Unafiki wa kina Profesa Mwandosya

tibwilitibwili

Senior Member
Sep 12, 2006
184
10
RAIA MWEMA UGHAIBUNI

Unafiki wa kina Profesa Mwandosya

Evarist Chahali, Uskochi Februari 27, 2008



BAADHI ya ndoto zangu za utotoni zimetimia, nyingine zinakaribia kutimia na nyingine zimekufa kifo cha asili.

Miongoni mwa ndoto zangu “zilizofariki dunia” ni pamoja na ile ya kuwa msanii wa muziki wa kufokafoka (rapa) ambaye pia ni mtengeneza muziki (prodyusa).

Ndoto za kuwa rapa zilikufa mapema nilipobaini kwamba nisingemudu “kumwaga vina” ipasavyo kutokana na “ulimi mzito.”

Ndoto ya uprodyusa ilichochewa zaidi na namna ninavyowathamini watu wanaomwezesha msanii kufanya vizuri kwenye fani yake bila wao (maprodyusa) kupata sifa zinazostahili.

Wimbo unapotamba, anayevuna sifa ni msanii, ni watu wachache sana wanaojihangaisha kujua nani aliyetengeneza wimbo huo. Na hiyo si kwenye muziki pekee, kwani mara nyingi hata tunapoona filamu nzuri, wengi wetu tunasahau umuhimu wa muongozaji mkuu, wataalam wa “stunts”, “special effects” na hata “extras”.

Sikufanikiwa kutimiza ndoto zangu za uprodyusa baada ya masuala mengine muhimu zaidi kujitokeza maishani mwangu. Hata hivyo, mapenzi yangu kwa muziki wa kufokafoka bado yapo palepale. Napata uhuru zaidi wa kuupenda muziki huo (ambao hupendelewa zaidi na vijana) kwa vile kwa mujibu wa taratibu zetu huko nyumbani umri si kigezo cha mwisho wa ujana (waulize UVCCM wakutafsirie kijana ni mtu wa aina gani.)

Mapenzi yangu kwenye rap yamekuwa yakinihamasisha kufuatilia kwa karibu kinachoendelea kwenye dunia ya muziki huo. Naamini wengi wenu mnamfahamu rapa maarufu Jay-Z.

Kwa wasiomfahamu, huyu ni mshirika wa Beyonce na waliambatana pamoja kwenye ziara yao ya hivi karibuni huko nyumbani ambako rapa huyo alifanya onyesho na kutekeleza jukumu lake la kuleta changamoto kwenye sekta ya maji duniani.

Rapa huyo ni miongoni mwa Wamarekani Weusi walio matajiri na wenye mvuto mkubwa kwenye jamii. Hivi karibuni alitoa albamu yake mpya iitwayo “American Gangster”.

Baadhi ya wachambuzi wa muziki wa kufokafoka nchini Marekani wamemlaumu Jay-Z kwa namna albamu hiyo ilivyo na mapungufu katika ujumbe kwa baadhi ya Wamarekani Weusi wenzie wanaoendelea kuamini katika maisha ya silaha, madawa ya kulevya, uhalifu na “ponda mali kufa kwaja” bila kusahau matumizi ya neno “nigger” (kwenye rap wanaita “nigga”).

Wachambuzi hao wanadai kwamba walitarajia kwamba rapa huyo ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter angeenda mbali zaidi ya staili ya kawaida ya muziki wa rap iliyotawaliwa na kujisifu kwingi, kuthamini “ghetto fabulous”, maneno yasiyofaa dhidi ya wanawake, “ujanja wa mtaani” ambao kwa bahati mbaya umeishia kujaza Wamarekani Weusi wengi magerezani na ujumbe mwingine usio na umuhimu mkubwa kwa mtu anayetaka kujikomboa kutoka tabaka la chini (social mobility).

Kimsingi, Jay-Z anaonekana machoni mwa wachambuzi hao kama mnafiki kwa kuthamini zaidi mauzo ya muziki wake bila kujali umuhimu wa ujumbe uliomo kwenye nyimbo zake.

Pengine hadi hapa msomaji wangu mpendwa unadhani kuwa makala hii ni kuhusu muziki pekee. Hapana. Dhana kuu ni UNAFIKI (kama huo wa Jay-Z).

Kwanza, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya aliwashangaza wengi hivi karibuni alipowataka DAWASCO kutowaanika hadharani mawaziri wanaodaiwa bili za maji. Binafsi, licha ya uwaziri wake, namheshimu Mwandosya kutokana na uprofesa wake kwenye fani inayohitaji akili ya kutosha.

Tafsiri pana katika hoja ya Mwandosya ni kwamba vigogo wanastahili “special treatment” kutoka kwa DAWASCO bila kujali kwamba kwa kufanya hivyo Mamlaka hiyo itajikuta inabagua wateja wake ambao wote wana haki na wajibu sawa katika kupata na kulipia huduma ya maji.

Kama waziri mpya anaanza kazi kwa “gea” ya namna hiyo, basi tuna safari ndefu na ya shaka katika visheni ya Taifa ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji.

Kati ya vikwazo vikubwa vya maendeleo barani Afrika ni tabia sugu ya kulindana. Deni ni deni tu, mdaiwa akiwa waziri au mpiga debe wa daladala wote wanapaswa kulipa deni wanalodaiwa ili kuiwezesha DAWASCO kuwahudumia wateja wake kulingana na matarajio.

Ushauri wa bure kwa Mwandosya ni huu: kama anajisikia vibaya pindi waziri mmoja anapotajwa kuwa mdaiwa sugu wa maji, anachopaswa kufanya ni kuwasiliana na waheshimiwa wenzie kwa faragha kwamba wanakwamisha ufanisi wa mamlaka hiyo iliyo chini ya wizara yake, na wasipolipa bili wataumbuka hadharani. Kuficha tatizo hakuwezi hata mara moja kuwa sehemu ya ufumbuzi wa tatizo hilo.

Unafiki wa pili umejitokeza huko Monduli katika mapokezi ya aliyekuwa waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambako Askofu Thomas Laizer wa KKKT alijiingiza kwenye ulingo wa siasa na kurusha vijembe kadhaa dhidi ya anaiodhani wanamwandama Lowassa kuhusu sakata la Richmond.

Kauli za mchunga kondoo wa Bwana huyo ndizo kwa namna moja au nyingine zinaakisi malalamiko ya baadhi ya Waislam kwamba wao wakizungumzia mambo ya siasa wanaambia ni mwiko kuchanganya dini na siasa, lakini akina Laizer wanaweza kupanda majukwaa ya kisiasa na kuleta porojo ambazo haziwezi kuwasaidia waumini wao kuuona ufalme wa Mbingu.

Hivi msomaji unapomsikia Askofu anatoa kauli kama hii (nanukuu maneno ya Askofu Laizer) “Ukuni ulioko kwenye kona usiucheke ukuni ulioko jikoni ukiungua kwa sababu nao unasubiri kuungua” unapata picha gani?

Tafsiri ya haraka haraka ni kwamba watu wanaomcheka Lowassa wanapaswa kujua kuwa nao wanaweza kukumbwa na “tsunami ya kisiasa” kama iliyomkumba Lowassa. Askofu huyo alipaswa kuacha vijembe na badala yake angesisitiza “kila kuni kuogopa moto wa milele unaowasubiri wadhambi wote siku ya kiama.”

Alinichanganya zaidi alipodai “kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe” kwani kama ukweli ndio huo basi tuna umuhimu gani wa kuwa na viongozi wa dini kwani “kila muumini atakwenda peponi au motoni kivyake.”

Unafiki wa tatu ni katika taarifa zilizopatikana hivi karibuni kwamba baadhi ya mafisadi walionufaika na fedha za EPA wameanza kuzirejesha. Hivi kwanini hadi leo hakuna hata mtu mmoja aliyefikishwa kwenye chombo cha dola kuhusiana na suala hilo? Kila siku tunasikia kwamba wahusika watachukuliwa hatua na uchunguzi unaendelea.

Sawa, hata uchunguzi wa kupata tiba ya ukimwi umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya muongo mmoja sasa na bado hakuna mafanikio. Kufanya uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa aliye huru ni sawa kabisa na kukwamisha uchunguzi huo kwa vile mtuhumiwa atauvuruga.

Katika utetezi wa hivi karibuni wa Lowassa, jina la Johnson Mwanyika limetajitokeza tena. Narudia kutoa wito kwamba Mwanyika na Edward Hosea lazima wajiuzulu. Hawa ni sehemu ya tatizo wanalolichunguza. Kuendelea kwao kuwa wajumbe wa tume inayochunguza ufisadi wa Benki Kuu ilhali Ripoti ya Tume teule ya Bunge imeonyesha bayana mapungufu waliyonayo kunaweza kuwafanya wananchi wapoteze imani kwa tume hiyo. Pia nafasi zao kama Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa TAKUKURU zimeshachafuka kutokana na Ripoti hiyo, na kwa kung’ang’ania kubaki madarakani wanaweza kupunguza pia hadhi za taasisi wanazoongoza.



Barua-pepe: epgc2@yahoo.co.uk
Blogu: http://chahali.blogspot.com
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom