Mlalahoi
JF-Expert Member
- Aug 31, 2006
- 2,182
- 883
I said it yesterday (angalia hapa https://www.jamiiforums.com/jukwaa-...lal-alikuwa-aondoke-ccm-7.html#post986362),na inaelekea jamaa wa Majira wana mtizamo kama huo.
CHANZO: Majira
Uteuzi wa Bilal neema kambi ya Lowassa 2015
Wednesday, 14 July 2010 04:56
Na Tumaini Makene
SIKU tatu baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukamilisha uteuzi wa wagombea wake wa nafasi za juu katika uchaguzi mkuu ujao, imefahamika kuwa hatua hiyo ni kicheko kwa moja ya makundi yanayokamia kupata urais mwaka 2015 kwa kuwa limefanikiwa kupanga safu yake.
Uchaguzi wa mgombea wa urais wa CCM Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein na uteuzi wa mgombea mwenza wa urais wa muungano, Dkt. Mohamed Gharib Bilal umeelezwa na vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya CCM, kuwa ni moja ya karata za muhimu katika mipango ya kundi hilo.
Kundi hilo linampigia chapuo Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Bw. Edward Lowassa kuingia ikulu baada ya rafiki yake, Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo pamoja na baadhi ya wadadisi wa masuala ya siasa nchini, kundi hilo linaloelezwa kuwa chini ya wafanyabishara na wanasiasa maarufu nchini, kwa muda mrefu sasa limekuwa likijipanga kwa njia nyingi, ikiwemo ya kuweka safu ndani ya serikali na CCM, ili muda muafaka utakapofika lisiwe na kikwazo cha kutimiza lengo lake.
Kundi hilo linatajwa kujipenyeza na kuwa nyuma ya Dkt. Bilal katika harakati zake za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, na kuwa huo ulikuwa mkakati wa kujiweka karibu na mmoja wa watu waliokuwa na mvuto na nafasi ya kupata nafasi hiyo.
"Mpaka sasa haieleweki kundi hilo lilijitokeza vipi na kudandia safari ya Dkt. Bilal, maana tayari alikuwa maarufu na alikuwa akikubalika wala hakuhitaji nguvu yao na fedha. Lakini kinachoonekana kundi hili lilitaka kutisha na kuonesha ubavu wake kwa mwenyekiti wa chama ambaye alionekana kuwa nyuma ya harakati za Dkt. Shein.
"Kwa vyovyote vile kundi hili lenye wafanyabiashara walioamua kuingia siasa kwa ajili ya maslahi yao na baadhi ya wanasiasa likiwa na mtandao mkubwa bara na visiwani, linatumia kila aina ya mikakati, mizuri au michafu kujipanga kwa ajili ya urais wa Tanzania mwaka 2015, hivyo wanawekeza katika kila fursa inayojitokeza," kilisema kimoja kati ya vyanzo vyetu.
Hata baada ya Dkt. Bilal kukosa nafasi hiyo ambayo amekuwa akiitafuta tangu mwaka 2000, kundi hilo limeelezwa kuwa lilijipanga upya na kuibua taarifa za vitisho juu ya kuwapo mgawanyiko, ili kushinikiza ateuliwe kuwa mgombea mwenza na hatimaye makamu wa rais.
Mbali ya kuwa anaelezwa kuwa mtu mwenye msimamo, Dkt. Bilal anaweza kutumika kurudisha fadhila, huku kundi hilo likifurahia uteuzi wake kwa sababu mpaka mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 70, umri ambao hautamwezesha kufikiria kupigania nafasi ya kuteuliwa mgombea urais wa CCM.
Bila ya kufafanua, moja ya chanzo chetu cha habari kutoka kambi ya kundi hilo kililiambia Majira, "nafasi hiyo itatufaa kwa mwaka 2015...
Imeelezwa kuwa mbinu ya kuhakikisha anapatikana makamu wa rais (iwapo CCM ikishinda uchaguzi) ambaye hatakuwa na ushawishi wa kuwania nafasi ya urais kupitia CCM, ilikuwa ni sababu ya kumuogopa Dkt. Ali Mohamed Shein iwapo angelibaki katika nafasi ya makamu wa rais kwa kipindi kingine.
Dkt. Shein alionekana kuwa kikwazo kwa sababu angelikuwa amekaa katika nafasi hiyo kwa miaka 15 na kumpatia uzoefu wa kutosha kuwa rais wa nchi, hivyo ikiongezewa na kitu kinachosemwa kuwa '2015 itakuwa zamu ya Zanzibar' ni wazi makundi yote yanayotarajia kusaka nafasi hiyo yasingekuwa na hoja pingamizi dhidi ya uteuzi wa Dkt. Shein.
Chanzo kingine cha habari kimelieleza Majira kuwa mkakati huo uliofanywa kwa uteuzi wa nafasi za juu unaendelea hata ngazi ya ubunge, udiwani na nafasi mbalimbali ndani ya chama ili kufungua njia ya 2015 kwa Bw. Lowassa.
CHANZO: Majira