Ukurasa wa 383: Miaka kumi ijayo

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Miaka kumi ijayo hutajivunia ni kwa haraka kiasi gani ulikuwa unajibu jumbe za simu unazotumiwa, au kupokea kila simu iliyokuwa inapigwa.

Miaka kumi ijayo hutajivunia ulikuwa kwenye makundi mangapi ya wasap, huenda hata kipindi hiko isiwepo kabisa...

Miaka kumi ijayo hutajivunia ni mitandao mingapi ya kijamii umetumia, na ipi mipya uliwahi kuingia haraka...

Miaka kumi ijayo hutajivunia ni habari kiasi gani umefuatilia, umejua kila kinachotokea, nani kamuua nani, au kambaka nani...

Miaka kumi ijayo hutajivunia kujua maisha ya wasanii yameendaje, nani anatembea na nani, na msanii gani analipwa sana.

Miaka kumi ijayo hutajivunia round za bia ulizozungusha, ulipokuwa na marafiki kwenye baa.

Miaka kumi ijayo hutajivunia kuwa shabiki namba moja wa timu fulani, au kwa jinsi gani kocha wa timu unayoshabikia alivyokuudhi...

Miaka kumi ijayo utajivunia ni kitu gani kikubwa umefanya kwenye maisha yako, kinachokunufaisha wewe na wanaokuzunguka pia.

Miaka kumi ijayo utajivunia biashara uliyoanza, na wengi wakasema huwezi, lakini ukapambana na hatimaye kusimamisha biashara imara.

Miaka kumi ijayo utajivunia kufanyia kazi kipaji chako, iwe ni mchezo, uandishi, kuigiza au chochote na ukafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Miaka kumi ijayo utajivunia kwa kuona maisha yako yamekuwa bora zaidi, umeondoka kwenye utegemezi wa chanzo kimoja na madeni na umeweza kutengeneza vyanzo vingi vya kipato.

Sikukatazi kwamba usifanye mambo ambayo yanakupa starehe, bali nakukumbusha kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako, ambayo yatafanya maisha yako na ya wanaokuzunguka kuwa bora zaidi.

Na pia nikukumbushe miaka kumi ijayo siyo mingi kama unavyofikiri, kumbuka Raisi Kikwete aliingia madarakani lini na sasa ameshatoka, je unaweza kujilinganisha hali yako ya maisha wakati anaingia na wakati anatoka? Miaka kumi ni michache sana, AMKA sasa na weka juhudi kuboresha maisha yako.

SOMA; Kushindwa Kunapatikana Sehemu Moja Tu, Na Kwa Bahati Nzuri Haupo Sehemu Hiyo.

TAMKO LANGU;

Nimejikumbusha ya kwamba mambo mengi ninayokazana kufanya sasa, miaka kumi ijayo sitaweza kujivunia nayo. Badala yake maisha yangu yatazidi kuwa hovyo sana. Kuanzia sasa nitaweka kipaumbele kwenye yale mambo ambayo ni muhimu zaidi kwangu na ambayo miaka kumi ijayo nitajivunia kwa kuchukua hatua leo.

NENO LA LEO.

It's better to look ahead and prepare, than to look back and regret.

Jackie Joyner-Kersee

Ni bora kuangalia mbele na kujiandaa, kuliko kuangalia nyuma na kujutia.

Angalia mbele miaka kumi na ujiandae leo na kuchukua hatua ili miaka kumi ijayo usije kuangalia nyuma na kujutia muda uliopotea.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.
 
Back
Top Bottom