Upinzani waunga mkono Muswada wa Katiba Mpya

Sumasuma

JF-Expert Member
Jun 23, 2011
342
110
Kafulila auponda, asema bado una matundu makubwa
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KAMBI ya Upinzani Bungeni, imeunga mkono mapendekezo ya Serikali katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya kusimamia mchakato wa Katiba Mpya.

Akiunga mkono marekebisho ya muswada huo bungeni mjini Dodoma jana kwa niaba ya kambi hiyo, Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Tundu Lissu, alisema Rais Jakaya Kikwete amekuwa msikivu katika jambo linalogusa maslahi ya Taifa.

Amesema kambi hilo inaunga mkono mapendekezo ya Serikali na kuwaomba wabunge wote wauunge mkono ili kupata Katiba Mpya wanayoitaka Watanzania.

Kutokana na maelezo hayo, Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda, alisema kilichoelezwa na Bw. Lissu ni jambo la kufurahisha na kupongezwa na kuwataka wabunge waache malumbano badala yake wabishane kwa hoja.

“Waheshimiwa Wabunge naomba muujadili muswada huu kwa pamoja ili Watanzania wapate mafanikio katika mazingira yenye umoja, upendo na amani,” alisema.

Akitoa maoni yake kuhusu muswada huo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Bw. Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema Rais Kikwete anastahili pongezi kwa jinsi alivyoweza kuushghulikia na kushauri wabunge wote bila kujali itikadi za vyama kuunga mkono.

Maoni ya David Kafulila muswada huo

Akizungumza na Majira nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini Bw. David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amedai kushangazwa na mvutano wa kisiasa kuhusu mabadiliko yaliyoletwa na Serikali wakati katika sheria hiyo, kuna mambo mengi ya msingi yanayopaswa kubadilishwa.

“Nilijaribu kuomba nafasi ya kuchangia ili nitoe maoni yangu lakini ikashindikana kwani Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, alisema chama chetu kilipewa nafasi ya mtu mmoja ambaye ni Mbunge wa Kasulu Mjini, Bw. Moses Machali.

“Ningependa kukumbusha kuwa, mimi na Mheshimiwa Felix Mkosamali, ndiyo tulikuwa wajumbe wa Kamati ya Sheria na Utawala, Mkosamali ni mjumbe wa kamati hii.

“Mimi ni miongoni mwa wajumbe ambao wameongezwa wakati wa kupitia muswada huu, pia ikumbukwe mimi na Mkosamali ndio tuliungana na Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), kutoka nje katika mkutano wa tano wa Bunge ili kupinga namna mchakato ulivyoendeshwa,” alisema.

Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hilo na nafasi aliyonayo, upo umuhimu mkubwa wa kuzungumza kwani mabalozi wa nchi tano za Ulaya walipokwenda bungeni katika mkutano wa tano wa Bunge, yeye alikuwa miongoni mwa wabunge ambao alikutana nao na kutoa maoni.

“Mimi naamini kuna mambo mengi ya msingi ambayo yalipaswa kubadilishwa na kuletwa katika marekebisho ya sheria hii baada ya vikao vya Rais na wadau wengine vikiwemo vyama vya siasa.

“Mabadiliko yaliyoletwa sio mambo ya msingi ambayo yangesaidia kuiboresha tume na mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya. Kwa mfano, hoja ya kumwondoa Mkuu wa Wilaya na kumuweka Mkurugenzi (DED), Wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanataka DC ndio asimamie, hotuba ya kambi rasmi ya upinzani inapendekeza DED,” alisema Bw. Kafulila.

Aliongeza kuwa, ukweli ni kwamba DED na DC wote hawafai kwa sababu ni sehemu ya Serikali badala yake ilipaswa jukumu hilo litekelezwe na tume yenyewe ambayo inapaswa kuwa huru.

“Hapa ndipo inakuja hoja ya mchakato mzima wa kura ya maoni kusimamiwa na Tume Huru, uamuzi wa kuifanya Tume ya Uchaguzi kusimamia mchakato huu ni kinyume na msimamo wetu wa awali kama wapinzani kwa sababu moja ya hoja ya mahitaji ya Katiba Mpya ni tume huru ya uchaguzi sasa haiwezekani tume mbovu ya uchaguzi isimamie mchakato wa kupata katiba huru,” alisema.

Bw. Kafulila aliongeza kuwa, kwanza wangekubaliana jinsi ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itasimamia mchakato wa kupata Katiba Mpya ambayo Watanzania wanaitaka.

Hoja ya Tume Huru kusimamia mchakato wa katiba

Alisema hoja hiyo iliachwa kwa sababu tume iliyopo inateuliwa na rais na ndiyo mwenye mamlaka ya kumtoa mjumbe yeyote hivyo marekebisho yaliyopelekwa bungeni ni mapendekezo ya kumtoa mjumbe wa tume anayetuhumiwa kukiuka kanuni za maadili.

“Kimsingi haikupaswa kuteua kamati badala yake sheria ilipaswa kutamka rasmi kamati hiyo itakuwa na akina nani ili iwe huru badala ya kuteuliwa na rais kwani yawezekana kosa mjumbe likawa mvutano unaohusu nguvu za Serikali kwa tume.

Hoja ya sekretaerit huru

Bw. Kafulila alisema, kwa mujibu wa sheria hiyo sekretarieti itaundwa na Waziri mwenye dhamana hivyo kuondoa uhuru wa utendaji kazi wake.

Alisema sekretarieti hiyo ilipaswa kuteuliwa na tume, kuwajibika kwa tume ili kupunguza mkono wa Serikali katika mchakato na utendaji wa kupata Katiba Mpya.

Aliongeza kuwa hoja ya ushiriki wa jumuiya za kiraia, taasisi za dini na vyama vya siasa, marekebisho yaliyopelekwa sehemu A, kifungu cha 7, yanatoa uhuru wa jumuiya hizo kushiriki kwa kualikwa na rais lakini marekebisho ya kifungu cha 8, inatamka rais hafungwi na mapendekezo hayo anapotaka kuteua watu wengine kuwa wajumbe.

“Hapa kwa tafsiri rahisi ni kwamba, haki imetolewa katika kifungu cha 7 na imepokonywa kwenye kifungu cha 8 kwa kuwaweka wananchi tayari ili wasishangae itakapotokea mapendekezo yaliyopelekwa na jumuiya yoyote kukataliwa yote.

“Ingepaswa kuweka wazi kuwa rais atalazimika kuteua miongoni mwa waliopendekezwa na sio nje ya waliopendekezwa, pamoja na sheria hii kupitishwa leo (jana), ina matundu makubwa ya kuweza kuifanya isimamie mchakato huu muhimu kwa uhakika, sheria hii bado inategemea dhamira ya rais mwenyewe kuliko mfumo tulioweka:A S 465:
 
Back
Top Bottom