Elections 2010 Ushindi wa Kishindo huu waja kwa CCM

Kabwela

Member
Feb 11, 2008
76
5
Katika hatua nyingine, wagombea wawili wa udiwani walizimia kwa nyakati tofauti baada ya kusomewa matokeo ya kura zilizopigwa, huku yakionyesha wao hawakupata kura hata moja licha ya kujipigia kura.
Wagombea hao wanaotoka Kata ya Chihanga, wametajwa kwa majina kuwa ni Elisi Kitendya na Rosemary Kaka, ambapo kura zilihesabiwa kwa zaidi ya saa 12.



Habari kamili hii hapa chini

Tanzania Daima: jumapili, 25 julai 2010

CCM ni kufa au kupona
• Wagombea udiwani wawili wazimia

na Mwandishi wetu


amka2.gif
HALI ya mwenendo wa kampeni za ubunge na udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imefikia pabaya, Tanzania Daima Jumapili imebaini.
Hali ya kutoaminiana kati ya wagombea katika maeneo mbalimbali imeendelea kutikisa huku baadhi yao wakilalamika kukosa imani na wasimamizi wa uchaguzi.
Habari zilizopatikana kutoka mkoani Dodoma, zinasema hali katika Jimbo la Dodoma Mjini imeendelea kuwa tete baada ya wagombea 18 wa ubunge kati ya wagombea 19 waliopo kulalamika kwamba hawana imani na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ambaye pia ni Katibu wa CCM wa wilaya, David Mzuri.
Malalamiko hayo na tuhuma za wagombea yaliwasilishwa kwenye uongozi wa CCM mkoa juzi usiku, baada ya kutoka kwenye kampeni, ambapo uongozi wa mkoa ulichukua hatua za kumpa uhamisho wa ghafla usiku huo huo katibu wa CCM wa wilaya na kumpeleka mkoani Morogoro ili kupisha uchunguzi.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Kapteni mstaafu John Balongo, alisema uchunguzi dhidi ya katibu huyo utafanyika kwa muda wa siku saba, ambapo nafasi yake sasa inakaimiwa na ofisa kutoka Makao Makuu ya CCM, Bernard Nduta.
Kapteni Balongo alisema walipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo kuwa mgombea mmoja amekuwa akifanyiwa kampeni na katibu huyo pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, Denis Bendera.
Mmoja wa wagombea hao Haidary Gulamali alisema ana ushahidi kuhusu katibu na mwenyekiti wake kumpigia kampeni kigogo (jina tunalo) katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Dodoma Mjini.
Wagombea wengine walisema hawajapendezewa na kitendo hicho cha viongozi wa wilaya kumpigia kampeni mgombea mwenzao kutokana na taarifa walizozipata kutoka kwa wapiga kura wao.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma, Eunice Mmari, alisema ofisi yake imepokea malalamiko mengi kutoka maeneo mbalimbali kuhusu kigogo huyo.
Katika hatua nyingine, wagombea wawili wa udiwani walizimia kwa nyakati tofauti baada ya kusomewa matokeo ya kura zilizopigwa, huku yakionyesha wao hawakupata kura hata moja licha ya kujipigia kura.
Wagombea hao wanaotoka Kata ya Chihanga, wametajwa kwa majina kuwa ni Elisi Kitendya na Rosemary Kaka, ambapo kura zilihesabiwa kwa zaidi ya saa 12.
SHINYANGA
WAGOMBEA 16 wa ubunge katika majimbo ya Bukombe na Mbogwe, mkoani Shinyanga juzi na jana walisusia kufanya kampeni zao kwa madai uongozi wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo unawabeba baadhi ya wagombea, hali iliyosababisha uongozi wa chama mkoani humo kuwasimamisha kusimamia kampeni Katibu wa CCM wa wilaya na msaidizi wake.
Habari zilizopatikana jana kutoka wilayani humo na kuthibitishwa na Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Mohamed Mbonde, zilidai kuwa katibu wa chama hicho wa Wilaya, Mberito Magova na msaidizi wake, Novatus Kibati, walisimamishwa kazi ya kusimamia uchaguzi huo katika majimbo ya Bukombe na Mbogwe.
Katika kikao hicho, wagombea hao waliandika barua za kujiuzulu huku wakiwataka Emmanuel Luhahula, agombee peke yake katika Jimbo la Bukombe na Ofisa Usalama wa Taifa wa Wilaya ya Geita, Agustino Masele, agombee pekee Jimbo la Mbogwe, kwa madai ya kuwa uongozi huo wa wilaya uliwaandalia mazingira ya ushindi, ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi peke yao ya kueleza sera wakati wa kampeni.
Madai mengine yaliyotolewa katika kikao hicho ni pamoja na wagombea hao kuwatuhumu viongozi wa chama kwa kugawa kadi kama njugu kwa wanachama wanaowaunga mkono wagombea hao wawili, hali ambayo ilionyesha wazi uongozi huo hauwatendei haki wagombea wengine.
JIMBO LA NACHINGWEA
Kutoka Nachingwea Mwandishi Mwanja Ibadi, anaripoti kuwa kampeni za uchaguzi zimeendelea kukumbwa na vibweka baada ya nyumba ya Katibu wa CCM tawi la Chingunduli Kata ya Chiola, Alafa Ntila kuchomwa moto.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Alafa alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana, majira ya saa 7 usiku.
Alisema mara baada ya kurudi kutoka kwenye mkutano wa Baraza la Wanawake la CCM uliofanyika mjini Nachingwea kufanya uteuzi wa kuwania Viti Maalumu vya udiwani.
Alisema baada ya kurudi majira ya saa 5 usiku, aliingia ndani ya nyumba yake na kulala, lakini ghafla alianza kuona nyumba inateketea kwa moto bila kujua chanzo chake.
Alisema baada ya moto kuanza alijitahidi kuuzima pamoja na majirani zake lakini ilishindikana na mali zote zilizokuwemo kuteketea.
“Kila kitu kimeteketea ikiwa na pamoja na vyakula na mifugo hivyo kwa sasa sina chochote,” alisema Antila.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Hamisi Kakanaga, alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo hata hivyo alishindwa kulihusisha na mambo ya siasa.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kama lina uhusiano na mambo ya kisiasa lakini naona ni chuki binafsi ndiyo zinasumbua wakati huu,” alisema Kakanaga.
ARUSHA
Kutoka mkoani Arusha, Mwandishi, Ramadhani Siwayombe, anaripoti kuwa kampeni kwa wagombea wanaowania viti mbalimbali vya ubunge na udiwani, wamekuwa kwenye wakati mgumu baada ya kuzomewa na kususiwa vikaoni katika baadhi ya kata hususan Jimbo la Arusha mjini na Arumeru Magharibi.
Waliokumbwa na adha hiyo mpaka sasa kwa kiasi kikubwa ni mbunge aliyemaliza muda wake, Felix Mrema na mbunge wa Arumeru Magharibi anayetetea jimbo hilo, Elisa Mollel, ambao mpaka sasa hali zao zinaonekana kuwa na mashaka ya kurejea katika nafasi hizo.
Siku ya kwanza ya kampeni za CCM, kwenye Jimbo la Arusha Mjini, Mrema akiwa katika Kata ya Murieti na wagombea wenzake alizomewa na wananchi wakidai wamemchoka aondoke, hali iliyotoa faraja kwa wagombea wengine wanaopambana naye, Dk. Hamisi Kibora na Dk. Batilda Burian.
Hali hiyo ya zomeazomea kwa mbunge huyo iliibuka tena katika Kata ya Sokoni, na hali ilikuwa mbaya zaidi katika Kata ya Sombetini, ambapo licha ya kumzomea wananchi waligoma hata kumsikiliza wakati akinadi sera zake.
Baadhi ya wagombea wa udiwani kutoka kata mbalimbali waliofika katika mkutano huo walisema yanayojitokeza hapo ni salamu tosha kwa CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu.
JIMBO LA MTAMA
Katika Jimbo la Mtama, mbunge anayemaliza muda wake, Bernard Membe, amekuwa mgombea pekee katika nafsi ya ubunge jimboni humo, baada ya aliyekuwa mpinzani wake, Shaibu Buriani, kuandika barua ya kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.
Akizungumza na Tanzania Daima, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Lindi, Albert Mgumba, alisema jana alipokea barua ya mgombea huyo ya kujiondoa kwenye kinyang’anyiro kwa kile alichosema ni kutaka kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM.
“Wanachama wawili walikuwa wamechukua fomu katika jimbo hilo, Shabani Buriani na Bernard Membe, lakini mpaka juzi Ijumaa saa 4 asubuhi nilipokea barua ya kujiondoa kwa mgombea Shabani Buriani,” alisema Mgumba.
Kufuatia kujiondoa kwa Buriani, Membe anaungana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (Mpanda Mashariki), Hanry Mwandri, Balozi Khamis Kagasheki (Bukoba Mjini) na Ezekiel Maige (Msalala) kupita bila kupingwa.
JIMBO LA ULANGA MASHARIKI
Kutoka jimbo hilo, Mwandishi Wetu, Juma Kasesa, anaripoti kuwa mmoja wa wagombea ubunge, Aziz Jawad Aziz (Kimetule), juzi aliangua kilio jukwaani wakati akijinadi kwa wanachama wa CCM Kata ya Mwaya ili apigiwe kura za maoni.
Hali hiyo ilisababisha mamia ya wananchi waliokuwepo katika eneo hilo kuungana naye kuangua kilio.
Tukio hilo lililoonekana kugusa hisia za wananchi wa kata hiyo waliojitokeza kwa wingi kuwasikiliza wagombea ubunge wa chama hicho, lilitokea baada ya Aziz kuwaeleza wananchi hao mkasa wa kukamatwa kwake na polisi wiki mbili zilizopita, kwa madai ya kukutwa na nyara za serikali, ambazo ni meno ya kiboko yenye uzito wa kilo tatu.
Aziz aliwaambia wananchi hao kuwa tukio hilo ni njama za maadui zake kisiasa kutokana na yeye kuonyesha nia ya kutaka kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania ubunge.
“Nimechukua fomu kwa kuwa tu mwaka 2005 mimi ndiye nilishinda kura za maoni na ushindi ule ulitokana na ninyi kuniamini, kwa hiyo heshima mliyonipa mwaka 2005 ndiyo naamini mtanipa tena safari hii,” alisema Aziz.
Jimbo la Ulanga Mashariki linawaniwa na wagombea watatu ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Celina Kombani, Daudi Kitolelo na Aziz Jawad Aziz.
Akijinadi kwa wananchi wa kata hiyo Kombani alijitetea kuwa amejitahidi kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2005 kwa kuboresha huduma za afya, elimu ya sekondari, na miundombinu ya barabara na madaraja.
Daraja la Mto Kilombero linalounganisha Wilaya ya Ulanga na maeneo mengine ya nchi liliahidiwa na serikali ya awamu ya nne kuwa lingekuwa limekamilika ifikapo mwaka 2008, lakini wananchi wanasema hakuna kilichofanyika, na ndiyo imekuwa kero kubwa kwao ya muda mrefu.
Kwa upande wake, Kitolelo aliwachekesha wananchi aliposema kuwa wasidanganyike na mbunge kudai kuwa ameleta maendeleo kama vile barabara na madaraja, kwani hiyo ni kazi ya serikali na kwamba mbunge anapaswa kueleza alichokifanya yeye kama mbunge nje ya mipango ya serikali.
JIMBO LA SIMANJIRO
Huko Mwandishi Wetu, Frank David anaripoti kuwa mchakato wa kuteuliwa kugombea viti vya udiwani na ubunge ndani ya CCM umezidi kunoga, baada ya baadhi ya wabunge machachari akiwemo Christopher ole Sendeka wa Simanjiro mkoani Manyara, kuanza kuonja joto ya jiwe licha ya kung’ara bugeni.
Hali hiyo ilimkuta Sendeka juzi, katika mji mdogo wa Mererani alipopanda jukwaani akitarajia kupata ushirikiano wa kutosha kutokana na sera yake ya kuwapiga vita mafisadi, lakini badala yake wanachama wa chama hicho walimgeuzia kibao, wakidai hafai kuwaongoza, hivyo kipindi cha miaka mitano alichotumikia kinatosha.
Sendeka alikumbwa na adha hiyo na kupandisha mori wa Kimasai baada ya kupigwa maswali aliyoona kuwa wauliza maswali hao walikuwa wametumwa na aliowaita mafisadi, likiwemo swali la nini alichowafanyia wananchi wa Kata ya Mererani tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo.
Huku akikumbana na vikwazo kadhaa katika hotuba yake fupi ya kujinadi, Sendeka alikwenda mbali zaidi hata kuwakemea, baadhi ya wanachama walioonekana wazi wazi kumpinga, na akisema: “Angalia wewe mtu mzima kama mimi, unadiriki kupiga kelele.”
Hali hiyo, ilimshinda Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Ramadhani Aikoo na Katibu wa chama hicho wa Wilaya, Jamillah Mujumgu, na kulazimika kuingilia kati bila mafanikio na kusababisha zogo, zaidi wakimtuhumu kuwa anambeba mbunge huyo.
JIMBO LA KIBAHA
Mwandishi Wetu Julieth Mkireri, anaripoti kuwa wanachama wa CCM katika Jimbo la Kibaha Mjini, wametakiwa kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi walio bora, ambao watawafaa katika harakati za kuleta maendeleo na kuachana na wagombea ambao wanatoa zawadi ili wapewe nafasi ya kuongoza.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kibaha Mjini, Maud Bundala, wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa madiwani wa Viti Maalumu.
Alisema baadhi ya wagombea wamekuwa wakiwarubuni wanachama kwa zawadi na ahadi kemkemu ili waweze kupitishwa kwenye mchakato wa kuchagua wabunge na madiwani ili wapate nafasi ya kuchaguliwa Oktoba 31, mwaka huu.
“Unajua watu wengine hawajatoa sadaka kanisani kwa kipindi kirefu na hiki ndicho kipindi chao, wakiwapa pokeeni na nyie mfanye maamuzi ya haki msirubuniwe chagueni kiongozi atakayewafaa ambaye hahangaiki kutoa zawadi,” alisema Bundala.
Katika uchaguzi huo, jumla ya wagombea 19 walijitokeza kuwania nafasi tano za udiwani wa Viti Maalumu, wawili kati yao walikuwa wakitetea nafasi zao.
Wagombea walioibuka kidedea katika uchaguzi huo na kukwaa nafasi hizo tano za udiwani wa Viti Maalumu ni pamoja na Selina Wilson, Tuaje Ponza, Nuru Lwambo na Joyce Mushi.


====================================

P Please consider the environment before printing this e-mail
 
Yale yaleee ya Bwana Mapesa "Cheyo" kuibiwa kura zote hata ya kwake kule bariadi enzui zile!
 
Back
Top Bottom