Vifo wakati wa uzazi vyaongezeka

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
TATIZO la vifo vya akinamama wakati wa uzazi limezidi kuwa kubwa nchini ambapo sasa kati ya 100,000, wanawake 454 hufa kila siku sawa na wanawake 7,700 kila mwaka.

Hayo yamebainishwa katika ripoti ya ukaguzi wa tatizo hilo uliofanywa kwa mujibu wa sheria na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyowasilishwa Dar es Salaam jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Akiichambua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alisema, ukaguzi wa CAG umeibua mambo mengi kuhusu tatizo la vifo vya kinamama ambapo ukubwa wake umechangiwa na udhaifu katika kutatuliwa kwake.

Cheyo alisema, ripoti hiyo ilibainishwa kuwa, kuna udhaifu katika ufuatiliaji wa mipango na mikakati ya kudhibiti tatizo hilo, kutokutolewa kwa elimu hasa kwa akinamama juu ya masuala ya afya ya uzazi na kutokuwepo kwa taratibu za kufanya tathmini juu ya maendeleo ya afya ya uzazi.

Aidha, alisema ripoti hiyo imeonyesha udhaifu kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika vipaumbele vyake wakati wa bajeti ambapo tatizo hilo limekuwa likipatiwa bajeti finyu, lakini pia kumekuwana udhaifu mkubwa katika eneo la takwimu zake.

Alisema, Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2000 lilitoa takwimu kuhusu vifo vya kinamama nchini kufikia 1,500 kati ya kinamama 100,000 wakati Wizara ilionesha ni kinamama 529 kati ya 100,000, ndiyo hufa.

Pia alisema mwaka 2005 WHO ilitoa takwimu kuwa tatizo hilo limeshuka nchini hadi kufikia akinamama 500 kati ya 100,000 ndio wanaokufa wakati wizara ilionyesha kuwa tatizo limeongezeka na kufikia akinamama 657 kati ya 100,000 wanaopoteza maisha.

“Tumeona tulijadili suala hili linahusu uhai wa watu, ripoti hii imeonesha mambo ya kushtusha yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuokoa maisha ya kinamama hawa, naomba na ninyi wizara mseme mnaichukuliaje ripoti hii,” alisema Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP).

Akichangia mjadala wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alikiri kuwa tatizo la vifo vya kinamama wakati wa uzazi ni kubwa na ndiyo maana wizara yake inatekeleza mpango wa miaka 10 ambao utalitatua tatizo hilo.

Alisema mpango huo unajumuisha kumaliza changamoto zinazoikabili afya ya uzazi ambazo ni uchache wa vituo vya afya, upungufu wa madaktari na watoa huduma za afya na umbali wa kufikia huduma hizo za afya.

Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa alikiri kuwa tatizo la takwimu bado ni changamoto inayoikabili wizara kwa kuwa hakuna vifaa vinavyotunza takwimu za matukio yote yanayohesabiwa yanayohusu afya ya uzazi.
 
Back
Top Bottom