Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,316
- 33,125
WANASAYANSI nchini wako katika hatua za mwisho kukamilisha kinga ya ugonjwa wa malaria baada ya utafiti kuonyesha kuwa chanjo mpya iitwayo RTS,S ambayo inaweza kukinga ugonjwa huo kwa asilimia 50. Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Afya Ifakara, Dk Salim Abdulla alipokuwa akizungumza katika warsha kuhusu matokeo ya utafiti wa chanjo hiyo. Dk Abdulla alisema utafiti huo pia umeonyesha kuwa chanjo hiyo mpya inaweza kuwakinga watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kinamama wajawazito kwa asilimia 47. Tuko katika awamu ya tatu ya utafiti huo na hali inaonyesha kuwa chanjo hiyo ni salama, alisema Dk Abdulla. Dk Abdulla alisema kuwa utafiti huo umefanyika katika maeneo mawili nchini; Korogwe mkoani Tanga na Bagamoyo, Pwani. Majaribio ya utafiti huo yalihusisha watoto 3,300. Taratibu zilizotumika zilikuwa sawa na watoto walioshiriki walipata huduma bora zaidi na kulikuwa na uchache wa vifo tofauti na tafiti nyingine, alisema Dk Abdulla. Alisema kuwa chanjo hiyo pia inaweza kupunguza maambukizi ya malaria kali kwa asilimia 47 na kwa asimilia hiyohiyo kwa malaria ya kawaida. Mtoto akipata chanjo hii au mama mjamzito anaweza kupata kinga ya kutokupata malaria, alisema. Alisema watoto waliotumika katika utafiti huo walikuwa wakiangaliwa afya zao kwa asilimia 99.9 ili kufanikisha matokeo ya chanjo hiyo. Alisema awamu hiyo ya tatu ya utafiti wa chanjo hiyo ni ya mwisho kabla dawa kuanza kusambazwa nchini kwa ajili ya matumizi. Awali, akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando alisema wajibu mkubwa wa Serikali katika kupambana na malaria ni kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa huduma zote za kinga na tiba. Ugonjwa wa malaria unaweza kukingwa na mojawapo ya njia madhubuti ni kutumia chanjo, alisema Dk Mmbando. Alisema takwimu kutoka vituo vya huduma za afya nchini zinabainisha kuwa takribani watu 20,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria na wengi wanaofariki ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kina mama wajawazito. Hata hivyo, utafiti unaonyesha kuwa asilimia 60 hadi 80 ya vifo hutokea nyumbani kabla ya wagonjwa kufikishwa katika vituo vya afya, hivyo idadi halisi ya vifo vinavyotokana na malaria ni zaidi ya 80,000 kila mwaka, alisema. Alisema kutokana na hali hiyo ni dhahiri kuwa chanjo hiyo mpya imekuja wakati mwafaka na itasaidia kukabiliana na tatizo hilo sugu na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria. Dk Mmbando alisema upatikanaji wa chanjo hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kupambana na malaria, ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo nchini. Hatuna sababu ya ugonjwa wa malaria kuendelea kututesa na kudhoofisha maendeleo ya nchi yetu. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kupambana na malaria katika nafasi yake. Alisema pamoja na upatikanaji wa kinga hiyo, bado njia zilizokuwa zikitumika kukabiliana na malaria zitaendelea kutumika. |
Chanzo: Ugonjwa wa malaria sasa wapata chanjo