Ugonjwa wa malale (trypanosomiasis/sleeping sickness)

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125

Ugonjwa wa malale ambao kwa kitaalamu hujulikana kama Human African Trypanosomiasis au African lethargy au sleeping sickness na Congo Trypanosomiasis ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinajulikana kama Trypanosome.Kuna aina tatu kuu za Trypanosome ambazo huathiri binadamu nazo ni;


I.Trypanosoma brucei gambiense (T.b.g.)-Hupatikana Afrika magharibi na Afrika ya Kati na husambaa hadi kwenye nchi za Uganda, Kenya na huchangia kwa asilimia 95 ya maambukizi yote ya ugonjwa wa malale.II.Trypanosoma brucei rhodesiense (T.b.r.)-Hupatikana katika nchi za

Afrika Mashariki na zile zilizo kusini mwa bara la Afrika na huchangia asilimia 5 tu ya maambukizi yote ya ugonjwa wa malale

III.Trypanosoma cruzi-Hupatikana katika nchi za Amerika ya kati na Amerika kusini na husababisha ugonjwa unaojulikana kama American trypanosomiasis au Chagas disease.

Watu 50,000-70,000 wanakisiwa kuambukizwa ugonjwa huu ingawa maambukizi yamepungua katika miaka ya hivi karibuni.Mwaka 2009, maambukizi yalikuwa 10,000 ambapo katika taarifa ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya Januari mwaka 2012, limesema, maambukizi haya chini ya elfu kumi ni ya kwanza kuripotiwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Maambukizi 7,319 yaliripotiwa mwaka 2010.Ugonjwa huu wa malale umeua watu 48,000 mwaka 2008.


Mzunguko wa maisha ya Trypanosome


Vimelea vya Trypanosome huhifadhiwa na kusambazwa na wadudu wanaojulikana kama Mbungo (Tse tse fly). Mbungo hupatikana kwa wingi kwenye nchi za kusini mwa janga la Sahara.


Wadudu hawa wakati ambapo wanafyonza damu kwenye mwili wa mtu, huingiza vimelea vya trypanosome kwenye ngozi ya mtu ambavyo kwa wakati huo hujulikana kama metacyclic trypomastigotes. Baada ya kuingia kwenye mwili wa binadamu kupitia kwenye ngozi,metacyclic

trypomastigotes husambaa hadi kwenye mfumo wa limfu (lymphatic system) na mfumo wa damu ambapo hubadilika na kuwa bloodstream trypomastigotes ambao huenea mpaka kwenye uti wa mgongo,lymph na huendelea kuzaliana kwa mfumo wa binary fusion.


Mbungo huambukizwa bloodstream trypomastigotes wakati wanafyonza damu kutoka kwenye mwili wa mtu au wanyama (kwa tryponosome brucei rhodesiense) kama ngombe na wanyama wa mwituni. Ndani ya mwili wa Mbungo, bloodstream trypomastigotes hubadilika na kuwa

procyclic trypomastigotes wanapofika kwenye koo ya Mbungo na kuzaliana kwa mfumo uleule wa binary fusion na hatimaye huingia kwenye hatua ya mwisho inayojulikana kama epimastigotes kwenye tezi za mate(salivary glands) ambapo husubiri mpaka pale mbungo atakapomngata

binadamu ili afyonze damu. Mzunguko huu wa maisha ya vimelea hivi huchukua takribani wiki tatu.


Mbali na kungatwa na mbungo, ugonjwa wa malale pia huweza kuambukizwa kwa njia zifuatazo;

•Maambukizi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto wake kutokana na vimelea hivi vya trypanosome kuwa na uwezo wa kuvuka ukuta wa kondo la uzazi (placenta barrier)
•Maambukizi kwa wafanyakazi wa maabara,hospitali ambao kwa njia moja au nyingine wamegusa damu yenye maambukizi ya vimelea hivi vya trypanosome.
•Maambukizi kwa wagonjwa ambao wamewekewa damu isiyokuwa salama
•Kwa njia ya kujamiana (kujamiana na mtu ambaye ameambukizwa vimelea vya ugonjwa wa malale)

Dalili na viashiria vya ugonjwa wa malale


Dalili ya kwanza ni maumivu makali yanayotokana na kungatwa na mdudu aina ya Mbungo. Sehemu ambayo imengatwa na Mbungo huwa nyekundu (inflamed) na kama mtu atakuwa amepata maambukizi ya ugonjwa wa malale baada ya kungatwa na Mbungo basi maumivu hujirudia tena baada ya siku 10 na sehemu ile huvimba (‘trypanosomal chancre’) na tezi zilizokaribu na sehemu hiyo iliyongatwa huvimba (‘Winterbottom sign’).


Ndani ya wiki 2-3, vimelea vya trypanosome huingia kwenye mfumo wa damu.

Dalili za ugonjwa huu hutokea kwa awamu mbili;
•
Awamu ya kwanza hujulikana kama haemolymphatic phase na huambatana na homa kali, maumivu ya mifupa,kichwa kuuma na kuwashwa mwili. Kuathirika kwa mfumo wa lymph (lymphatic system) na wa damu huambatana na kuvimba sana kwa tezi. Kuvimba kwa tezi nyuma ya shingo hutokea (‘winterbottom sign’) na kama mgonjwa hatapata tiba, kinga ya mwili huzidiwa nguvu na ugonjwa huu na hivyo kusababisha kuathirika kwa figo, moyo (myocarditis), mapafu kujaa maji, (pleural effusion), ugonjwa wa ini (hepatitis),upungufu wa damu mwilini (anemia),na kuathirika kwa mfumo wa homoni (endocrine system).


•Awamu ya pili inayojulikana kama neurological phase, hutokana na kuathirika kwa mfumo wa fahamu kutokana na vimelea vya ugonjwa wa malale kuwa na uwezo wa kuvuka kinga ya ubongo (blood brain barrier) ambapo ndio jina la ugonjwa wa malale (sleeping sickness) linapopatikana kwani mgonjwa huwa na dalili za mtu kuchanganyikiwa, kuharibika kwa utaratibu wa kulala (mtu kutopata usingizi usiku na

kulala wakati wa mchana), uchovu. Iwapo mgonjwa hatapata tiba wakati huu, basi mgonjwa huweza kupata ugonjwa wa akili pamoja na kupoteza fahamu au kuingia kwenye koma (coma). Kuathirika kwa mfumo wa fahamu hakuwezi kurekebishika na mgonjwa hudumu na hali hiyo kwa kipindi chote cha maisha yake yote. Hali ya kuhisi usingizi kila wakati hutokana na kemikali aina ya Tryptophol inayotolewa na vimelea vya ugonjwa wa malale.


Maambukizi ya Trypanosome brucei rhodesiense huwa ya ghafla na hatari sana kuliko ya Trypanosome brucei gambiense na mgonjwa huweza kufariki kabla hajaingia kwenye awamu ya pili (‘neurological phase’).Iwapo maambukizi haya ya Trypanosome brucei rhodesiense sio makali,

mgonjwa huingia kwenye awamu ya pili ya neurological phase na hatimaye hupoteza fahamu au huingia kwenye koma (coma).

Maambukizi ya Trypanosome brucei gambiense, huwa sio makali kwani yanaweza kutokea taratibu kwa muda wa mwezi au baada ya miaka mingi, ambapo mgonjwa atakuwa anapata homa za mara kwa mara,kuvimba ini na bandama (spleen), kuvimba tezi ambazo huwa ngumu,ndogo (discrete),zinazoteleza (rubbery), zisizokuwa na maumivu. Ikiwa mgonjwa hatapata tiba,baada ya miezi kadhaa mgonjwa ataingia kwenye awamu ya pili ya neurological phase.

Vipimo vya uchunguzi


1.Serology tests (wb-CATT,wb-LATEX, micro-CATT)-Vipimo vya damu vinavyotumika kuangalia maambukizi ya Trypanosome brucei gambiense tu pamoja na kuangalia dalili ya kuvimba tezi za shingo.


2.Vipimo vya uti wa mgongo (Cerebrospinal fluid tests)-Kipimo cha kuangalia maji ya uti wa mgongo, kiwango cha protini kitakuwa juu na kiwango cha sukari kitapungua.Kupatikana kwa kiwango kikubwa cha IgM au kuonekana kwa IgM kwenye maji ya uti wa mgongo wakati wa kufanya kipimo cha antibody test, kunaashiria uwepo wa maambukizi wa ugonjwa wa malale.


3.Complete Blood Count-Kipimo cha kuangalia wingi wa damu pamoja na chembechembe tofauti za damu.


4.Lymph node aspiration-Kipimo kinachofanywa kwa kuchukua kipimo kutoka kwenye tezi iliyovimba na kuangaliwa maabara kwa kutumia hadubini kama kuna maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa malale au la.


Tiba ya ugonjwa wa malale


Tiba ya ugonjwa huu hutolewa bure kulingana na hatua ya ugonjwa wa malale.

Mgonjwa aliye kwenye hatua ya kwanza (Haemolymphatic phase) hutibiwa kwa dawa aina ya Pentamidin au Suramin. Dawa hizi hazina madhara sana na ni rahisi kutumiwa.

Mgonjwa aliye kwenye hatua ya pili (Neurological phase) hutibiwa kwa kutumia Melarsoprol, Eflornithine (ambayo ni ya uhakika dhidhi ya Trypanosome brucei gambiense tu), pamoja na tiba ya mchanganyiko wa nifurtimox na eflornithine.Dawa hizi zina madhara na matumizi yake

yanahitaji uangalifu mkubwa na umakini. Melarsoprol husababisha madhara ya ubongo yajulikanayo kama reactive encephalopathy (encephalophatic syndrome) ambayo huweza kusababisha kifo kwa asilimia 3-10.

Bila tiba, mgonjwa wa ugonjwa wa malale huweza kufariki ndani ya miezi sita kutokana na kuathirika moyo (cardiac failure) au kutokana na maambukizi ya Trypanosome brucei rhodesiense yenyewe.

Kinga ya ugonjwa wa malale



Kuna hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa ili kukinga watu dhidhi ya maambukizi ya ugonjwa huu wa malale, hatua hizo ni;

I.Kutokomeza na kuangamiza kabisa wadudu aina ya Mbungo ambayo hupunguza maambukizi ya ugonjwa huu.Pia kwa kutumia wadudu tasa (sterile insect technique) iliyobuniwa na wanasayansi Dr. Raymond C. Bushland and Dr. Edward F. Knipling.Wadudu hawa(mbungo wa kiume)

ambao wamefanywa tasa kwa kutumia mionzi (radiation), huachiwa kwenye eneo linaloaminika kuwa na mbungo wengi wa kike,hivyo mbungo hawa tasa (wa kiume), wanapojamiana na mbungo wa kike, matokeo yake ni kuwafanya mbungo wa kike kushindwa kuzaa na hivyo kupunguza kiwango cha mbungo na maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa malale.


II.Ufuatiliaji wa mara kwa mara wa kuangalia uzalianaji wa Mbungo pamoja na udhibiti wake,ugunduzi wa ugonjwa wa malale na tiba ya uhakika ya maambukizi mapya ya ugonjwa huu ni kati ya hatua muhimu za kukabiliana na ugonjwa huu wa malale.


III.Kufanya kliniki au medical camps zitakazofanya uchunguzi dhidhi ya ugonjwa wa malale(screening test) bure kwa jamii zilizokwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu


IV.Kuepuka kufanya ngono na mtu ambaye ameathirika kwa ugonjwa huu pamoja na kuacha kufanya ngono zembe (bila kinga) hasa kwa jamii inayoishi kwenye maeneo ambayo ugonjwa huu hupatikana kwa wingi (endemic areas)


V.Wasafiri wanaokwenda kwenye maeneo yenye ugonjwa wa malale,kuhakikisha wanafanyiwa uchunguzi wa kina mara tu wanaporudi kutoka maeneo hayo


VI.Mama mjamzito anayeishi kwenye maeneo ambayo ugonjwa wa malale hupatikana,kuhakikisha anahudhuria kliniki na kufanyiwa uchunguzi wa kina na kama ameambukizwa kutibiwa ili asihatarishe afya yake pamoja na ya mtoto.
Ugonjwa wa Malale (Trypanosomiasis/Sleeping Sickness)
 
Back
Top Bottom