakini akasema Wazanzibari wana haki ya kuwa na vitambulisho kwani vitasaidia kuwatambulisha wakati wa kupiga kura katika uchaguzi wa Wawakilishi na Rais.

Hata hivyo, Waziri Khatib alisema anadhani hatua ya SMZ kuamua kutunga sera hiyo kwa lengo la kuwapa kipaumbele Wazanzibari katika ajira, inatokana na Zanzibar kuwa kisiwa kidogo, chenye nafasi ndogo ya ajira, lakini kina watu wengi.

``Zanzibar ni kisiwa kidogo, kina watu wapatao milioni moja hivi, kina nafasi ndogo ya ajira, hivyo wanafikiri kwamba ni busara wawape nafasi hizo za ajira Wazanzibari wachache waliopo. Lakini sidhani kama watawazuia wananchi wa Bara,`` alisema Waziri Khatib.

Wakati huo huo, SMZ imesema kwamba suala la kurejesha hati za kusafiria kwa watu wenye asili ya Tanzania Bara wanaoingia Zanzibar linazungumzika.

Waziri Shaaban: La paspoti linajadilika

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Ramadhani Abdallah Shaaban, alipokuwa akichangia mjadala wa sera mpya ya vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi Zanzibar katika Mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea mjini hapo.

Waziri Shaaban alisema Zanzibar inaweza kudai kurejeshwa kwa utaratibu huo kwa vile utaratibu huo ulifutwa kutokana na maombi yaliyotolewa na wananchi wenyewe wa Zanzibar kwa malengo ya kuimarisha sekta ya biashara nchini.

``Zanzibar ndiyo iliyodai kuondolewa kwa hati za kusafiria kwa watu kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar,`` alisema Waziri Shaabani.

Alisema kwamba wananchi wa Zanzibar wapatao 15 waliwasilisha maombi yao katika serikali ya Muungano kutaka utaratibu huo kuondoshwa kwa malengo ya kukuza sekta ya biashara na kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa mwaka 1964.

``Matumizi ya hati za kusafiria kwa watu wanaoingia Zanzibar wakiwemo kutoka Tanzania Bara ni mambo yanayozungumzika,`` alisema Waziri Shaaban.

Aidha, alisema kwamba kama kumeonekana kuna madhara baada ya kuondosha utaratibu huo SMZ inao uwezo wa kushughulikia tatizo hilo.

Alisema kwamba lengo la kuanzishwa kwa vitambulisho vya Mzanzibari ni kutaka kuwatambua Wazanzibari wakaazi ili serikali iweze kupanga mipango yake ya maendeleo kwa wananchi kulingana na idadi ya watu.

Vilevile, alisema kwamba suala la kumtambua nani Mzanzibari ni jambo ambalo limeoanishwa katika sheria ya Mzanzibari mkaazi na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Akifunga mjadala huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, alisema kwamba serikali inatarajia kutoa Vitambulisho vya muda kwa watu wote wanaoishi Zanzibar ambao siyo Wazanzibari.

Waziri Nyanga alisema kwamba kutokana na mchanganyiko katika jamii kati ya wazawa na wageni kuna haja kwa watu hao kupatiwa vitambulisho ili waeleweke sambamba na kupatiwa haki zao za kijamii.

Imeandaliwa na Muhibu Said, Richard Makore, Dar na Mwinyi Sadallah Zanzibar.

SOURCE: Nipashe
 

Atleast it's now diluted....

---------------------------------
WATANZANIA Bara hawawezi kulazimika kuingia Zanzibar kwa pasipoti kutokana na sheria ya uraia kukataza utaratibu huo ndani ya Jamhuri moja.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani Bw. Abdi Ijimbo, wakati akizungumza na Majira kuhusu hoja zilizoripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni, vikiwanukuu baadhi ya watu wakisema ni vyema Watanzania Bara waingie Zanzibar kwa pasipoti.

Bw. Ijimbo alisema sheria za Uhamiaji zinaruhusu Mtanzania anayetaka kutoka nje ya nchi kuwa na pasipoti, ili ajulikane kuwa ni Mtanzania aliyefuata taratibu ambazo zipo duniani kote.

"Hadi sasa Serikali haina sababu ya kuanzisha pasipoti kuingia Zanzibar, kwa vile hakuna sheria inayosema hivyo na Zanzibar ipo katika Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, ndiyo maana hata huko nyuma hati ya kuingilia Zanzibar ilifutwa," alisema.

Bw. Ijimbo aliongeza kuwa katika Serikali ya Awamu ya Pili, Watanzania Bara walikuwa wanaingia Zanzibar kwa hati ambayo ilikuwa pia haina hadhi ya pasipoti, bali ulikuwa ni utaratibu fulani tu uliowekwa na baadaye kuonekana hauna sababu ya kuendelea kuwapo.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya Watanzania wanazungumzia jambo hilo ndani ya nchi zilizoungana na kuwa kwenye Jamhuri ya Muungano.

Nayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesisitiza kwamba vitambulisho vinavyotolewa vya Mzanzibari mkazi ni kwa wale tu wanaoishi visiwani humo, anaripoti Ali Suleiman.

SMZ imesema Watanzania kutoka Bara wataweza kutambuliwa kwa vitambulisho hivyo, baada ya kutimiza masharti yaliyopo.

Imesema vitambulisho hivyo havina malengo ya kisiasa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu kwamba ni mikakati ya CCM kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Akitoa juzi majumuisho ya mjadala wa sera ya vitambulisho vya Mzanzibari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali Zanzibar, Bw. Suleiman Othman Nyanga, alisema Zanzibar haiwezi kutoa vitambulisho vya uraia kwani yenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Serikali ya Muungano.

Alisema sera iliyoandaliwa ni ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi na si ya vitambulisho vya Mzanzibari.

“Mheshimiwa Spika ni vyema kutambua kuwa hii sera ni ya vitambulisho vya Mzanzibari kwa sababu michango mingi iliyotolewa, imezungumzia suala la Mzanzibari, lakini hapa tunasema ni sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi kwa sababu Mzanzibari tunayetaka kumpa kitambulisho ni yule ambaye anakaa Zanzibar,” alisema Waziri huyo.

Waziri Nyanga alisisitiza, kwamba vitambulisho hivyo hatapewa Mzanzibari anayekaa nje ya visiwa hata kama anakaa Dar es Salaam, lakini ikiwa si mkazi, hatakuwa na halali ya kupata kitambulisho hicho, ambacho ni kwa ajili ya Wazanzibari wanaoishi Unguja na Pemba.

“Tunayemsema sisi hapa ni Mzanzibari mkazi ndiye tutakayempa kitambulisho, kama anakaa Dar es Salaam maadam si mkazi yeye hahusiki na kitambulisho hiki cha sera hii, ambayo tunataka kuipitisha,” alisema.

Waziri huyo alisema SMZ haitatoa vitambulisho vya uraia kwa sababu suala hilo ni la Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amaan Karume alitoa vitambulisho vya uraia kwa Zanzibar.

“Wakati huo vitambulisho kweli vilitolewa na viliitwa pasi ya uraia iliyotolewa wakati huo na kwa kuwa kuna neno uraia, na uraia kwa Tanzania ni mmoja, kwa hivyo vitambulisho hivyo kama utavitazama vitakuwa vimeandikwa pasi ya uraia na vimeandikwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zanzibar ... haikuwa pasi ya uraia ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema.

Alisema watakaopaswa kupewa vitambulisho ni wale walioamua kuwa wakazi wa Zanzibar, ambao watakuwa na makazi yao ya kudumu na watakuwa wanahitaji huduma za kila siku za Serikali ambao takwimu zao zitasaidia kupanga mipango ya maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Waziri Nyanga alisema Mzanzibari yeyote anayeishi nje ya Zanzibar anapoamua kurudi Zanzibar, basi ana haki ya kuomba kitambulisho na atapewa baada ya kuthibitisha kuwa na sifa zinazohitajika.

“Kwa hiyo akiweza kuthibitisha sifa zilizotajwa, atapewa vitambulisho ingawa wengine walitoa maoni kwamba vielezwe kuwa ni vitambulisho vya uraia kwa kuwa suala la uraia ni la Jamhuri ya Muungano na hakuna raia wa Zanzibar, kwa hiyo vitambulisho hivi vitakuwa bado ni vya Mzanzibari mkazi na si vitambulisho vya uraia wa Zanzibar," alisema.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha sera ya vitambulisho vya ukazi vya Zanzibar, hatua ambayo itasaidia kuweka kumbukumbu na kusaidia takwimu za nchi katika maendeleo.

CHANZO: Majira
 
Back
Top Bottom