Unategemea kujifunza nini mwaka 2009

Yona F. Maro

R I P
Nov 2, 2006
4,202
218
Unategemea kujifunza nini mwaka 2009?
Heri ya mwaka mpya! Hakika 2009 imeingia kwa kishindo. Hekaheka za kujipanga upya zinaendelea. Huu ndio wakati wa kuorodhesha malengo yetu ya mwaka kwenye shajara mpya.

Sasa nami nachukua kalamu yangu ya kiteknolojia niorodheshe malengo yangu mahususi. Safari hii sitaki kabisa kuwa na matazamio mengi. Sitaki kujipa ahadi nyingi tamutamu zisizotekelezeka. Sipendi madeni hata kama ni madeni binafsi. Si wahenga walituasa kuwa ahadi ni deni au sio?

Mwaka huu moja ya malengo yangu makuu ni kujifunza kuhusu utamaduni wetu. Mwalimu wangu alinifundisha kuwa utamaduni ndio mwenendo mzima wa jamii fulani. Maisha ya watu wa jamii hiyo, tabia zao, miiko yao, sera/sheria zao, mipango yao na kadhalika ndio utamaduni wao.

Kama hiyo ndio maana ya utamaduni basi njia rahisi ya kujua kwa nini mambo yanakwenda hivi au vile nchini ni kujifunza utamaduni wetu. Kumbe inawezekana kabisa kuwa ufisadi, umaskini, uuaji wa maalbino, uchomaji wa vibaka na kadhalika ndio utamaduni wetu hasa. Kha! Kweli?

Labda ni kweli. Lakini kwa kuwa sina uhakika ndio maana nimedhamiria kujifunza kwa undani kuhusu utamaduni wetu. Lazima mwaka huu nijue ni kwa nini tunafanya mabaya yote tunayoyafanya japo tunadai jamii yetu ina utamaduni wa utulivu, upendo, utu, udugu na ujamaa.

Ndio, lazima nijifunze kuna nini kwenye nyimbo, methali, misemo na vichekesho vyetu vinavyodhihirisha utamaduni wetu. Naam, kama sanaa ni kielelezo cha utamaduni wetu na kioo cha jamii yetu basi lazima nijifunze nini hicho katika riwaya zetu na michezo yetu ya kuigiza kinachoakisi tabia za kifisadi, kichoyo na kiuaji ambazo sasa zimeshamiri sana katika nchi yetu.

Ayub Rioba endelea kuandika makala zinazochambua methali na misemo yetu kutuonesha jinsi gani zinachangia kutujengea mazoea fulani. ‘Asiyesikia la mkuu huvunjika guu’. Aisee hivi hii methali ina maana tusipowasikia wakuu wenye ushauri wa busara basi tutapoteza mwelekeo? Au ina maana tusipowasikia wakuu wenye ujasiri wa kifisadi basi ‘kitumbua kitaingia mchanga’?

Eti utamaduni wa jamii yenye maneno kama ‘kula na wakubwa’ na ‘liwa ule’ ni utamaduni wa aina gani? Ewe Mzee Kifimbo Cheza naomba uendelee kunyanyua kifimbo chako cha Kiswahili Sanifu nijifunze mwenendo wa jamii yenye maneno ya mtaani kama ‘hilo dili’ na ‘kipusa hicho’ ni mwenendo wa aina gani. Enyi wasanii nielezeni inakuwaje ‘usanii’ maana yake sasa ni ujanja?

Bakita naomba mwaka huu mnieleze inakuwaje neno ‘kitu kidogo’ linatumika sana. Basata inakuwaje wakati jirani zetu wanaimba ‘nchi ya kitu kidogo ni nchi ya watu wadogo’ sisi tunazidi kujenga jamii inayotumia sana neno ‘kitu kidogo’? ‘Bosi wangu, sh-ka-moo’ nayo inatokea wapi?

‘Chezea bahati’. ‘Cheza salama’.‘Chama letu.’ ‘Chizi wangu.’ ‘Chachandu yangu.’ ‘Chai yako.’

‘Vijisenti.’ ‘Viepa.’ ‘Vimwana.’ ‘Vitotoz’.‘Vodafasta.’ ‘Vitigo.’ ‘Vikuku.’ ‘Vipusa.’ ‘Vigogo.’

Jamani niambieni nini maana ya maneno haya yote yanayozuka na kutumika kila kukicha! Je, ni matokeo ya utamaduni au ndio utamaduni wenyewe? Jamii yetu inaweza kujifunza nini kuhusu mwenendo wake kutoka kwa maneno tete/tata kama haya? Jiulize, au umeshajijibu ‘sina jinsi’?

Rai yangu kwako leo ewe msomaji mwema ndio hii: ungana nami tujifunze undani wa msingi na mwenendo mzima wa jamii yetu. Rejea mifumo na mitazamo yetu ambayo labda ndio chanzo cha matatizo makubwa ya kitaifa yaliyotuyumbisha sana 2008. ‘Rusha roho’ ya jamii hii kwa kuzihoji na kuzifuatilia nyendo zake kwa kina ili tuutafakari upya utamaduni na mustakabali wa taifa letu.

Pengine tukijiuliza kwa nini tunaongea jinsi tunavyoongea, tunafanya kazi jinsi tunavyofanya kazi na tunafikiri jinsi tunavyofikiri basi tutapata jibu kwa nini hali iko kama ilivyo sasa na kutambua tunapaswa kufanya nini hasa ili kuiboresha au kuibadili. Pamoja na yote jamii hii ina hazina nzuri ya kiutamaduni tunayoweza kuitumia vilivyo 2009 kupambana na hali halisi. Penye nia pana njia.

Uvivu nyumba ya njaa. Utamu wa muwa kifundoni.Ukiona vyaelewa vimeundwa. Ukitaka cha uvunguni sharti uiname. Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Usiache mbachao kwa msala upitao.

© Chambi Chachage
 
Back
Top Bottom