Vigogo BoT wakatwa posho kwa asilimia 75

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Date::12/25/2008
Vigogo BoT wakatwa posho kwa asilimia 75

Ramadhan Semtawa
Mwananchi

VIGOGO ndani ya Benki Kuu Tanzania (BoT), sasa wamebanwa zaidi, kufuatia hatua ya uongozi wa benki hiyo, kupunguza posho na marupurupu yao kwa asilimia 75.

Hatua hiyo, imekuja siku kadhaa tangu Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, apigie marufuku matumizi binafsi ya magari ya kifahari aina ya Mercedes Benz.

Duru za habari za kuaminika kutoka ndani ya BoT na ambazo zimethibitishwa na Profesa Ndulu , zilisema posho zilizopunguzwa ni pamoja na ile maarufu kama '105'.


Akizungumzia uamuzi huo, Gavana Ndulu alisema unalenga katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi wote wa chombo hicho muhimu.

"Hiyo posho ya ('105'), ikimaanisha Sh105,000 na nyingine zimepunguzwa kwa asilimia karibu 75," alifafanua Profesa Ndulu.

Alisema katika siku za hivi karibuni, yalijitokeza malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa chini, kuhusu namna baadhi ya watu wanavyolipwa posho na marupurupu makubwa.

Alisema ili kuondoa malalamiko hayo, benki imeona ni vema posho hizo zikapunguzwa kwa asilimia 75.


"Utaona uamuzi huo pia unalenga kuondoa malalamiko na kuleta utengamano ndani ya benki, kwa kumridhisha kila mmoja," alisisitiza Profesa Ndulu.

Profesa Ndulu ambaye amekuwa akijitahidi kuisafisha BoT na kurejesha imani yake kwa umma, alisema posho na marupurupu yaliyopunguzwa, sasa yataelekezwa katika mishahara ya wafanyakazi wengine.

Alisema BoT imekuwa katika mchakato wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake wote na kwa hiyo sehemu hiyo ya posho itaongeza nguvu katika kufanikisha mpango huo.

"Tumeamua sehemu hiyo ya posho ambayo tumepunguza, sasa ielekezwe katika mishara ya watumishi wote, ili kuboresha maslahi," alifafanua.

Wakati hayo yakiendelea habari zaidi zilisema kumekuwepo na mkakati mwingine wa ulaji miongoni mwa baadhi ya maofisa wa BoT na kwamba mkakati huo ni wa kujiwekea ratiba za vikao ili kujilipa kiasi posho kwa muda mfupi.

Katika duru za ndani ya BoT, zilisema mara nyingi vikao hivyo vya wakubwa vinafanyika ndani ya benki hiyo.


Kwa mujibu wa habari hizo, tayari malipo ya posho hizo zinazowanufaisha baadhi ya wafanyakazi, yamezua malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wengine wa BoT.

Inasemekena posho hizo zimekuwa kama moja ya miradi ya vigogo na vijana wao ndani ya BoT kujipatia kipato cha ziada kwa mwezi.

"105 ni posho zinazolipwa wakati watu wakijadili miradi, lakini ukweli ni kwamba ni mradi wa watu kujipatia kipato cha ziada," zilidokeza duru huru.

Kwa ufafanuzi, duru hizo zilisema, chini ya utaratibu wa '105' watendaji wa idara na baadhi ya wenye mafungumano na wakuu wa idara wamekuwa wakijiingizia fedha kwa kuitisha vikao hata visivyokuwa vya msingi na kulipana kiasi hicho cha fedha katika kila kikao.

Vyanzo vya habari vilisema wakati mwingine baadhi ya wakuu wa idara, huamua kuitisha kikao hata cha muda dakika 20, ili kujihalalilishia posho hiyo.

"Unaweza kumuona mkuu wa idara anaita vijana, anakaa nao kwa muda wa nusu saa tu kisha wanamaliza eti wameshajadili mradi, kisha kulipana '105'," kilisisitiza chanzo hicho.


BoT ambayo ni mhimili mkuu wa mwelekeo wa uchumi wa nchi, katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi.

Tuhuma za ufisadi ndani ya EPA kwa sasa ndizo ambazo zimekuwa zikijadliwa kufuatia kufanyika uchunguzi huru uliofanywa na Kampuni ya Ernst & Young, ambao matokeo yake yametoka na kubaini ufisadi wa zaidi ya sh 133 biliioni za umma.
 
Hii isiwe kwa vigogo wa BOT tu, iwe kwa wote.

Board members wa boards mbalimbali za idara na mashirika; na vigogo wengine kwenye wizara.

Haba na haba hujaza kibaba.....
 
Back
Top Bottom