Upungufu wa madawa Sekta ya Afya

Msanii

Platinum Member
Jul 4, 2007
22,548
29,623
Wakuu,
nawakilisha taarifa kuhusu utafiti uliofanyika kuhusiana na hali ya sekta ya afya nchini ktk eneo la upatikanaji wa madawa.
Nimeambatanisha na attachment ya documents husika
[h=2] Taarifa kwa Vyombo vya Habari Jumapili 30 Octoba 2011[/h][h=2]Upungufu wa madawa walemaza Sekta ya Afya[/h]
Huduma ya afya nchini imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji usioridhisha, kutokana na kuwa na upungufu na ukosefu wa dawa na vifaa tiba. Utafiti uliofanywa na Sikika hivi karibuni juu ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umebaini kwamba vituo vya kutolea huduma ya afya hukosa dawa muhimu na vifaa vya tiba kwa kipindi cha hadi miezi sita; wakati mwingine.

[h=1]Kwa nini Sikika ilifanya utafiti huu?[/h]Sikika iliamua kufanya utafiti huu baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watoa huduma na watumia huduma ya afya juu ya upungufu wa bandeji aina ya ‘absorbent gauze’ (kifaa muhimu kinachotumika wakati wa kufanya upasuaji na kusafishia vidonda, n.k), katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya. Bandeji za absorbent gauze ilikuwa lengo kuu la utafiti huu ingawa pia ulihusisha upatikanaji wa dawa kama ALU (dawa ya mseto ya malaria), glavu za kufanyia upasuaji, bomba za sindano, amoxilin na sindano za quinine. Utafiti ulifanyika katika halmashauri za wilaya 71 Tanzania bara na katika vituo 30 vya kutolea huduma ya afya. Aidha, utafiti huu pia ulihusisha baadhi ya nchi katika jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo baadhi wa maafisa kutoka Kenya na Uganda walihojiwa. Maafisa kutoka nchi hizo walihojiwa ili kulinganisha upatikanaji wa dawa na vifaa vya kutolea huduma ya afya. Utafiti huu ulifanyika kupitia mahojiano kwa njia ya simu.
[h=1]Je utafiti huu ulibaini nini?[/h]Kwa mujibu wa utafiti huu, asilimia 48 ya wilaya zilizofanyiwa utafiti zilikuwa na bandeji za absorbent gauze. Asilimia 8 tu ya wilaya hizo zilikuwa na kiasi cha kutosha cha bandeji hizo. Asilimia 63 ya vituo vya kutolea huduma za afya vilikuwa na tatizo la upatikanaji ambapo asilimia 37 ya hivyo havikuwa na bandeji hizo kabisa. Asilimia 10 kwa muda wa miezi mitatu hadi mitano. Hali hii ilikuwa hivyo kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita kabla ya utafiti.
[h=1]Upungufu huu husababishwa na nini?[/h]Upungufu wa bandeji za upasuaji (pamoja na vifaa vingine vilivyotajwa) huchangiwa na sababu kadhaa kama ifuatavyo: vipindi virefu kati ya agizo moja na jingine ambapo kwa kawaida vifaa tiba huagizwa kila robo mwaka. Utafiti huu ulibaini asilimia 70 vituo vilivyohojiwa husubiri kwa miezi miwili na zaidi kupata vifaa walivyoagiza. Asilimia 10 tu hupata vifaa walivyoagiza ndani ya mwezi mmoja.

Aidha, upungufu wa vifaa huchangiwa na upungufu wa fedha zinazotengwa na kusambazwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba kutoka serikali kuu. Upungufu huu huathiri uwiano kati ya matarajio na maagizo halisi yanayofanywa.


Pia, kuna ugumu katika upatikanaji wa fedha zinazotokana na uchangiaji huduma, CHF, na Mfuko wa Bima ya Afya. Vituo vya huduma hulazimika kupitia michakato mirefu kupata fedha hizo ambazo huwekwa chini ya udhibiti na uangalizi wa Ofisi ya Afya Wilayani (DMO). Kwa mujibu wa utafiti huu, iwapo fedha hizi zitatumika zitachangia kupunguza kero ya upungufu wa dawa na vifaa tiba. Utafiti umebaini kwamba asilimia 30 tu ya vituo vya huduma vilikuwa na uwezo wa kununua vifaa kutoka kwa wasambazaji binafsi kupitia vyanzo mbadala vya fedha.


Pia, utafiti huu umebaini maagizo yanayopelekwa na Ofisi za Afya za Wilaya katika Bohari ya Dawa (MSD) huwa ya chini ikilinganishwa na mahitaji ya robo mwaka. Kwa kawaida, wilaya huhitaji vifurushi 148 vya bandeji za upasuaji ambapo wastani wa kila agizo ni vifurushi 108. Hali hii pia imejitokeza katika vituo vya huduma vilivyohojiwa ambapo ilibainika kwamba mahitaji yao ya robo mwaka kwa wastani ni vifurushi 12 na wao huagiza vifurushi 8. Lakini hali hii huchangiwa na uchache wa fedha zinazotengwa katika akaunti zao za Bohari ya Dawa. Pamoja na udhaifu katika makadirio ya mahitaji, Ofisi nyingi za Afya za Wilaya asilimia 93 na vituo vya huduma asilimia 90 vilipata vifurushi pungufu vya bandeji na hivyo kusababisha upungufu na wakati mwingine ukosefu wa bandeji hizo.


Mapendekezo

Katika ripoti yake Sikika inapendekeza Bohari ya Dawa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia upya utaratibu wa kupokea maagizo kila baada ya miezi mitatu ili angalau maagizo yawe yanafanywa kila mwezi. Marekebisho haya yatapunguza idadi ya siku ambazo vituo vya afya hukosa vifaa vya tiba vinavyopatikana Bohari ya Dawa. Pia, Wizara ya Fedha na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa pamoja zinapaswa kuweka kanuni za usambazaji wa fedha kwa ajili ya dawa muhimu katika vituo vya huduma. Lakini pia, zinapaswa kuhakikisha fedha zinapatikana na zinasambazwa kwa wakati.


Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Wizara ya Afya zinapaswa kufanya uchunguzi ili ziweze kubaini chanzo cha ugumu katika upatikanaji wa fedha zinazotokana na michango mbalimbali ambazo kwa kawaida huifadhiwa katika akaunti za wilaya. Fedha hizi zinaweza kusaidia ununuzi wa dawa pindi Bohari ya Dawa inapoishiwa akiba yake ya dawa.

Ingawa utafiti huu ulitumia bandeji za absorbent gauze kama chanzo cha utafiti, lengo
ilikuwa kuchunguza na kujadili matatizo yanayokabili ununuzi na mfumo wa usambazaji dawa nchini. Sikika itatumia matokeo ya utafiti huu kutetea uboreshaji taratibu za ununuzi na mfumo wa usambazaji dawa.


Mr. Irenei Kiria

Mkurugenzi wa Sikika, P.O.Box 12183 Dar es Salaam, Simu: +255 222 666355/57,
Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz, Tuvoti:
www.sikika.or.tz
 

Attachments

  • Press statement- gauze report final.docx
    92 KB · Views: 63
  • Taarifa kwa umma Gauze swa .doc
    114.5 KB · Views: 118
Back
Top Bottom