Urais CCM balaa

bambumbile

Senior Member
Aug 30, 2009
109
0
Hizi siasa chafu tutazishuhudia sana mwakani na 2015 ndio itakuwa balaa kabisa. Mtandao walianzisha, sasa wamejiunga na wengine kwenye mambo ya kuchafuana.
Urais CCM balaa
• Malecela, Dk. Salim, Prof. Mwandosya wajeruhiwa

na Mwandishi Wetu

NAFASI ya kuwania kiti cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi sasa inaonekana kuzusha balaa yenye kuogopwa na wagombea mbalimbali, kutokana na kuzingirwa na mbinu chafu zenye kudhalilisha kwa kila mwenye kuiwania.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili unaonyesha kwamba, baadhi ya hoja nzito za hivi sasa zinazohusisha baadhi ya wanasiasa na harakati za kugombea urais ndani ya CCM ama 2010 au 2015, zinatoa mwelekeo ule ule wa kuchaguana na kuchafuana kama ilivyokuwa mwaka 2005.
Majeruhi wa kwanza wa siasa hizo safari hii ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye jina lake limekuwa likihusishwa na harakati hizo kutaka urais.
Lowassa mwenyewe katika mahojiano aliyofanya na gazeti dada la hili, alihusisha hoja hizo juu yake kuwa sehemu ya mkakati wa watu ambao hakuwataja, wa kumkosanisha na Rais Kikwete.
Wachambuzi wengine wa mambo wanasema kwamba kusukwasukwa kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta nako kunahusishwa kwa namna moja au nyingine na harakati za urais ndani na nje ya chama hicho.
Ingawa wana CCM wamekuwa wakikubaliana kuwa mwaka 2010, Rais Kikwete ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuendelea kugombea kwa tiketi ya chama chake, hali inaonekana kuwa tofauti na kinyang'anyiro cha mwaka 2015, ambapo majina kadhaa makubwa yamekuwa yakitajwa.
Miongoni mwa wanaohusishwa na kusaka urais mwaka 2015 ni pamoja na Lowassa, Sitta, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha - Rose Migiro na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Hofu hiyo pia imewakumba baadhi ya vigogo waliowania kiti hicho mwaka 2005, ambao sasa wameonekana kuwa kimya zaidi huku wakisisitiza kutotaka kusikia au kukumbushwa yale yaliyowakuta katika mchakato huo uliowafanya wachafuke katika jamii kiasi cha kusababisha makovu yasiyofutika.
"Bwana mdogo nisingependa uniulize kuhusu kuwania urais, kilichonipata mwaka 2005 siwezi kukisahau, urais ni tishio, sitaki kujihusisha nao tena," alisema mmoja wa aliyewahi kugombea nafasi hiyo alipokuwa akizungumza na Tanzania Daima Jumapili.
Baadhi ya wanachama wa CCM waliozungumza na gazeti hili wamebainisha matukio ya udhalilishaji na vitisho walivyofanyiwa wagombea waliowahi kujitokeza kuwania kiti hicho, ndiyo yanayowafanya waione nafasi hiyo mwiba.
Hofu hiyo inachagizwa zaidi na mambo yaliyofanyika katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ambapo Dk. Salim Ahmed Salim, aliyekuwa mmoja wa waliokuwa wakiwania nafasi hiyo alipozushiwa mambo kadhaa, ikiwamo kuhusishwa na kifo cha aliyekuwa Rais wa Zanzibar, hayati Abeid Aman Karume.
Dk. Salim pia aliambiwa si raia wa Tanzania (Mwarabu), pamoja na kuwa mwanachama wa Chama cha Hizbu ambacho kilikuwa kikiutambua utawala wa sultani visiwani Zanzibar, hivyo kuhusishwa moja kwa moja na Waarabu.
Kashfa hizo kwa kiasi kikubwa zilichangia kuharibu sifa ya Dk. Salim ndani na nje ya CCM, hivyo kujikuta akikosa kutimiza ndoto yake ya kuwania kiti hicho ambacho kwa wakati huo kilikuwa na upinzani mkubwa ndani ya CCM.
Baada ya kukumbwa na tuhuma hizo, Dk. Salim aliweka bayana wazi kuumia kwake na kutoridhishwa na mbinu chafu zilizokuwa zikitumiwa na washindani wake, hasa kundi la wanamtandao, kwa kumzushia mambo yenye kumhatarishia maisha yake, pamoja na kupandikiza chuki kwa Wazanzibari na familia ya Karume.
Mgombea mwingine ambaye alionja adha ya kuwania urais ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, ambaye naye kupitia vyombo vya habari alianikwa kumiliki akaunti yenye zaidi ya sh trilioni tano nje ya nchi.
Sumaye alionekana kushtushwa na habari hizo pasipo kujua ni mkakati kabambe wa kumchafulia jina lake ili asiweze kupitishwa na vikao vya juu vya chama hicho kuwa mgombea urais.
Kiongozi huyo pia alishutumiwa kumiliki mashamba makubwa kwa njia zinazotiliwa shaka katika Kijiji cha Kibaigwa, wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma.
Tuhuma hizo zilimfanya kiongozi huyo mstaafu kukwaa kisiki katika mchakato huo huku akiendelea kuugulia majereha aliyoachiwa na wanamtandao waliodhamiria kumuingiza Rais Jakya Kikwete, Ikulu pasipo kuangalia madhara ya mbinu zisizofaa walizokuwa wakizitumia.
John Samwel Malecela, ni miongoni mwa majeruhi wa wanamtandao katika kinyang'anyiro cha urais, ambapo katika pilikapilika hizo alizushiwa maneno kadhaa, ikiwamo uhusiano wake na nchi za Kiarabu, ambazo zilikuwa zikimsaidia kifedha.
Katika lengo hilo hilo la kumchafua Malecela, alihusishwa kutokuwa na uwezo wa kukikalia kiti hicho kutokana na umri wake kuwa mkubwa, tofauti na Kikwete ambaye alipambwa kwa nyimbo za kuwa ni kijana na mwenye kufanya kazi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.
Wakati propaganda hizo na mambo mengine yakiendelea, Malecela alijitokeza na kudai kuwa mbinu zinazotumika si za kiungwana, huku akiwaponda wale wanamuona mzee huyo hafai kuongoza, kwa kuwaambia kuwa kiti cha urais si kwa watu wenye nguvu za kubeba zege, bali huhitaji busara, utulivu wa mhusika pamoja na kuzungukwa na watendaji imara.
Wachambuzi wa masuala ya siasa waliziona mbinu za wanamtandao zilikuwa mbaya na zisizofaa katika medani ya siasa, kwa kuwa zililenga kuchafua majina ya watu na kupandikiza chuki ambazo mwisho wake ni kukigawa chama na wananchi.
Wakati wanasiasa waliojitokeza kuwania urais wakishughulikiwa kwa stahili hizo mwaka 2005, Lowassa anatajwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya CCM iwapo atasimama kugombea nafasi hiyo mwaka 2015.
Pamoja na ushawishi huo unaoelezwa kuwa anao Lawassa, bado atakabiliana na wakati mgumu dhidi ya Membe ambaye ameshaanza kupigiwa chapuo ya kuwania kiti hicho Dk. Asha -Rose Migiro naye anaweza kutoa changamoto kubwa katika kinyang'anyiro hicho hasa kutokana na uwezo wake wa kuongoza Umoja wa Mataifa. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanabashiri Migiro anaweza kupata wakati mzuri kwa kuwa baadhi ya watu hivi sasa wangependa kuona mageuzi kwa nchi kuongozwa na rais wa kike mwanamke kama ilivyo Liberia. Wachambuzi hao pia wanaonya kwamba kama vigogo wa CCM hawataacha matumizi ya kampeni chafu katika kuwania kiti hicho, makundi ndani ya chama hicho yatakimaliza na kuna hatari uhusiano baina ya wanachama ukazidi kudorora kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.
 
kweli nchimbi akiwa rais nahama nchi- kilaza huyu?????? anyebwebwa na JK.
dataz zinasema waliingia mkataba kwamba fadhila zake zilipwe kwa ''kubebwa'' na kuhakikisha anakuwa waziri!
waliuziana nini,au walipigana tafu wapi hiyo naomba ''iwe siri''
 
JK lazima atafute mtu wa kumlinda ili asije akamletea shida baadae, so Nchimbi anaweza kuwa chaguo lake, ila wananchi nao tuwe na chaguo letu kwa kuwa mtu kama Nchimbi hatufai
 
dataz zinasema waliingia mkataba kwamba fadhila zake zilipwe kwa ''kubebwa'' na kuhakikisha anakuwa waziri!
waliuziana nini,au walipigana tafu wapi hiyo naomba ''iwe siri''

nasikia kijana yupo fiti sana kwenye kamati ya ufundi, inawezekana huko ndiko alipoweka mkataba na JK
 
nasikia kijana yupo fiti sana kwenye kamati ya ufundi, inawezekana huko ndiko alipoweka mkataba na JK

naam!
lakini HERI MIMI SIJASEMA BWANA!maanake mambo madogo haya utashangaa yudabliyutii wanaanza kukuwambala
 
Jk amekana kuwa ilani ya uchaguzi ya ccm hakuandika yeye! Kwa maana nyingine yeye hahusiki! Ila imemuweka madarakani!!!
Just the matter of time ... Wote mlio ichafua hii ardhi tukufu mtakiona chamtemakuni ... Wananchi hawashangilii vogue zenu wala nyumba zenu wala nguo zenu wala hongo zenu za kanga, vitenge na visheti... Si mbali wewe jk na wenzio mtajibu kwanini mliteketeza ardhi hii tukufu na kuacha wana wa tz wakihaha na kuangamia ktk lindi kubwa la ufukara na umaskini usiomithilika... Mtaiba , mtakaba, mtadhulumu uchaguzi lakini kamwe historia haitafutika ...
 
Habari iumejaa udaku mtupu, sijui vyanzo vya kuaminika, sijui mtu ambae hakutaka jina lake litajwe, sijui uchunguzi wa gazeti letu nk haya ni mambo ya kutunga na kufikirika zaidi kuliko ukweli, lakini kwa kuwa hayo ndio tunayopenda kusikia tuendelee kujadili upupu huu
 
Back
Top Bottom