JoJiPoJi
JF-Expert Member
- Aug 8, 2009
- 2,907
- 3,261
Robert Nyanda
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibadilishe sifa ya umri wa kupiga kura kutoka miaka 18 ya sasa na kuwa miaka 14 ili kutoa fursa kwa vijana wengi wenye umri huo kutumia haki yao ya msingi ya kupiga na kupigiwa kura.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar kwa nafasi za udiwani, ubunge na urais zilitia nanga Oktoba 30, 2010. Zilidhirisha umuhimu wa kubadilishwa kwa ibara ya 5 (1) ya Katiba yetu.
Katika kipindi chote hicho cha kampeni tulishuhudia wagombea wakijinadi kwa sera za vyama vyao na kutoa ahadi lukuki ili mradi kuwashawishi wapiga kura kuwachagua kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kutokana na mwamko wa Watanzania katika uchaguzi ukihanikizwa na vyombo vya habari vilivyo kuwa bega kwa bega na wagombea katika harakati zao za kuomba ridhaa ya wananchi kuongoza.
Watu wengi walijitokeza katika kampeni hizo, hali iliyoonyesha mwamko wa kweli kwa Watanzania kuhusiana na mambo ya uchaguzi na kupelekea wanasiasa wengi hasa vijana kuamini kuwa utakuwa na mabadiliko makubwa.
Kampeni hizo zilishuhudia mchuano mkubwa sana kati CCM na CHADEMA kutokana na wagombea wake kuteka nyoyo za wengi na kutoa matumaini ya kuleta maisha bora kwa Mtanzania kwa kipindi cha miaka mitano endapo watawapa ridhaa ya kuwaongoza.
CCM ilimsimamisha Jakaya Kikwete wakati CHADEMA iliwakilishwa na Dk. Willbrod Slaa ambaye alikuwa akipata mapokezi makubwa wakati wa kampeni zake.
Umati mkubwa uliokuwa ukimlaki mgombea huyo, uliwafanya CCM kupata kiwewe na kuamini kuwa hali haikuwa kama ilivyotarajia kabla ya kampeni kuanza.
Huu umati uliokuwa ukijitokeza katika mikutano ya kampeni za wagombea wa udiwani, ubunge na urais ndiyo hasa msingi wa mada yangu leo.
Nimehudhuria mikutano mbalimbali ya wagombea kwa nafasi za urais na kwa haraka haraka niligundua kuwa kuna haja ya kubadili sheria ya uchaguzi kuhusu umri unaostahili kwa mpiga kura.
Ibara tajwa hapo juu inasema Every Citizen who has attained 18 years is entitled to vote in any election. Maana yake Kila raia aliyetimiza umri wa mia 18 na mwenye akili timamu ana haki ya kupiga kura katika uchaguzi wowote.
Ni ukweli usiopingika kuwa wengi wanaohudhuria katika mikutano hiyo ni vijana wa chini ya umri wa miaka 18 ambao kimsingi sheria ya uchaguzi haiwaruhusu kushiriki kupiga kura kwa kiongozi wanayemtaka.
Sheria hiyo inamtambua kama mtoto asiyekuwa na ufahamu mzuri wa mambo na hivyo hawezi kutoa uamuzi sahihi wa kura yake.
Sheria hii imepitwa na wakati na kwa hali hiyo inatakiwa kubadilishwa ili iendane na mazingira halisi ya Mtanzania wa sasa. Mabadiliko hayo yazingatie umri wa kuishi (life expectance) wa Mtanzania kwa sasa ambao ni kati ya miaka 47 na 50.
Nikirejerea nyuma kidogo wakati sheria hii inatungwa (1977), yawezekana ilizingatia zaidi umri wa kuanza na kumaliza elimu ya msingi ambayo kipindi hicho ilikuwa ya lazima. Lakini pia kumaliza elimu ya sekondari.
Kwa wakati huo haikuwa rahisi kwa mtoto kuanza darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka mitano ama sita kama ilivyo sasa.
Tume ya uchaguzi kwa wakati huo yawezekana kabisa iliamini kuwa mtu mwenye akili timamu na mwenye uwezo wa kupiga kura ni yule ambaye ana umri wa kuwa sekondari, hata kama hakubahatika kusoma.
Kama elimu ya sekondari ndiyo ilikuwa kigezo cha mtu kupiga kura kwa wakati huo, basi kwa sasa hali ni tofauti kabisa, kwani umri wa kwenda shule umebadilika mno.
Sasa umri wa kwenda shule ni kati ya miaka mitano hadi saba kitu ambacho kinafanya watoto hawa kuhitimu Elimu ya msingi wakiwa na umri wa miaka 11 hadi 13. Na kwa mantiki hiyo basi umri wa kuanza sekondari ni kati ya mika 12 na 14.
Kwa mtazamo wangu, katika kipindi hiki cha vuguvugu la mabadiliko ya Katiba, napendekeza suala la umri wa mpiga kura uangaliwe upya.
Mfanye haya kwa kuzingatia umri wa kuishi wa Mtanzania ambao kwa sasa umekadiriwa kuwa ni chini ya miaka 40, fikirieni pia mabadiliko ya kimaumbile ya vijana ambao wanaonekana wazee hali wakiwa.
Pia zingatieni kuwa kijana ni taifa la leo na mtoto ni nguvu kazi mbadala.