Ujambazi unarejea kwa kasi, tuamke

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,293
33,078
KATUNI%28189%29.jpg

Maoni ya katuni.



Kuna kila dalili kwamba ujambazi unarejea kwa kasi hasa kwenye maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya watu kuvamiwa majumbani usiku na hata maeneo ya biashara kama ilivyotokea huko Vingunguti Faru usiku wa kuamkia juzi.
Katika tukio la Vingunguti, mbali ya majambazi hao kufunga mtaa na kuendesha uhalifu wao wa kupora duka moja baada ya jingine, pia waliua raia wawili kwa kuwapiga risasi. Tunawapa pole wote walioguswa na vifo hivyo, tunaomba ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu hao wawe na subira katika kipindi hiki kigumu cha kupoteza wapendwa wao.
Tunatambua wazi kwamba ujambazi ni uhalifu wa kiwango cha juu ambao kwa kweli nguvu kubwa zaidi inahitajika kukabiliana nao. Nguvu hii ni walinzi wa usalama ambao wamefuzu vizuri kwa kuwa mara nyingi majambazi hujihami kwa silaha nzito.
Tunajua na kutambua kwa dhati kabisa kwamba kazi ya kukabiliana na majambazi si nyepesi hata kidogo, pia tunajua kwamba polisi wanajitahidi kutimiza wajibu wao katika maeneo mengi.
Hata hivyo, tunaamini kwamba pamoja na mafanikio mengi ambayo polisi wamefanikiwa kuyafikia katika kukabili uhalifu, hususan ujambazi, bado kuna kila sababu ya kuendelea kukaza uzi ili kufanya vitendo kama hiki cha Vingunguti Faru kuwa ni mambo yasiyosikika kabisa katika miji yetu.
Tunasema haya kwa sababu kuna taarifa kwamba katika baadhi ya mitaa ya Mbezi Juu Ndumbwi nje kidogo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam, wakazi wake wamekuwa Wakiendesha ulinzi kwa kujilinda wenyewe kwa kuwekeana zamu baada ya kukithiri kwa matukio ya ujambazi, huko nyumba zao zimekuwa zikivamiwa moja baada ya nyingine na vifo vimeripotiwa huko.
Tunaelewa kwamba Jiji la Dar es Salaam limezidi kupanuka siku hadi siku hali ambayo pia inahitaji kupanuka kwa huduma muhimu kwa ajili ya usalama wake. Ni kwa njia hiyo mkoa wa Dar es Salaam uligeuzwa kuwa kanda maalum ya kipolisi ikiwa na mikoa mitatu ya kipolisi.
Nia ya mabadiliko hayo ya kiutawala ilikuwa na bado inaendelea kuwa, kuimarisha utendaji wa polisi katika maeneo yote ya mkoa huo, hatua hizo kama ambavyo tumekwisha kusema mara nyingi, tulizipokea na kuzipongeza tukijua kwamba hali ya usalama kwa wakazi wa Jiji hilo itaimarika zaidi.
Kweli, awali kulikuwa na mabadiliko makubwa, na tumeendelea kuona mabadiliko hasa tunapoona polisi wanaotumia pikipiki wakilinda doria mitaani; pia tumeona ongezeko la trafiki barabarani ambao wanajitahidi kila siku iendayo kwa Mungu kuongoza magari barabarani ili kupunguza msongamano ambao umekuwa kero kubwa.
Kukomesha ujambazi ni changamoto nzito ambayo pamoja na ugumu wake ni lazima ionekene ikifanyiwa kazi inavyopaswa. Ni kwa maana hiyo tunaamini kwamba pamoja na yote ambayo Jeshi la Polisi limefanya, kuunda kanda maalum ya polisi Dar es Salaam; kuanzisha polisi jamii; kuongeza doria za askari wa pikipiki na mambo mengine mazuri, tunaona kwamba bado hatua zaidi zinastahili kuchukuliwa.
Hatua hizi kwa mfano ni kuongeza vitendea kazi kwenye vituo vidogo ambavyo vimeenea kila kona ya miji yetu. Umma ungependa kuona polisi wapo karibu zaidi na wananchi katika makazi yao, wanapohitajika wanapatikana kwa wakati, lakini muhimu zaidi wanapatikana wakiwa na vitendea kazi vya kuweza kuwadhibiti majambazi.
Ndiyo maana kila tunapotafakari hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam na kuzidi kupanuka kwa eneo lake na tukitafakari vitendo hivi vya ujambazi tunafikia hitimisho la kutoa changamoto kwa polisi ili izidi kujipanga kwa njia ambayo itawasogeza karibu zaidi na wananchi, lakini la umuhimu zaidi juhudi zifanyike kuongeza vitendea kazi kwenye vituo vilivyo ndani kabisa kwenye makazi ya wananchi ili kufanikisha malengo ya polisi jamii kufikiwa.



CHANZO: NIPASHE
 
Ila kwetu matukio haya huwa mengi kulekea X-mass na mwaka mpya, mwenyewe unaweza kuhisi wahusika, i.e. waharifu! Lakini nikilinganisha na matukio ya ujambazi kabla ya uchaguzi mkuu 2005 naona kama yanafanana na ya sasa hivi na yatachukua kasi kubwa mpaka uchaguzi mkuu upite; ni kama vile ni namna ya kukusanya pesa za uchaguzi!
 
Back
Top Bottom