Vita dhidi ya malaria si sahihi...

cabhatica

JF-Expert Member
Sep 30, 2010
1,081
480
Chanzo cha malaria ni mtu kuumwa na mbu aina ya anopheles mwenye vijidudu vya malaria (protozoa aina ya plasmodium na jamii zake). Ugonjwa huu bahati mbaya hauna chanjo mpaka sasa lakini unatibika mgonjwa anapowahi kupata matibabu sahihi.

Kwa Tanzania kumbukumbu zinaonyesha watu kati ya milioni 14 hadi 18 huugua malaria (clinical malaria cases) kwa mwaka. Wanaofariki ni kati ya 140 hadi 650 kwa kila wagonjwa 100,000.

Hatua mbalimbali zimechukuliwa na serikali pamoja na asasi zisizokuwa za kiserikali katika kupunguza vifo vinavyotokana na malaria. Kampeni ya malaria haikubaliki imezinduliwa na Rais wa nchi.

Rais ametangaza vita dhidi ya malaria. Na hapa ndipo ninapotofautiana na Rais.

Kwanini ni vita dhidi ya malaria? Kwanini isiwe vita dhidi ya mbu? Kwanini mkazo unakuwa kutumia chandarua chenye dawa? Kwanini tulazimishwe kuamini kwamba anopheles anauma tu usiku wa manane na sio wakati mwingine wowote? Maswali haya yanahitaji majibu yanayoingia akilini. Nitafafanua.

Kunapokuwa na janga la nzige mathalan, kwanini hatutengenezi vyandarua vikubwa na kuyafunika mashamba yetu ili nzige wasiweze kushambulia mazao yetu?

Malaria ni matokeo na sio chanzo cha tatizo. Kukimbilia kuweka vyandarua chumbani huku mbu wakiachiwa huru wazaliane wanavyotaka na kuuma watu jinsi wapendavyo ni kuangalia ulipoangukia badala ya ulipojikwaa. Hii haina tofauti na kuacha kuondoa kisiki ulipojikwaa na kukimbilia kutandika godoro ulipoangukia kusudi utakapojikwaa tena ukianguka usiumie. Huu ni wendawazimu.

Ukweli unaouma hapa ni kwamba watanzania tumeamua kwamba kufikiri sasa basi.

Tumeamua tuwaachie wengine wafikirie kwa niaba yetu na kila wanachotuambia tunasema hewala wala hatuna ujasiri wa kuhoji na kuhakiki hayo tunayoambiwa. Muhimbili ambayo ni hospitali ya taifa eti nako kukaibuka janga la mbu hata wauguzi wakashindwa kutekeleza majukumu yao sawasawa. Bado hatutaki kufungua macho.

Kila nikiwaza na kuwazua kuhusu kampeni zinazoendelea kuhusu namna ya kupambana na malaria, mlango wangu wa sita wa fahamu unakataa kukubali mapokeo haya.

Mosi, kama sumu inaweza kudumu kwenye chandarua kwa miaka mitano, hewa nitakayovuta kila siku kwa miaka mitano ndani ya chandarua ni nani anaweza kunihakikishia sitapata madhara ya mapafu au njia ya hewa kutokana na sumu hii.

Ninavyofahamu hakuna dawa isiyokuwa na side effect. Hata vipeperushi vinavyouzwa na dawa mbalimbali vinaonya kuhusu madhara (side effect) yanayotokana na dawa husika. Sijaona kipeperushi kinachoonyesha madhara ya dawa hii ya kwenye vyandarua inapovutwa (inhaled) au kwenye mwili kwa kugusa (contact). Anayejua atujulishe!

Pili, kwanini dawa hii inayodumu miaka mitano tunakimbilia kuiweka kwenye vyandarua badala ya kupulizia kwenye nyumba nzima na mazingira kusudi mbu wakimbie kabisa kutoka kwenye makazi ya watu ili hata mwanafunzi anayelazimika kusoma usiku au mlinzi anayekesha usiku asipate malaria? Kwanini hatufungui macho tukaona? Kwanini tunaogopa kutazama ukweli?

Tatu, takwimu zinaonyesha kwamba malaria ndio ugonjwa unoongoza kwa kuua watu wengi duniani. Kwanini ugonjwa wa kifua kikuu ambao haukaribii hata theluthi moja ya vifo vya malaria lakini tiba yake ni bure, malaria kulikoni?

Kwanini dawa zinazoaminika kutibu malaria ikiwa ni pamoja na mseto zinatoka kwenye mataifa ambayo malaria siyo tishio? Akili yangu ya kawaida inaniambia kuwa kuna maslahi ya kibiashara kwenye suala la malaria. Kwamba lazima malaria iendelee kuwepo kwasababu ni ajira kwenye sekta nzima ya tiba ya malaria. Tufanye juhudi kujua misaada ya fedha zinazotumika kufanya tafiti za chanjo ya malaria zinatoka wapi? Maabara zinazotumika kusimamia tafiti hizi zinamilikiwa na akina nani na zinapata mafungu ya kuendesha shughuli zake wapi? Vituo vyetu vya utafiti wa malaria vimefika wapi mpaka leo hii. Kuna sababu yoyote kumlipa mshahara mtafiti mpaka anastaafu bila kuwa na matokeo yanayoonekana, fedha hiyo si ielekezwe kwenye eneo lingine? Kama fedha za kuendeshea tafiti zinatoka kwenye makampuni yanayojihusisha na tiba ya malaria, ninaweza kuapa hapa kwamba chanjo ya malaria haitakaa ipatikane.

Utafiti ambao umefanyika kuhusu maisha ya mbu unaonyesha kwamba maisha ya mbu (life span) ni siku zisizozidi kumi na tano (tovuti ya wikipedia). Nini kinashindikana kumtokomeza?

Najua hatukosi visingizio. Suala la gharama ya kufanya fumigation kwenye majumba na mazingira ili kumtokomeza mbu litaonekana ni mzigo usiobebeka na tutataka wahisani wasaidie. Kwanza watume wataalamu wao, kisha watupe dawa wao na halafu watusaidie kunyunyiza. Halafu mbu wasipotokomezwa tunaamini kwamba mbu ameshindikana. Mwenye akili na afahamu.

Kwenye kumtokomeza mbu ambaye hata mkono waweza kumuua siyo suala la wahisani. Mbu wanatuua sisi na ni sisi peke yetu ndio tunapaswa kuwa wapiganaji wa mstari wa mbele kwenye vita hii. Hakuna kurudi nyuma wala kugeuka nyuma. Kama ambavyo tulipigana kufa na kupona kumngoa yule nduli amini basi tufanye hivyohivyo kwa huyu nduli mbu. Sababu ya kumpiga tunayo na uwezo wa kumpiga tunao, nia tu ndio inakosekana hapa. Tutie nia na tuanze sasa kwani tumeshachelewa sana. Gharama ambayo taifa limeingia kwa kuchelewa kumtokomeza nduli mbu ni kubwa kiasi kwamba ingetosha kuondoa nakisi ya bajeti yetu na kuacha kutegemea pengo hilo kuzibwa na wahisani. Hii ndio tafsiri sahihi ya kujitegemea.

Hebu kwa ufupi tu tuangalie hasara ambayo taifa linapata kwa kuendelea kumlea mbu. Hasara hiyo imegawanyika kwenye maeneo makubwa matatu: kupoteza nguvukazi (watu kufariki), gharama za mazishi na gharama za kutibu malaria.

Ni shilingi ngapi zinaweza kurejesha uhai wa aliyefariki kwa malaria? Kama anayefariki ndiye mtafutaji wa riziki kwa familia, maisha ya wale wategemezi wanaobaki yatakuwa sawa? Wataendelea kusoma? Kwanini watoto wa mitaani wasiongezeke? Kwanini uhalifu wa aina mbalimbali usiongezeke? Na kama ni muajiriwa, atakuwa ameondoka na utaalamu/uzoefu wake na mwajiri ataingia gharama nyingine kujaza pengo lile (recruitment cost) na pia uzalishaji au utoaji wa huduma utaathirika. Ukiamua vyote hivi kuvithamanisha itakuwa shilingi ngapi?

Tuangalie gharama zinazoweza kuthamanishwa.

Kwa wastani takwimu za hapo juu zinaonyesha kuwa kwa mwaka watu wanougua malaria ni milioni 16 na wanaokufa ni 63,200.

  • Kama gharama ya matibabu (usafiri, kumuona dr, maabara, dawa) tuseme ni shilingi elfu tano kwa kila case, basi kwa mwaka watanzania wanatumia bilioni 80 kujitibu peke yake bila kujali kama utapona au la
  • Kama gharama za mazishi (gharama za kusafirisha mwili, nauli za wanandugu, michango ya rambirambi, gharama za jeneza nk) tukikadiria shilingi milioni moja, basi kwa mwaka ni bilioni 63.2
  • Serikali iliweka bajeti ya USD milioni 76 kwa ajili ya kupambana na malaria kati ya 2002 na 2007 kupitia mpango wake wa MMTSP, hii ni sawa na shilingi bilioni 22 kwa mwaka. N.k

Kuna gharama zaidi kumlea mbu kuliko kumtokomeza. Tuanze sasa vita dhidi ya MBU. Tafakari !

Source ya takwimu: Tovuti ya Wizara ya Afya
 
Back
Top Bottom