Ukuu wa chama ndiyo tatizo la Tanzania

Kigarama

JF-Expert Member
Apr 23, 2007
2,492
1,230
Ukiziangalia kwa undani sana siasa za Tanzania ni kama vile ni siasa za kurithi mifumo toka kurithi mfumo wa Kikoloni kulikofanywa na Serikali ya Tanganyika huru chini ya chama cha TANU, na urithi wa katiba za vyama vingi toka katiba ya zamani ya CCM pamoja na mifumo yake. Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mbali ya kubadili majina ya nchi hizo mbili na kuwa Tanzania kila kitu katika kuendesha Tanzania mpya kiliegema kwenye Katiba iliyorithiwa toka kwa Wakoloni.

Bahati mbaya TANU na ASP zilipoungana na kuundwa CCM, chama kipya kilirithi tabia mbili mbaya toka vyama asisi. CCM ililirithi ubabe na urasimu wa umilikaji siasa za nchi toka kwenye vyama hivyo. Kwa bahati mbaya sana vyama vingine vilivyoanzishwa baada ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa mwaka 1992 vilitohoa au kunakili katiba ya CCM ya mwaka 1977.

Leo tunapoona Ukuu wa chama (Party Supremacy) kwenye maisha ya kila siku kwenye siasa zetu ni lazima tujue inatokana na vyama vyetu kurithi tabia ya kutukuza chama toka CCM. Kuna wakati ndani ya CCM kauli mbiu ya " hakuna mtu maarufu kuliko chama" ilishamiri, kauli mbiu iliyotumika kugandamiza mawazo huru ya wanachama ndani ya chama hicho.

Leo ni vigumu sana ndani ya vyama vyetu kupingana kimawazo na wakuu wa chama kwa sababu kwa tafsiri rahisi iliyorithiwa toka CCM, wakuu wa chama ndiyo chama chenyewe. Kupinga mawazo ya wakuu wa chama inachukuliwa kama ni Uasi au hujuma dhidi ya chama.

Hali hii imejenga tabia ya wanasiasa wetu kujipendekeza kwa wakuu wa chama ili waendelee kuwemo kwenye siasa za kichama, na maamuzi mengi yanayofanywa na viongozi wa chama hufanywa bila ya kujali kama athari zake zina madhara hasi kiasi gani kwa wanachama wengine.

Tabia hii ya ukuu wa chama ambayo ni ukuu wa viongozi wa chama, huua au kuviza mawazo mapya toka kwa wanachama wa kawaida kwani kama mawazo ya wanachama hao si njozi ya viongozi wa chama basi huchukuliwa kama ni kitu kisichotakiwa kuwepo. Tatizo letu kama Taifa ni kuendeleza kutukuza ukuu wa chama ambao njia pekee ya kuumaliza ni kuruhusu wagombea huru kwenye chaguzi za kitaifa!!
 
Back
Top Bottom