Urais Zanzibar ni ufa mwingine kwa CCM

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,109
vuainao.jpg
Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Bw. Shamsi Vuai Nahodha akiwa Bungeni na mkewe

Waandishi Wetu, Zanzibar na Dar

IDADI kubwa ya makada wa CCM waliojitokeza kuwania urais Zanzibar imetafsiriwa kuwa ni ishara kuwa chama hicho kina mpasuko mkubwa wakati kikielekea kwenye uchaguzi mkuu.Hadi jana, wanachama 11 walishaonyesha nia ya kuwania urais kumrithi Amani Abeid Karume ambaye amemaliza muda wake na miongoni mwa waliojitokeza ni vigogo katika serikali ya Muungano na ya Zanzibar (SMZ), akiwemo Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha na msaidizi wake, Ali Juma Shamhuna.

Makamu wa Rais Mohamed Shein anaongoza kundi la wana-CCM wanaotaka urais wa Zanzibar na ni mmoja kati ya makada saba waliochukua fomu Jumatatu.

Idadi hiyo imetafsiriwa kuwa inaashiria kufufuka kwa makundi yaliyokuwa yamejijenga kutokana na mitafaruku. Mitafaruku hiyo ni pamoja na mvutano kuhusu hoja ya maridhiano ya Wazanzibari, hoja ya Rais Karume kuendelea au kutoendelea kuongoza visiwa hivyo, suala la uunguja na upemba na uarabu na uafrika.

Mbali na hayo kundi jingine ni lile linalowahusisha watuhumiwa wa ufisadi katika matukio kadhaa ya kashfa zilizoibuka nchini siku za karibuni pamoja na watu wanaowaunga mkono, wakati kundi la pili linawahusisha wanaopinga vitendo vya ufisadi, ambavyo athari zake zinatoka visiwani hadi bara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasomi na wachambuzi wa masuala mbalimbali ya siasa za Zanzibar wamesema kujitokeza kwa makada nane kutoka CCM kuchukua fomu za urais kunaashiria mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho.

“Wingi wa watu waliojitokeza kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais Zanzibar unaashiria kuwepo kwa magawanyiko ndani ya chama hicho hasa huko Visiwani,” alisema Profesa Issa Shivji.

Profesa Shivji alisema katika hali ya kawaida na yenye mshikamano ni vigumu idadi kubwa ya watu kutoka chama kimoja kujitokeza kugombea nafasi moja.

Hata hivyo, Shivji alisema pamoja na kujitokeza kwa idadi kubwa, Zanzibar inahitaji kiongozi atakayekuwa na sifa ya kuweza kumudu kuongoza mshikamano wa jamii ya wakazi wa huko.

“Swali la kujiuliza ni kuwa katika hawa waliojitokeza yupo mwenye sifa ya kuongoza jamii ya Wazanzibari kwa mshikamano,” alihoji Profesa Shivji.

Pia wasomi hao wamesema kulingana na siasa za visiwa hivyo, kunahitajika kiongozi imara aliye na sifa ya kuweza kumudu kuimarisha mshikamano baina ya jamii za huko.

Naye mhadhiri msaidizi wa Kitivo cha Siasa ya Sayansi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Bashiru Ally alisema CCM inakabiliwa na changamoto kubwa na kwamba kati ya waliojitokeza kutaka kuteuliwa wapo ambao hawaaminiki kutokana na rekodi pamoja misimamo yao katika uongozi na wengine wamejitokeza kuwasindikiza wenzao ili waweze kukumbukwa katika utawala.

“Lakini katika kinyang’anyiro hiki natoa nafasi kwa Dk Shein, Vuai na Dk Bilal,” alisema Ally.

Ally ambaye ni mchambuzi wa wa siasa za ndani na nje, alifafanua kwamba anampa nafasi ya kwanza Dk Shein kutokana na kuwa mara nyingi rais anatokana na Baraza la Mawaziri.

“Uzoefu unaonyesha ni vigumu rais akatoka nje ya Baraza la Mawaziri na 'system' (utawala).
Ukiangalia katika uongozi Dk Shein ni mkubwa kwa Vuai na Dk Bilal,” alisema Ally.

Hata hivyo, mhadhiri huyo alisema CCM ina changamoto kubwa ya kuepuka makundi ambayo yanaweza kujitokeza mara baada ya kuteua mgombea wake na kwamba hali hiyo ikijitokeza itampa nafasi kubwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kushinda urais kwa mara ya kwanza baada ya kujaribu mara tatu bila ya mafanikio.

“Kwa bahati mbaya CCM Zanzibar inapambana na Maalim Seif ambaye ni mpinzani wa kweli, mwenye nguvu na anayejua vizuri siasa za huko hivyo wana changamoto kubwa,” alisema Ally.

Naye Profesa Mwesiga Baregu alisema Zanzibar wamezoea michuano mikali ya kisiasa na kwamba si mara ya kwanza kujitokeza wagombea wengi katika nafasi hiyo.

Alisema mbali na kukumbwa na mitafaruku mbalimbali ya kisiasa kwa namna moja au nyingine katika miaka ya hivi karibuni, miongoni mwa wagombea hao nane wapo waliohusika moja kwa moja na mitafaruku hiyo.

“Mtu ambaye hakuhusika katika mitafaruku hiyo ni Dk Shein na inaonekana ataweza kuunganisha Wazanzibari wote na hata maamuzi ya kumteua yanaweza yasiwagawe Wazanzibari,” alisema Profesa Baregu.

“Pia Dk Shein hayuko kwenye makambi haya ya akina Karume wala Dk Salmini au CCM Asilia na CCM Mtandao, hivyo haya ni mambo yatakayomfanya achaguliwe,” alisema Profesa Baregu.

Alisema kwa miaka mingi kumekuwa na malalamiko kwamba wapemba hawapewi nafasi ya kuongoza serikali ya Zanzibar, hivyo hiyo inaweza kuwa sababu nyingine kubwa ya kumweka Shein madarakani.

Baregu, ambaye pia ni mhadhiri wa siasa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine alisema: “Kwa sababu waswahili wanasema ‘mchawi mpe mtoto amlee’, safari hii utamaduni wa kwamba Mpemba hatawali unaweza kumalizika na "Shein akapewa mtoto wa kulea”.

“Shein amekuwa katika mchakato wa kuleta maridhiano kwa upande wa Muungano, lakini pia nampa nafasi ya pili Mohammed Seif Khatib ingawa hajachukua fomu wala kutangaza nia,” aliongeza Profesa Baregu.

Mhadhiri wa sheria wa UDSM, Dk Sengondo Mvungi alisema idadi kubwa ya wanaowania urais swa Zanzibar “inaonyesha kiwango cha juu cha uelewa wao wa katiba ya nchi na haki zao”.

“Hilo la kwamba nani anaweza kushinda tuwaachie wenyewe, lakini mimi nadhani kwa vile Dk Shein alikuwa huku katika nafasi kubwa tena isiyo na kikomo, basi hadi kuamua kwenda kurudi Zanzibar ni mipango ishapangwa. Lakini sisi tusijiingize huko hebu tuwaachie wenyewe wajiamulie,” aliongeza Dk Mvungi.

Mwenyekiti mwenza wa Mpango wa Utafiti wa Elimu ya Demokrasia (Redet), Dk Benson Bana alisema: “Kwanza tuwapongeze tu wametambua haki yao na wameonyesha ukomavu wa demokrasia.”

“Kwa kusisitiza tu ni kwamba Zanzibar kwa sasa inahitaji rais mwanamaridhiano ili atupeleke mbele katika amani na maendeleo wala asiturudishe nyuma katika maafa ya mwaka 2001.”
Chanzo Urais Zanzibar ni ufa mwingine kwa CCM

Kwa mawazo yangu CCM imeshapitwa na wakati, haswa Kisiwani Zanznibar jamani CCM itabidi waache Zanzibar safari hii ichukuwe CUF. CCM imezeeka katika mambo ya uongozi.
 
Maalim Seif: Wagombea CCM hawanitishi


KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatishwi na wagombea wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu kwa ajili za kuwania urais wa Zanzibar. Kauli ya Maalim Seif inakuja wakati kesho jumla ya wagombea sita wa CCM akiwemo Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein wanatarajiwa kuchukua fomu za kuwania urais visiwani humo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili, Seif alisema anamsubiri kwa hamu mgombea atakayeteuliwa na CCM katika kinyanganyiro cha kuwania urais na kwamba, kati ya waliojitokeza hakuna atakayemtisha. “Kwa kweli sitishwi na wagombea wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu kwa ajili za kuwania urais wa Zanzibar. Namsubiri kwa hamu mgombea wao,” alisema Maalim Seif huku akionekana ni mwenye furaha.

Seif aliyasema hayo mara baada ya kufungua mkutano mkuu maalumu wa kupiga kura ya maoni ya kuchagua wagombea Ubunge wa Jimbo na viti maalumu kupitia chama hicho katika jimbo la Temeke na Kigamboni. Hata hivyo, Katibu mkuu huyo ambaye hii itakuwa ni mara ya nne kugombea, alisema wagombea wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu wametekeleza haki yao ya msingi ya kuchaguliwa na kuchagua kwa mujibu wa Katiba.
“Pamoja na kwamba ninamsubiri mbele ya safari mgombea wa CCM, nawapongeza wagombea waliojitokeza kwa kuwa wametumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchaguliwa na kuchagua,” alisema Maalim Seif Wagombea wa CCM watakaochukua fomu kesho kwa ajili za kuwania urais wa Zanzibar katika Ofisi Kuu Kisiwandui ni Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Abeid Karume, Kamishna wa Idara ya Utamaduni Zanzibar, Hamad Bakari Mshindo.

Wengine ni Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamuhuna, Waziri Kiongozi Mstaafu, Dk Mohammed Gharib Bilal. Awali, akifungua mkutano huo, Maalim Seif alikemea vikali vitendo vya rushwa na siasa za kuchafuana, akisema mgombea anayefanya mambo hayo amekosa sifa na asichaguliwe.

Alisema siku zote wamekuwa wakiisema CCM kutokana na viongozi wake kugubikwa na vitendo vya rushwa, hivyo hali kama hiyo haitakiwi ndani ya CUF. “Tunaisema CCM kutokana na viongozi wake wengi wamepatikana ka njia ya rushwa, hivyo ukiona mgombea anatoa rushwa pamoja na kuwapaka matope wenzake huyo amekosa sifa na hapaswi kuchaguliwa na hata kuwa kiongozi wa CUF,” alisema Maalim Seif Katibu mkuu huyo alisema kampeni safi ndio inahitajika ndani ya chama hicho na aliwataka wanaCUF kuchagua viongozi wasio na majivuno wenye uwezo na ambao wanauzika katika majimbo yao.

Alisema CUF inahitaji wananchama pamoja na viongozi ambao ni watihifi walio na msimamo na watakaofanya kazi kwa mujibu wa maelekezo ya chama na si mamluki. “Mamluki ndani ya CUF hawatakiwi, chama kimtamshughulikia yoyote ambaye atabainika kufanya vitendo vya rushwa pamoja na kufanya siasa za kupakana matope,” alisema. Kuhusu uchaguzi, Maalim Seif alitaka ufanyike kwa uwazi ili usiwe na malalamiko na alitahadharisha chaguzi zisiongozwe na hisia za kidini na kikabila. “Natahadharisha uchaguzi usiongozwe na hisia za kidini na ukabilia na ufanyike kwa uwazi ili usiwe na malalamiko yoyote,” alisema
Matokeo ya Uchaguzi Zanzibar mwaka 2005, Mgombea wa CCM, Amani Abeid Karume alipata kura 239,332 sawa na asilimia 53.2 akifuatiwa na Seif Sharif Hamad kura 207,303 sawa na asilimia 46.1. Wagombea wengine ni Haji Musa Kitole wa chama cha Jahazi Asilia aliyepata kura 2,110, Abdulah Alli Abdulah wa DP kura 509, Simai Abdurahaman wa NRA, kura 449 na Mariam Ahmed Omari wa Sauti ya Umma (SAU) kura 335. Kura Zilizoharibika 9,613 sawa na asilimia 2.1.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000 mgombea wa CCM Rais Amani Abeid Karume alibuka na ushindi wa asilimia 67 na mpinzani wake Hamad alipata asilimia 33. Mwaka 1995 Hamad alipata asilimia 49.8 wakati Rais mstaafu Dk Salmin Amour alipata asilimia 50.2 lakini Hamad alilalamika kuwa uchaguzi ulitawaliwa na mizengwe na kwamba aliibiwa kura baada ya kushinda.

Chanzo Maalim Seif: Wagombea CCM hawanitishi

Waambie Ukweli Maalim Seif najuwa kama haki itatendeka, utawashinda wote hao hongera Maalim Seif. Nakutakia Safari hii Ushindi Mkubwa dhidi ya Wapinzani wako.
 
Je, hiyo sio demokrasia iliyokomaa? Hivi mmoja tu kuchukua fomu ndio inaonesha hakuna ufa? Au mmoja kuchukua fomu ndio ufa uliowazi na kutoweka kwa demokrasia? Mmoja kuchukua fomu ni sawa na kuchagua mtu na kivuli kama wakati wa Julius Kambarage ambao ni upuuzi na ujinga wa hali ya juu ambao sasa unafanyika ndani ya ssem katika ngazi ya muungano.
 
Back
Top Bottom