Elections 2010 Uhuni huu kwenye uchaguzi haukubaliki

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,268
33,040
Katuni%283%29.jpg

Maoni ya katuni



Wakati wa mchakato wa uchaguzi, kuanzia kura za maoni, uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura na kutangazwa kwa washindi, kumekuwa na kawaida ya kuibuka kwa vituo vya aina mbalimbali.
Miongoni mwa vituko hivi ni staili za wagombea za kuomba kura, wapo wanaopiga magoti wakiomba kura, wengine wakimwaga shikamoo kwa watoto, wapo wanaomwaga machozi, lakini pia wapo ambao huibuka na ahadi ambazo hadi mwisho wa dahari hazitatekeleza. Yote haya ni mbwembwe na bashasha za uchaguzi.
Lakini kuna hili moja, baya, chafu na ambalo katu halipendekezi, hili ni la kuleta vurugu katika kampeni. Tunasema kwa mdomo mpana kabisa kwamba halikubaliki kwa sababu zozote zile.

Tumesikia, tumeandika na hata leo tuna habari za wafuasi wa vyama vya siasa kufanya vurugu. Hawa wanapiga wenzao, wanavamia mikutano ya vyama vingine, wanachana bendera na picha za wagombea wa vyama vingine. Kwa kifupi wanaendesha uhuni mbaya mno. Hali hii imeshuhudiwa Kwimba, Mwanza; Bariadi, Shinyanga; Morogoro Kusini, Morogoro; Vunjo, Kilimanjaro; kutaja kwa uchache tu.

Tunajua wanaofanya vitendo hivi ni wahuni. Hawa si washabiki au wafuasi wa vyama, mara nyingi ni watu wanaohongwa pombe na vijisenti ili kuvuruga mikutano ya wapinzani wao kwa kuwa tu wameona mambo ya wenzao yanakwenda vizuri.

Tunajua miongoni mwa maadili ya uchaguzi ambayo vyama vya siasa vilisaini ni pamoja na kufanya kampeni za kistaarabu kwa amani na utulivu, kutokuharibu mali au aina yoyote ya utambulisho wa wagombea na vyama vyao, kwa maana ya bendera, picha na hata mabango mengine yoyote yanayotambulisha chama cha siasa.

Kila hatua katika mchakato wa uchaguzi ni muhimu, ili uchaguzi uwe huru na wa haki pamoja na mambo mengine unatakiwa uendeshwe katika mazingira ya uhuru, wanachama na wagombea wao wawe huru kunadi sera zao, wananchi nao wawe huru kufika katika mikutano ya kampeni kuwasilikiza wagombea na sera zao ili mwishowe waamue nani wa kumpigia kura.

Kitendo cha kukodisha wahuni kwa nia ovu ya kuvuruga mikutano ya kampeni ya vyama vingine, au kitendo chochote cha kuharibu picha, mabango au bendera za vyama vingine, ni vitendo vinavyolenga kuvuruga uchaguzi ili usiwe huru na wa haki.
Hali hii kamwe haikubaliki, haiwezi kukubalika na sisi tunaikataa na kuwataka wote wanaitakia nchi hii mema waikatae na kuungana nasi kuwalaani wote wanaohusika na uhuni huu mbaya.

Pamoja na kulaani, tunaamini vyombo vya dola vipo, sheria za kuwashughulikia wahuni hawa zipo, sababu na nia ya kuwashughulikia ipo, na mara nyingi ushahidi wa wazi kabisa upo wa kuwafikisha mahakamani ili kuwaondoa uhuni katika fikra zao kwa kuwapa adhabu kali zinazostahili ili iwe fundisho kwao na wale wote wanaoota kufanya uhuni kama huo.
Ni kwa maana hii tunaomba mamlaka zifuatazo, Jeshi la Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), waingilie kati uhuni huu kwa kuwashughulikia wote walioshiriki vitendo hivi.

Kama wahuni hawa hawatashughulikiwa vilivyo, kuna uwezekano wa kuambukiza tabia hiyo chafu maeneo mengine zaidi na hivyo kutumbukiza nchi katika vurugu za kijinga.
Tungependa kuwakumbusha wote, yaani wahuni wanaoleta vurugu katika uchaguzi pamoja na wote ambao ama wanawachochea au wanawalipa ili kufanya wendawazimu wao kwenye mchakato wa uchaguzi kwamba machafuko mengi katika nchi za Bara la Afrika chimbuko lake ni kwenye uchaguzi.

Tunaamini pamoja na kashoro za kisheria kwa maana ya udhaifu uliopo katika sheria zinazosimamia uchaguzi wetu, bado tumefanikiwa kuendesha chaguzi kwa amani na utulivu, ingawa kuna ulazima wa kuzitazama upya sheria hizi, tungependa kuona wote wanaotaka kututumbukiza katika zahama ya machafuko wanadhibitiwa na kuadhibiwa vilivyo. Tuwakatae wahuni hawa na wote wanaowatuma.



CHANZO: NIPASHE
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom