Ufisadi wa mabilioni kama Richmond - Umeme wa dharura - Mipango ya utapeli yakwama Marekani

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Umeme wa dharura

Waandishi Wetu

ngeleja.jpg


Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja


Mipango ya utapeli yakwama Marekani

Ngeleja mikononi mwa Bunge

UTAPELI mithili ya ule wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond,ambao nusura uchote Sh bilioni 85 kupitia mpango wa Serikali wa umeme wa dharura ulioridhiwa na Bunge katika mkutano wake wa bajeti uliopita, umekwama,Raia Mwema, limethibitishiwa.

Utapeli huo ulipangwa kufanyika kupitia moja ya ahadi za Serikali bungeni katika kutatua tatizo la umeme kwa njia ya dharura. Ahadi ya Serikali ilihusisha kufanyika kwa miradi kupitia kampuni Symbion, IPTL, Aggreko International na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Kama ilivyokuwa kwa Richmond, utapeli huo pia ulipangwa kukamilishwa nchini Marekani na fedha hizo zingeliwa kupitia Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambalo ni miongoni mwa taasisi zilizoahidi kusaidia uzalishaji wa umeme wa dharura.


NSSF iliahidi kuzalisha umeme wa megawati 150 katika awamu tatu, kuanzia Septemba, Oktoba na Novemba. Hata hivyo, ahadi hiyo imeshindwa kutekelezeka katika mazingira yanayozua maswali mengi zaidi, ikiwamo mpango huo mkubwa wa utapeli.


Katika taarifa yake ya Novemba 4, mwaka huu, kuhusu ahadi yake juu ya mkakati wake wa kuondoa mgawo wa umeme nchini iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Nishati, Serikali inakiri NSSF kushindwa kukamilisha ahadi yake kwa wakati.


Sasa ombwe linalotokana na kushindwa kwa NSSF kukamilisha ahadi yake hiyo limezibwa na kampuni ya Jacobsen, ambayo awali ilipangwa kukamilisha mradi wake wa megawati 100 Julai mwakani, sasa itabidi ikamilishe Desemba mwaka huu.


Taarifa za uhakika ambazo pia zinathibitishwa na maelezo rasmi ya Serikali zinaeleza kuwa miradi karibu yote imekuwa katika mwelekeo wa kukamilika isipokuwa ule wa NSSF.


"Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilitarajiwa kuzalisha umeme megawati 50 mwezi Septemba, megawati 50 Oktoba na megawati 50 Novemba.

"Pamoja na NSSF kufanya mazungumzo ya awali na Tanesco ya kuwekeza katika ufuaji wa umeme wa megawati 150, hadi sasa mitambo husika haijapatikana.
"Kutokana na kuchelewa kupatikana kwa mitambo hiyo kwa wakati, utekelezaji wa mradi huo huenda usikamilike ndani ya kipindi cha mpango wa dharura," inaeleza taarifa rasmi ya Serikali iliyotolewa Novemba 4, mwaka huu, mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati.

Mchoro wa utapeli wakwama

Hali hiyo ya kushindikana kutimia kwa ahadi hiyo imebainika kuwa msingi wake ni mpango wa utapeli ulioandaliwa, kukwama.

Taarifa za kiuchunguzi ambazo pia gazeti hili limethibitishiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati, Januari Makamba, zinaeleza kuwa NSSF ilijiandaa kwenda kutafuta mitambo kwa kutumia timu maalumu ya watu tisa kutoka maeneo yanayohusika na nishati hiyo pamoja na dola.


Kwa mujibu wa taraifa hizo, timu hiyo ilijielekeza kwa mtu ambaye awali alitambulishwa kuwa ni mwenye kampuni na anao uwezo wa kuwauzia mitambo hiyo ya kufua umeme.


Lakini kabla ya kuelekea huko, NSSF walikuwa wamekwishakubaliana na Tanesco, pamoja na ahadi yao kutolewa rasmi ndani ya Bunge katika mkakati rasmi wa Serikali.


Timu hiyo iliondoka kwenda Marekani ambako huko baada ya kukutana na mhusika katika kuuziana mitambo, walitakiwa walipe kwa utangulizi dola za Marekani milioni 50.


"Baada ya mkutano wa Bunge wao (timu hiyo) walikwenda Marekani kwa ajili ya kuangalia hiyo mitambo, lakini ni kweli kama unavyosema waligundua kuwa mtu waliyekuwa wamekwenda kwake ni tapeli na muongo.


"Alitaka wampatie kwanza dola milioni 50 kama malipo ya utangulizi lakini wao wakagundua huyo mtu hata ofisi hana wala kampuni," alieleza Januari Makamba alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa mjini Nairobi, Jumatatu wiki hii.


Kutokana na utapeli huo mithili ya ule wa kampuni ya Richmond ambayo nayo, hasa baada ya utafiti wa iliyokuwa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harisson Mwakyembe kuwa haikuwa kampuni inayojihusisha na masuala ya umeme nchini Marekani, safari hii, utapeli huo umegonga mwamba.


Ni kwa sababu hiyo, Januari Makamba amelieleza gazeti hili kuwa NSSF wameendelea kuhangaika kutafuta mitambo katika nchi nyingine mbili ambazo ni Ufaransa na Sweden.


Mazingira haya ya kushindikana kutekelezwa kwa ahadi ya NSSF sasa yanaiweka Serikali na hasa Wizara ya Nishati na Madini katika kubanwa na Bunge.


"Sasa sisi (Kamati ya Nishati) tunashangaa na kujiuliza mambo mengi. Kwanza, ahadi inaonyesha mtambo wa kwanza wa NSSF wa umeme wa megawati 50 ulipangwa kukamilika Septemba, kumbe mitambo ilikuwa ya kwenda kutafuta. Je, nani aliyeshinikiza ahadi hii yenye utata kutolewa bungeni? Kumbuka ahadi ya mpango huu ilitolewa Agosti 13.


"Ukiwauliza Tanesco wanasema ni NSSF wenyewe ndiyo walitoa muda wa kukamilisha kazi zao lakini NSSF wanasema ni Tanesco.


"Lakini pia hili suala la kutoa ahadi kumbe ndiyo kwanza unakwenda kutafuta mitambo tena bila uhakika bado haliingii akilini. Wamekosa mitambo Marekani sasa wanakwenda kutafuta Ufaransa na Sweden. Hapa kuna gharama ya kuzunguka kutafuta mitambo lakini ni dhahiri ahadi yao haikuwa ya uhakika. Ahadi haikuwa na muamana," alisema Makamba.


NSSF kuondolewa orodha ya dharura

Inaelezwa sasa kwamba NSSF ambayo iliingizwa katika utekelezaji wa kuzalisha umeme wa dharura, itaondolewa kwenye udharura na kuingizwa kwenye mpango wa kati, ambao umepangwa kukamilika Julai, mwakani.

Taarifa za uchunguzi na za uhakika za gazeti hili zinaeleza kuwa nafasi ya NSSF sasa imechukuliwa na kampuni ya Jacobsen ambayo awali, ilifanya mazungumzo na Tanesco ili kuweka mitambo yake eneo la Kinyerezi na kwamba ujenzi wake ukamilike Juni, mwaka 2012 lakini sasa kazi zake zitakamilishwa Desemba, mwaka huu badala ya Juni. Mitambo ya Jacobsen inatumia mafuta ya mepesi (mafuta ya ndege) aina ya Jet A-1.


Hali ilivyokuwa bungeni

Serikali iliahidi kuibua mpango wa dharura baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Julai 18, mwaka huu, kuliomba Bunge kuahirisha kupitisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Kutokana na kauli hiyo ya Pinda, Wizara ya Nishati na Madini, kupitia kwa Waziri wake, William Ngeleja, iliwasilisha mpango wake wa dharura na wa muda wa kati. Mpango wa dharura ulitajwa kukamilika Desemba mwaka huu.


Kwa ujumla, mipango hiyo ilitarajiwa kuingiza katika Gridi ya Taifa umeme wa megawati 572. Ahadi hizo zinahusisha awamu mbili. Awamu ya kwanza ni kuzalisha megawati 300 (hadi Desemba, 2011) na ya pili ni kuzalisha megawati 310 hadi kufikia Desemba 2012.


Mbali na ahadi hizo, ahadi nyingine iliyotolewa ni upanuzi au ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi ya asili kutoka Songosongo na Mnazi Bay, hadi Dar es Salaam ili kuongeza kiwango cha gesi kinachotumika kuzalisha umeme katika mitambo ya Dar es Salaam.










 
Tukihesabu kwa utulivu kabisakabisa pesa iliyopotea (Net Loss) kupitia umeme tokea usanii wa IPTL hadi leo tunaweza tukahitajika hata kama hatupendi kuwanyonga watu tena kwa kutumia kamba ya kufungia meli
 
Tukihesabu kwa utulivu kabisakabisa pesa iliyopotea (Net Loss) kupitia umeme tokea usanii wa IPTL hadi leo tunaweza tukahitajika hata kama hatupendi kuwanyonga watu tena kwa kutumia kamba ya kufungia meli
 
Sasa huu utapeli au umbumbumbu, hao NSSF wako karne ya ngapi, mitambo anauza mtu na si kampuni? au mnatumia madalali, mnazunguka kwa pesa zetu kutalii marekani mnajifanya mlitaka kuingizwa mkenge.
Hayo mambo yenu tushawashtukia sasa hivi mnaenda tena Ufaransa na Sweden kula bata, mje na majibu mengine.
 
Hapo kuna ufisadi gani wakati NSSF wamekuwa makini kuepuka kutapeliwa?
 
Back
Top Bottom