Ufisadi mpya BoT kutinga bungeni

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Date::6/30/2008
Ufisadi mpya BoT kutinga bungeni

*Naibu Gavana asema ripoti bado ni siri

*Ni ule wa Sh 5 bilioni zilizolipwa kwa kampuni mbalimbali

*Homa ya EPA nayo juu

*Lipumba amtuhumu Mkulo kuandaa mkakati wa kuchota nyingine

Ramadhan Semtawa na Muhib Said
Mwananchi

Ufisadi huo ambao umebainika katika Ripoti ya Hesabu za BoT kwa mwaka 2006/07, ambayo iliwasilishwa katika Bodi ya Wakurugenzi ya BoT Juni 6 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, umekuja wakati jinamizi la wizi wa Sh 133 bilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kutoka BoT likiwa bado linaitafuna serikali na taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka kutoka kwa vyanzo huru vya habari, ripoti hiyo inapaswa kuwasilishwa bungeni huku BoT ikipaswa kueleza hatua ambazo imekwishachukua katika ufisadi huo, ikiwemo hatua dhidi ya maofisa wake waliohusika.

Alipoulizwa na gazeti hili, Naibu Gavana wa BoT (Utawala), Juma Reli, alisema hadi sasa ripoti hiyo ni siri na haijawa rasmi kutolewa kwa umma.

Hata hivyo, Reli alithibitisha kwamba ukifika wakati ripoti hiyo itawasilishwa bungeni, lakini akakata kuthibitisha tuhuma hizo wala kukataa zaidi ya kusisitiza kuwa: "Siwezi kuzungumzia taarifa ambazo ni za siri, subirini kama ni kweli mtaelezwa."

Reli alifafanua kuwa, hadi sasa Waziri mwenye dhamana yaani wa Fedha na Uchumi, hajaona ripoti hiyo. "Hata waziri hajaiona, unataka nizungumzie nini, inapaswa kupita kwa waziri kisha aweze kuisaini. Sasa unataka nizungumze kitu ambacho hakijawa rasmi?" alihoji.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba hakuna kitu kitakachofichwa kwani moja ya mambo muhimu ambayo BoT inazingatia kwa sasa ni kuendesha mambo yake kwa uwazi.

Mchanganuo wa ripoti hiyo ambayo ilitolewa katika kikao hicho, unaonyesha kwamba ufisadi huo ambao ni mbali ya EPA, haukufikishwa mbele ya Tume ya Rais (Task Force) ambayo imekuwa ikichunguza tuhuma za wizi wa awali wa Sh 133 bilioni kwa miezi sita sasa.

Utouh alieleza kuwa, ukaguzi ulikuwa ni wa kawaida kwa hesabu za mwaka na haukuwa na uhusiano na EPA.

Katika sehemu ya ripoti hiyo, mchanganuo unaonyesha Sh 4.74 bilioni zililipwa kwa kampuni moja ya jijini Arusha (jina tunalo), ambayo hujihusisha na biashara mbalimbali, Sh 1 bilioni zililipwa kwa kampuni maarufu ya uwakili jijini Dar es Salaam (jina tunalo) na Sh 500 milioni kwa kampuni ya Canada, kwa ajili ya kusambaza vifaa vya mfumo wa kupiga picha maalum. Ripoti hiyo yenye kurasa karibu 100, pia sehemu yake inaonyesha Sh 455 milioni zililipwa kwa kampuni ya jijini Dar es Salaam jina (tunalo).

Hali ikiwa ni hiyo katika hesabu za mwaka 2006/07, taarifa zaidi kutoka serikalini zinasema Timu ya Rais chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johson Mwanyika, iko katika wakati mgumu huku hofu ya kutoeleweka kwa umma ikitanda. Kwa mujibu wa taarifa hizo, timu hiyo inahofu kwamba ripoti yake ambayo inatarajiwa kukabidhiwa kwa Rais Julai 9, inaweza kuwa nyepesi tofauti na matarajio ya umma.

"Sasa hivi timu ya EPA yenyewe haijiamini, inahofu matokeo yake hayataeleweka kwa wananchi, ni kinyume na matarajio, subiri utaona," kilisisitiza chanzo hicho kutoka idara nyeti ya serikali. "Kwa hiyo ni homa tu, jamaa wenyewe wanahofu, kila siku wanapanga namna ambayo wataweza kuwasilisha ripoti hiyo na umma utakavyoipokea."

Homa hiyo imekuja wakati muda wa timu hiyo ambayo ilipewa jukumu hilo, Januari 9 ikitarajiwa kukamilisha kazi hiyo huku tayari serikali ikianza kufanya 'usanii' kwa kutoa taarifa tata kuhusu fedha za EPA, kwamba si zake wala za BoT.

BoT katika kipindi kuanzia mwaka 2005/06, imeweza kukumbwa na tuhuma nzito za ufisadi ambazo ni pamoja na EPA na ujenzi wa majengo pacha kwa gharama kubwa za takriba Sh 600 milioni.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kwamba fedha za EPA katika BoT, si za serikali wala umma, ni mbinu ya baadhi ya wana-CCM ya kutaka kuendelea kuchota fedha katika akaunti hiyo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.
 
Back
Top Bottom