Utata wa mkataba wa Kampuni ya Karamagi wafikia kikomo

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,462
21,334
Utata wa mkataba wa Kampuni ya Karamagi wafikia kikomo
Na Ramadhan Semtawa
HATIMAYE serikali imemaliza utata wa mkataba wa Kampuni ya Tanzania International Container Service (Ticts), baada ya kuiondolea ukiritimba wa shughuli za kupakua shehena na makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.
Uamuzi huo umefikiwa siku chache baada ya gazeti hili kuripoti kwa mara ya kwanza, kuundwa timu ya mawaziri wanne chini ya Dk Shukuru Kawambwa (Miundombinu), kuibana Ticts ili kuondoa ukiritimba na kuuza asilimia 25 ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku serikali ikijiandaa kutoa ripoti kamili ya utekelezaji kuhusiana na suala hilo Julai 30, mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo alilithibitishia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuhusu uamuzi wa kutaka kuondoa ukiritimba huo wa TICTS.
Hata hivyo, uamuzi huo wa serikali bado haujaanza kutekeleza azimio la Bunge la Aprili 25 katika mkutano wa 11 mwaka jana lililotokana na hoja binafsi ya mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyeitaka serikali kufuta nyongeza ya mkataba kwa Ticts.
Waziri wa zamani wa Nishati na Madini Nazir Karamagi, anamiliki asilimia 30 ya hisa za Ticts kupitia Kampuni ya Harbours Investment Limited (HILI), huku Kampuni ya Hutchison Port Holdings (HPH) ya Hong Kong, China ikimiliki asilimia 70.
"Ndiyo, lengo la kuondoa ukiritimba ndilo jambo kubwa linalopaswa kufanyika," alithibitisha Chambo kwa kifupi na kusema maelezo kuwa wakati huo alikuwa katika mkutano.
Azimio hilo la bunge kutaka kusitishwa kwa mkataba wa TICTS, lilipitishwa karibu na wabunge wote isipokuwa Karamagi, aliyetoa sauti bungeni ya 'siyo' baada ya Spika kuhoji wabunge wanaoafiki na wasioafiki.
Mkataba huo uliongezwa na serikali Desemba 30, mwaka 2005 na kufikia miaka 25 badala ya miaka 10 ambao ulikuwa unaisha mwaka 2010.
Nyongeza ya mkataba kwa miaka 15, ilifanywa kupitia barua Na. TYC/R/160/32 ya Septemba, 2005, iliyoandikwa na kutiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Basil Mramba, ambayo pamoja na mambo mengine, ilimtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ahakikishe muda wa mkataba unaongezwa kuwa wa miaka 25.
Hata hivyo, ingawa serikali haijatekeleza azimio hilo, duru zaidi za vyanzo huru vya habari kutoka ndani na nje ya serikali na baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Miundombinu, vilisema hadi sasa hatua ya kuondolewa ukiritimba imejadiliwa kwa kina na kukubaliwa katika mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, ingawa serikali imeshindwa kuvunja mkataba huo na TICTS kama bunge lilivyoagiza, bado uamuzi huo wa kuondoa ukiritimba utapunguza nguvu za kampuni hiyo kwa sehemu kubwa kiutendaji.
Vyanzo hivyo huru viliongeza kwamba, katika mazungumzo hayo ambayo yalimhusisha bosi wa Ticts kutoka Hong Kong, serikali imeweza kuibana kampuni hiyo katika kipengele cha mkataba kwa kutumia udhaifu wa kiutendaji ambao uko chini ya viwango.
Miongoni mwa vipengele vilivyotumika kuibana Ticts ni pamoja na uwezo wake mdogo wa kupakua makontena kutoka mizunguuko 25 (kitaalamu) kwa saa hadi 18, kinyume na mkataba.
"Kwa hiyo, kwa kutumia mkataba wenyewe serikali iliweza kuibana Ticts ikiwa ni pamoja na kuangalia udhaifu wa kiutendaji chini ya viwango vya mkataba," kilifafanua chanzo kimoja huru kutoka Kamati ya Bunge ya Miundombinu.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba, timu hiyo ya mawaziri pia ilieleza bayana kwamba, Rais Jakaya Kikwete, amekuwa akichukizwa na utendaji mbovu na kuzorota kwa shughuli za kiuchumi bandarini, hivyo aliamua ukiritimba huo uondolewe.
"Pia Ticts waliambiwa kabisa kwamba, bwana mkubwa (Rais) anataka ukiritimba huo uondolewe mara moja kwa sababu unazorotesha utendaji kazi wa bandari," kilifafanua chanzo hizo.
Kwa mujibu wa chanzo kingine huru, mbali ya kubanwa katika upakuaji wa mizunguuko kutoka 25 hadi 18 serikali pia ilitumia udhaifu wa vitendeakazi bandarini ambavyo vinamilikiwa na Ticts hadi kuamua kutumia vya Mamlaka ya Bandari (TPA).
Hata hivyo, ingawa serikali imechukua uamuzi huo bado itakuwa imeshindwa kutekeleza Azimio la Bunge la Aprili mwaka jana, ambalo liliitaka ivunje mkataba huo mara moja.
Mkataba huo uliongezwa kwa miaka kumi hadi 25 ambao ulifanywa katika serikali ya awamu ya tatu kwa nguvu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ulipingwa na wabunge baada ya mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi, kuwasilisha hoja binafsi.
Hoja hiyo binafsi ya Zambi iliungwa mkono na bunge kwa pamoja likaazimia serikali itengue mkataba huo mara moja kuhakikisha Ticts inaondolewa ukiritimba.
Nyongeza ya awamu ya pili ya mkataba wa Ticts iliwahi kuibua mjadala mapana bungeni, hadi Karamagi kutakiwa na bunge athibitishe kama nyongeza ya awamu ya pili ya mkataba huo ilikuwa na baraka za Baraza la Mawaziri.
Baadaye Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alimsafisha Karamagi ambaye ni mbunge wa Bukoba Vijijini, kuhusu kauli yake kwamba uamuzi wa kuongezewa muda wa mkataba kati ya serikali na Ticts.
Hata hivyo, Zambi alipingana na kauli hiyo akisema uamuzi huo wa Baraza la Mawaziri ulikiuka sheria.
Zambi ambaye Aprili 24, jana aliiwasilisha hoja hiyo alisema si kweli kwamba Baraza la Mawaziri halifayi makosa.
Akifafanua zaidi, alisema kama kweli baraza hilo liliamua kuhusu mkataba huo, basi lilikiuka Sheria ya Manunuzi Serikalini namba 21 ya mwaka 2004, kauli ambayo baadaye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alithibitisha nyongeza ya pili ya mkataba huo ilikuwa ya kifisadi.
CAG katika taarifa yake ya ukaguzi ulioishia Juni 30, mwaka 2007, ilitaja kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi serikalini katika mkataba wa TICTS.
Takwimu za mwaka jana zinaonyesha msongamano wa mizigo uliongezeka na kufikia asilimia 88.7 ikilinganishwa na kiwango cha kimataifa cha asilimia kati ya 50 na 60.
Tayari TPA imetoa taarifa mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ikieleza namna ambavyo Ticts ilivyoshindwakazi na kudhofisha utendaji na kuifanya imezwe na Bandari ya Mombasa.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom