Vigogo wamega maeneo ya vijiji Pwani

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Vigogo wamega maeneo ya vijiji Pwani Thursday, 20 January 2011 20:55
Julieth Ngarabali, Pwani
Mwananchi

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Anna Tibaijuka sasa atalazimika kutumia nguvu za ziada kupambana na wavamizi wa ardhi, kufuatia zaidi ya vigogo kumi serikalini kuhusishwa katika uvamizi wa eneo la ekari 60,000 mkoani Pwani.

Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani zimeeleza kuwa vigogo hao wakiwemo mawaziri, wamepata maeneo hayo kinyume na taratibu.

Nakala ya hati miliki ya baadhi ya maeneo hayo iliyopatikana jana kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani, imeonyesha kuwa wengi wa vigogo hao (majina tunayo), walitumia njia za udanganyifu kupata maeneo hayo.

"Kamati ya Ulinzi na usalama imebaini utata wa miliki za eneo hilo pamoja na ina wasiwasi iwapo majina yaliyotajwa ndiyo wamiliki halisi," alisema Mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani, Hajjat Amina Mrisho.

Aliongeza,"Wote waliopimiwa maeneo hayo hawakufuata taratibu, hivyo umiliki wao hautambuliki na siyo halali".

Habari zinasema kuwa uongozi wa mkoa wa Pwani umegundua tatizo hilo baada ya kuzuka kwa mgogoro wa mipaka katika vijiji vitatu vya Kitomondo, wilayani Kibaha Mafizi na Mihugwe wilaya ya Kisarawe.

"Baada ya mzozo huo, iliilazimu kamati nzima ya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa chanzo chake ambapo iligundulika kuwa kuna mwekezaji mmoja ambaye alijisajili katika kijiji cha Kitomondo akidai kuwekeza katika kilimo na kwamba ndiye anayeendelea kumega maeneo mengine ya vijiji jirani bila kuwashirikisha viongozi," kilisema chanzo chetu cha habari.

Katika ufuatiliaji huo iligundulika kwamba mtu huyo tayari alishajichukulia zaidi ya ekari 60,000 kwa madai kwamba ni za chama cha ushirika wa kilimo Kibaha (CUKK) na kwamba wajumbe wa ushirika huo ni viongozi mbalimbali ngazi za juu wakiwemo mawaziri, wakuu wa wilaya, mikoa, wabunge na wakurugenzi wa benki kadhaa nchini.

Inadaiwa kuwa eneo hilo tayari limegawanywa kwa vipande vya ukubwa wa ekari 100 kila kimoja, huku wamiliki wake wakitajwa kwa majina ya vigogo hao na kwa mujibu wa taarifa hizo imechorwa ramani na hati miliki feki kuhalalisha mgawo huo.

Uchunguzi huo wa awali ndiyo uliwezesha uongozi wa mkoa wa Pwani kubaini "mchezo mchafu", huku baadhi ya vigogo wa ngazi za juu serikalini wakiwemo mawaziri wakituhumiwa kutumia nafasi zao kuwatapeli wananchi kwa kumega maeneo ya vijiji hivyo.

Baadhi ya watu wanaotajwa kutumia nyadhifa zao kutapeli wananchi na kuchukua maelfu ya ekari katika wilaya hizo ni pamoja na mfanyakazi wa idara ya ardhi makao makuu (jina tunalo) ambaye amechukua shamba katika kijiji cha Kitomondo lenye ukubwa za ekari 3,000 isivyo halali.

Mwingine ni Ofisa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo (jina tunalo) ambaye yeye pamoja na kutumia majina ya vigogo ikiwemo la Rais Jakaya Kikwete, pia alikutwa akiwa na hati miliki za ardhi zenye picha na majina ya viongozi wengine wakubwa.

Wakazi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti waliiambai Kamati ya Ulinzi na usalama ya mkoa huo ilipowatembelea kuwa hawana tarifa zozote za kuwepo kwa vigogo hao katika vijiji hivyo na kwamba wanashangaa kumegwa kwa maeneo yao.

Wanakijiji walisema watu ambao majina yao yanasomeka kwenye ramani hiyo pamoja na hati hizo hawawatambui kwani hawajawahi kufika kijijini hapo kuomba maeneo na kwamba hata kama wangepewa isingekuwa zaidi ya ekari 50.

Kufuatia maelezo hayo, Kamati hiyo ya ulinzi na usalama ikatoa tamko kwamba "maeneo yote yaliyopimwa katika vijiji hivyo hayapo na pia wale wote waliopewa maeneo hayo pia hawatambuliki kisheria kwani hawajafuata utaratibu wa kumiki ardhi".

"Kamati ya ulinzi na usalama imepitia kila hatua na imejiridhisha waliopo katika ramani na katika hati miliki ambazo sisi tumebaini ni feki hatuwatambui,"alisema Hajjat Amina Mrisho.

Kadhalika Hajjat Mrisho alielekeza kukamatwa kwa Ofisa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na yule wa Wizara ya Ardhi makao makuu ili waweze kusadia kupatikana kwa ukweli kuhusu suala hilo.


"Tulichogundua kwa baadhi ya majina yaliyopo katika ramani ni huyu mtu katumia ujanja wa kutapeli kwa kutumia nyadhifa ya viongozi wakubwa Serikalini ili apore ardhi,Kamanda wa Polisi,afisa usalama Taifa ondokeni na watu hawa moja kwa moja watatusaidia zaidi".

Sakata la utapeli wa mashamba ya wanavijiji limeshika kasi katika wilaya za Kisarawe, Mkuranga, Rufiji, Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja zaidi ya kesi nne za utapeli wa mashamba makubwa zimeripotiwa.

Kesi kubwa ni ile ya wilaya ya Bagamoyo ambayo matapeli walifika na kuchukua shamba la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kujimilikisha isivyo halali na kisha kuanza kuyauza kwa bei kubwa kwa wakazi wa jiji la Dar esalaam

Mbinu kubwa wanayoitumia wajanja hao ni kupitia kauli mbiu ya Taifa ya Kilimo Kwanza ambapo watu hujitokeza na kujifanya kuunda ushiriki wa kilimo na kuchukua na kuhodhi mashamba makubwa wakitumia majina ya viongozi waandamizi wa serikali kuu na kisha kuyauza mashamba hayo kwa bei ya kuruka.
 
Back
Top Bottom