Uwezo mdogo kwa wanasheria wetu waligharimu taifa

mzambia

JF-Expert Member
Dec 31, 2010
885
60
Send to a friend

Claud Mshana
UZOEFU na uwezo mdogo wa Mawakili na Wanasheria wa Serikali katika kuangalia mikataba ya kimataifa umegundulika kuwa ndio unaoifanya Tanzania kuingia katika hasara ya mara kwa mara inayosababisha kupoteza mabilioni ya fedha.

Mawakili hao pia wanadaiwa kusindwa kutetea maslahi ya taifa kwenye mikataba ya madini na hata kwenye baadhi ya masuala ya uwekezaji ambayo serikali imejikuta ikichelewa kupata faida wakati wawekezaji wakineemeka.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa wanasheria wengi Serikalini, hawana uzoefu na uwezo wa kutosha kufahamu masuala ya kisheria na hasa kwenye mikataba ya kibiashara baina ya Serikali na kampuni ama mashirika ya kimataifa.

Hali hiyo ya ukosefu wa wanasheria waliobobea katika uzoefu na taaluma hiyo muhimu unatokana na wimbi la wataalamu wa sheria kukimbilia katika kampuni binafsi za uwakili kutokana na maslahi kiduchu.
Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema aliiambia Mwananchi Jumapili, kwamba ofisi yake inakabiliwa na tatizo hilo na kwamba imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha inawajengea uwezo kisheria juu ya masuala ya mikataba.

“Nakubali wakati mwingine kunakuwa na upungufu wa weledi na uadilifu kwa baadhi ya wanasheria katika ofisi yangu, tumeyabaini mapungufu hayo na tunayafanyia kazi siku hadi siku,” alisema Jaji Werema ambaye ni mteule wa Kwanza wa Rais Jakaya Kikwete.

Serikali imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za kisheria katika masuala ya mikataba na mashirika au kampuni za wawekezaji ambapo hivi karibuni, kampuni ya kufua umeme ya Dowans imeshinda kesi dhidi ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), na kutakiwa kulipwa Sh185 bilioni.

Jaji Werema alifafanua kuwa serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) wanaendesha programu ya pamoja ya mafunzo kwa wanasheria na mawakili wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
“Tunawafundisha mambo mengi tu kama masuala ya uchumi, sheria ya fedha, kodi, masuala ya umeme ili wanapokuwa katika mazungumzo na wawekezaji kwa ajili ya kusaini mikataba na wawekezaji hao, wawe na ufahamu wa kutosha wa masuala mbalimbali, na si sheria peke.”

Jaji Werema aliongeza kuwa, “Zamani wanasheria wetu wengi walikuwa hawajui mambo mengi nje ya sheria, hivyo walikuwa wakikwepa wanapopelekewa mahesabu na kusisitiza kuwa wao wanahusika na sheria pekee, lakini kwa mafunzo haya, watakuwa na uwezo na ufahamu zaidi ya sheria.”
Mwananchi Jumapili imebaini kuwa wahitimu wengi wa sheria ambao wana uwezo mkubwa kitaaluma, wanakwepa kufanya kazi katika ofisi hiyo kutokana na maslahi duni.

Vyanzo vyetu vya habari vilibainisha kuwa, mishahara yao inaanzia Sh 300,000 kwa mujibu wa viwango vya mishahara vya serikali.
Kiwango hicho ambacho hakikidhi mahitaji yao katika wakati huu wa kupanda kwa gharama za maisha, huwafanya wanasheria wengi kufikiria kujiunga na kampuni binafsi za uwakili ambazo huwa zinalipa vizuri.
Kuhusu suala hilo, Jaji Werema alisema elimu ya chuo kikuu peke yake haitoshi kumfanya mtu awe na uwezo mkubwa kazini, bali mafunzo ya mara kwa mara kulingana na mahitaji ya kiofisi ndio humfanya awe na weledi mkubwa kikazi.

“University' (chuo kikuu) ni elimu ndogo tu anayopata mfanyakazi, lakini ndani utajifunza mambo mengi, kwa mfano chuoni watu wanajifunza 'contracts law' (sheria ya mikataba), lakini ni lazima mtu ajue pia namna ya kuongea na kushauriana wakati wa kuingia mikataba, mambo ambayo hayafundishwi vyuoni,” alifafanua Jaji Werema.
Mtaalamu wa masuala ya sheria, Tundu Lissu aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa jambo hilo ni la hatari kwa taifa.
“Unapokuwa na watendaji hafifu, ina maana kwamba rais anapata ushauri hafifu, mawaziri wanapata ushauri hafifu na idara zote zinapata ushauri hafifu, jambo hili ni la hatari kwa taifa, ndio chanzo cha mikataba mibovu na madhara yake, sote tunayafahamu,” alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), aliongeza kuwa "Namna ya kutatua tatizo hilo, si kwa serikali kuwajengea uwezo wanasheria wake na kwamba wanatakiwa kuajiri watu wenye uwezo mkubwa na kuhakikisha serikali inajenga mazingira mazuri yatakayowafanya walioko katika ofisi hiyo, waendelee kuwepo."

Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni alifafanua, “Serikali iwaboreshee maslahi yao, kwanini mtu afanye kazi ambayo haimsaidii katika kujenga maisha yake, ni lazima serikali ihakikishe inaweka vivutio kwa wafanyakazi wake waendelee kubaki na kufanya kazi kwa amani.”
Kuhusu maslahi, Jaji Werema alisema "Kazi ya uwakili ni wito na kwamba serikali inawalipa watumishi wake kutokana na makusanyo ya kodi."

Aliongeza kuwa, kuwa kuna mafao mazuri zaidi kwa wafanyakazi wa serikali, kuliko kwa wale wanaokimbilia kampuni binafsi za uwakili.
“Ukitaka uwalipe kama wanavyolipwa kwenye kampuni binafsi, utawalipa shilingi ngapi? Serikalini kuna faida nyingi ambazo mtu atazipata ikiwa ni pamoja na usalama wa kazi, huko nje watu wanafukuzwa kazi hovyo hovyo," alisema Jaji Werema na kuongeza:

"Kinachotakiwa hapa ni kufanya kazi kwa kuridhika, serikali inaweza kuwalipa vizuri kama pia makusanyo ya kodi yatakuwa mazuri.”
Katika hatua nyingine, Jaji Werema alisema pia wanapata madai ya baadhi ya mawakili wa serikali wanaoteuliwa kuwatetea watuhumiwa wasio na uwezo wa kutafuta mawakili kwamba wanashindwa ovyo kesi kutokana na uwezo mdogo na mengineyo.

Werema alisema mawakili wote wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa maadili ya kanuni ya kazi yao yanavyowataka kufanya.
Alisema wakili anayeenda kinyume na maadili na wajibu wa kazi zake, anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Felix Kibodya alikiri kuwepo kwa malipo kidogo kwa mawakili wanaoteuliwa kuwatetea watu wasio na uwezo katika kesi zao na kwamba ni wajibu wa kila wakili kutekeleza wajibu wake.
“Ni kweli tumekuwa tukipokea malalamiko mengi sana kuwa mawakili wetu hawawatetei vizuri watuhumiwa ambao hawana uwezo wa kuwalipa, lakini mara nyingi tunapofanya uchunguzi, tunagundua kuwa tatizo linakuwa kwa watuhumiwa wenyewe,”

Kibodya aliongeza kuwa, “Hata hivyo kuna kesi chache ambazo ni kweli mawakili wanakuwa wana makosa na inapotokea hivyo, musika anaitwa katika kamati zilizopo katika ngazi mbalimbali na kama atabainika kuwa alitenda kosa kubwa, basi atanyang’nywa hata leseni ya kazi.”
SOSI: MWANANCHI LEO.
 
Back
Top Bottom