Ufisadi wapamba moto Monduli kwa Lowassa; Waathiri ujenzi wa ofisi yake ya ubunge kugharimu sh.200M

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Paul Sarwatt
Arusha
27 Jul 2011
Toleo na 196
  • Waathiri ujenzi wa ofisi yake ya ubunge
  • Umepangwa kugharimu Sh. milioni 200
  • Wawili wasimamishwa kazi, wengine washushwa vyeo
TUHUMA za ufisadi zimeitikisa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha na kusababisha miradi kadhaa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa ofisi za Mbunge wa jimbo hilo na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kusimama kwa muda.

Taarifa za kuwepo kwa ufisadi katika miradi kadhaa ya maendeleo; hasa ya unjezi wa shule, zahanati na ofisi ya mbunge ziliibuliwa wiki iliyopita katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmshauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.

Kutokana na tuhuma hizo, baraza hilo limeagiza Kamati ya Fedha,Utawala na Mipango, kuwasimamisha kazi mara moja watumishi wawili wa Halmashauri hiyo na pia kuwashusha cheo wengine wawili kutokana na kuhusika kwao na tuhuma kadhaa za ufisadi.

Waliopendekezwa kusimamishwa kazi mara moja ni pamoja na Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Sylivester Chinengo na Meneja wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Monduli, Kanaeli Pallangyo.

Kwa mujibu wa maelekezo ya Baraza la Madiwani, maafisa walioshushwa vyeo vyao na kuwa watumishi wa kawaida ni Afisa Ardhi, Kitunda J. Mkumbo na Afisa Ugavi wa Halmashauri hiyo, Mangwala Kilanga. Wote tayari wameanza kutumikia adhabu hiyo.

Akitoa tuhuma dhidi ya Mhandisi wa Halmashauri wakati akichangia katika kikao cha baraza hilo, Diwani wa Kata ya Monduli Mjini, Isaack Joseph, alieleza kusikitishwa kwake na hatua ya mhandisi huyo kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa madarasa, majosho, nyumba za walimu na uwekaji uzio wa Halmashauri na soko la Monduli.


Diwani huyo alieleza kuwa mhandisi huyo wa Halmashauri anahusika na uzembe na usimamizi mbovu katika ujenzi wa ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambapo hadi sasa Shilingi milioni 40 zimeshatumika, lakini fedha hazilingani na thamani ya kazi iliyofanyika.


Ujenzi wa ofisi hiyo ya Mbunge Lowassa ulipangwa kugharimu Shilingi milioni 200. Mradi huo unatekelezwa na Serikali ambapo pia utahusisha ujenzi wa ofisi kama hiyo kwa Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, katika jimbo lake mkoani Rukwa ikiwa ni mpango wa Serikali kuwajengea ofisi nzuri mawaziri wakuu wastaafu katika majimbo yao.


“Ujenzi huo umefanywa chini ya kiwango na hali hiyo inaonekana kwa macho ya kawaida. Kuta zote za jengo zimepinda na kuta za ndani hazijaunganishwa kabisa; ilhali katika mahesabu inaonyesha kiasi cha Shilingi milioni 40 zimeshatumika na kwamba mkandarasi aliyehusika ameshalipwa”, alieleza Isaack.


Diwani huyo aliongeza: “Mhandisi ameridhia malipo kwa majengo ambayo yamejengwa chini ya viwango vya kawaida na sisi kama wawakilishi na wasimamizi wa fedha za umma hatuwezi kukubaliana na uzembe wa aina hiyo”, alisema diwani huyo.


Tuhuma nyingine, kwa mujibu wa Isaack, ni hatua ya mhandisi huyo kuhusika na uzembe katika ujenzi wa josho la kijiji cha Mswakini ambapo Shilingi milioni 20 zilitumika; huku ukuta wa josho ukiwa umejengwa kwa tope badala ya saruji.


“Haiwezekani Shilingi milioni 20 zitumike kwa ujenzi wa josho ambalo matofali yameunganishwa kwa tope badala ya saruji na fedha nyingi kiasi hicho zimetumika na malipo yamefanyika”, alieleza.


Tuhuma nyingine kwa mujibu wa diwani huyo ni malipo ya Shilingi milioni 14 kwa ajili ya kuweka nyaya za kuzuia wezi kuzungushia juu ya ukuta wa majengo ya Halmashauri na matumizi mengine ya Shilingi milioni 13 kuweka uzio katika eneo la soko.


“Katika ujenzi wa miradi hiyo miwili, BOQ (Bill of Quantity) haionyeshi kiwango cha fedha zilizotumika katika ununuzi wa vifaa; hali inayotia mshaka kuwa kuna njama za kufuja fedha za Halmashauri”, alieleza diwani huyo huku akishangiliwa na madiwani wenzake.


Ujenzi wa majengo mengine unaolalamikiwa ni ule wa mabweni mawili ya Shule ya Msingi Mferejeni yaligharimu Shilingi milioni 100 na ujenzi wa nyumba kadhaa za waalimu uliogharimu Shilingi milioni zaidi ya 80.


Kwa upande wa tuhuma zinazomkabili Meneja wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Monduli, Kanaeli Pallangyo, ni pamoja na kushindwa kukusanya madeni ya maji ya kiasi cha Shilingi milioni 60 kutoka kwa wadaiwa sugu, na hivyo mamlaka hiyo kukosa uwezo wa kujiendesha na kukatiwa umeme katika mitambo ya kusukuma maji kutokana na kushindwa kulipa gharama za umeme wa TANESCO kwa muda mrefu.


Tuhuma nyingine ni kufanya ufisadi wa malipo hewa ya Shilingi milioni 6.5 na kufanya malipo yasiyoidhinishwa na bodi ya Shilingi milioni 14.

Tuhuma nyingine ni kushindwa kuitisha vikao vya Bodi ya Maji kwa mujibu wa sheria.

“Kwa tuhuma zote hizo, mapendekezo yetu ni wahusika hao kusimamishwa kazi hadi hapo uchunguzi zaidi juu yao utakapofanyika na hatua za kinidhamu zichukuliwe iwapo tuhuma zitathibitika”, alieleza Isaack ambapo aliungwa mkono na madiwani wenzake.


Watumishi wengine waliokumbwa na “hasira kali” za madiwani hao ni Ofisa Ardhi, Kitundu Mkumbo ambaye anatuhumiwa kukata miti zaidi ya 300 katika msitu wa asili wa Monduli bila kibali cha Halmashauri, na alipoagizwa atoe taarifa akadanganya kuwa ni miti 75; hali iliyowafanya madiwani kuunda kamati na kwenda kukagua msitu huo.


“Ofisa huyo alidanganya kikao cha Baraza na pia alishindwa kuleta taarifa ya robo ya pili ya mwaka ya mapato na matumizi ya idara yake, na hivyo kwenda kinyume na kanuni za utumishi wa halmashauri yetu”, alieleza diwani mwingine, Julius Kalanga.


Ofisa wa nne aliyepitiwa na “panga” la Madiwani hao ni Ofisa Ugavi, Mangwala Kilanga ambaye ameshushwa cheo kuwa mtunza stoo wa Idara ya Biashara katika Halmashauri hiyo.


Tuhuma zilizokuwa zinamkabili Ofisa huyo ni pamoja na fedha za manunuzi ya idara kutoingizwa kwenye leja, kuchelewesha mikataba ya ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Ole Sokoine iliyopo kijiji cha Monduli juu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 80 na pia kukaidi maagizo ya Baraza ya kuwasilisha taarifa.


“Maafisa hao wote wanaotuhumiwa wanahujumu juhudi za serikali kuwaletea maendeleo wananchi, na hivyo ni lazima Halmashauri ichukue haraka hatua za kuwawajibisha; la sivyo wananchi hawatatuelewa”, alieleza Kalanga.


Diwani huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CCM wilaya ya Monduli, alisema kuwa maafisa hao kushindwa kusimamia miradi husika ni moja ya sababu za wananchi kuichukia serikali ya CCM, na kimsingi ni haki yao; kwani kipimo cha serikali kuwajibika ni kutekeleza ilani.


“Kama hatua za kinidhamu hazitachukuliwa, maana yake ni kwamba serikali itapoteza sifa na uhalali wake machoni pa wananchi. Ni lazima fedha za miradi ambazo ni za walipa kodi zisimamiwe kwa nidhamu ya hali ya juu,” alisema.


Watumishi wengine watatu wanaotuhumiwa pia kuhusika na ufisadi huo hawakupatikana kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwao na madiwani, lakini Raia Mwema lilifanikiwa kuzungumza na Mhandisi wa Wilaya, Sylivester Chinengo, juzi, kwa njia ya simu, ambapo alikanusha tuhuma zinazoelekezwa kwake na madiwani hao.


Chinengo alieleza kuwa tuhuma hizo hazina uzito kwa kuwa si yeye aliyehusika kuwapitisha makandarasi waliohusika na ujenzi wa majengo hayo; bali ni Bodi ya Zabuni na kuongeza kuwa suala la majengo hayo kuwa chini ya viwango ni la kitaalamu zaidi na kwamba tathmini hawezi kufanywa kwa macho au na mtu asiye mtaalamu wa majengo.


“Anayeweza kuthibitisha jengo lolote kwamba lipo chini ya kiwango ni mtaalamu ambaye amesomea fani ya ujenzi, na si mtu yeyote.


Kwa hiyo, hakuna diwani anayeweza kuthibitisha kuwa majengo hayo yamejengwa chini ya kiwango isipokuwa mtaalamu, na mimi kama mhandisi sikubaliani na yale yanayozungumzwa na madiwani”, alieleza Chinengo.


Mhandisi huyo aliongeza kuwa hadi juzi alikuwa bado hajapata barua yake ya kusimamishwa kazi, lakini atajibu zaidi tuhuma hizo pindi atakapopata barua rasmi kutoka kwa mwajiri wake.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Samwel Mlay, hakupatikana kuelezea utekelezaji wa maazimio hato ya Baraza la Madiwani; kwani simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila ya kujibiwa kila alipopigiwa.

Ufisadi katika halmashauri nyingi nchini umekithiri na kuwa kikwazo kikuu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi; huku juhudi zinazofanywa na mamlaka za kiserikali kuthibiti hali hiyo zigonga mwamba mara nyingi; huku sababu kubwa ikielezwa kuwa nikujengeka kwa tabia ya kulindana miongoni mwa watumishi wa serikali wa ngazi zote.
 
Back
Top Bottom