Ufisadi hadi kwenye vyombo vya habari?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Ufisadi hadi kwenye vyombo vya habari?

Lula wa Ndali-Mwananzela Aprili 15, 2009

Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

NAOMBA leo nisizungumzie mambo ya siasa kwa kadiri tunavyoziona siku hizi (mafisadi vs wazalendo).

Sitaki kumzungumzia Rostam Aziz au Dk. Harrison Mwakyembe au kuwazungumzia wanasiasa wetu wa kila siku. Naomba leo nizungumzie kwa kifupi sana juu ya vyombo vyetu vya habari.

Wanasiasa kadhaa wamekuwa wakirusha lawama kwa vyombo vya habari nchini, baadhi yao wakidai kuwa waandishi wa habari hawajasoma sana ndiyo maana wanaandika mambo fulani fulani kwa kiwango cha chini, na wapo wengine wanaolaumu vyombo hivyo kwa kujipanga na makundi fulani ya kisiasa nchini.

Wapo pia ambao wanaangalia vyombo vya habari kwa dharau, kwani licha ya wingi wake ubora wake wa kazi unalingana kabisa na ubora wa kazi za watu wengine ambao wanaandikwa kwenye magazeti au kutajwa kwenye vyombo hivyo, yaani ni duni.

Ninaamini kuwa kuna changamoto kubwa kadhaa kwa vyombo vyetu vya habari ambazo kwa namna moja au nyingine, zimechangia sana katika kutufikisha hapa na ninaamini kama zikifanyiwa kazi zitainua vyombo vyetu vya habari kuelekea ubora wa hali ya juu.

Changamoto ya kwanza ni ujuzi wa mambo

Sijui ni kwa kiasi gani waandishi wetu hujisomea juu ya mambo mbalimbali ambayo wanapenda kuyaandikia. Ninaposema kujisomea nina maana kufuatilia jambo fulani kisomi, kulielewa undani wake na kuelewa kwa kina ili utakapokutana na mtu unataka kumuuliza swali basi angalau mnakuwa kwenye kundi moja.

Vinginevyo, waandishi wetu wamebakia kuwa kama vile vinasa sauti ambavyo vinarudia tu maneno wanayosikia bila kuyaweka katika maudhui yake.

Mfano mzuri ni suala la Benki Kuu au masuala ya fedha ya TRA. Kiongozi wa Benki Kuu au TRA anapokuja na hesabu mbalimbali na kusema “mwezi uliopita mfumuko wa bei ulikuwa hivi” au akisema “TRA itakusanya mapato kidogo mwezi huu” wana maana gani? Sasa mwandishi akiripoti na kusema “Benki Kuu imesema x,y” au “TRA imesema m,n” wanachofanya ni kurudia tu kile kilichosemwa lakini kwa mtu wa kawaida anaweza asielewe kabisa wanamaanisha kitu gani kinachohusiana na maisha yao ya kawaida.

Hivyo, changamoto ya kwanza ni kuwa waandishi wa habari wanaoandika habari fulani maalumu ni vizuri wakajiendeleza au kujielimisha katika uelewa jambo hilo. Ni kwa sababu hiyo utaona baadhi ya vyombo vya habari vilivyoendelea vinachukua mwandishi ambaye ni mwanasheria kuandika mambo ya sheria, mwandishi aliyesomea uchumi kuandika mambo ya uchumi na mwandishi ambaye ni daktari kuandika na kutolea taarifa mambo ya kitabibu.

Naamini, vyombo vikubwa vya habari vinaweza kukusanya nguvu na kuanzisha kozi angalau za wiki moja moja kwa waandishi wao ili kuweza kuwapatia ufahamu wa mambo mbalimbali.

Kwa mfano, kozi ya waandishi wa habari za sheria ambao wataenda kupigwa msasa kuelewa dhana mbalimbali za kisheria, mfumo wa utawala n.k na ni wao wanaporudi kwenye magazeti au vyombo vyao vya habari hupewa nafasi za kuandika habari au kutolea maoni ya kisheria.

Kozi hizo zinaweza hata kufikia nafasi za shahada kabisa. Kwa kufanya hivyo tunawasaidia waandishi wetu, tunavisaidia vyombo vyetu na kwa hakika tunawasaidia wananchi kuweza kusoma habari zenye kina, zilizo na hoja na ambazo zimewekwa katika maudhui ya maisha ya mwananchi.

Changamoto ya pili ni uthubutu wa kuhoji

Mojawapo ya vitu ambavyo bado tunavihitaji katika fani ya uandishi wa habari nchini ni uthubutu wa kuhoji habari, hoja, na kauli za viongozi wetu mpaka majibu ya kuridhisha yanapopatikana au hadi wanapoamua kurusha ngumi!

Kwa kiasi kikubwa miaka hii mitatu iliyopita tumeweza kutoa maoni yetu kwa uhuru zaidi, tukiandika na kujenga hoja mbalimbali. Kwa kiasi kikubwa maoni hayo yameonyesha uthubutu mkubwa na yamekuwa yakivumilika sana na watawala.

Hata hivyo, hatua inayofuata si tu kuandika na kutoa maoni bali kuwahoji na kuwabana wahusika wakubwa wa habari zetu.

Hapa ninamaanisha kuwa mwandishi anapokwenda kuuliza au kufuatilia habari fulani, asikubali kamwe maelezo nusunusu ya kiwoga au yenye mwelekeo wa kibabe. Mwandishi asikubali kudharauliwa na mtu yeyote yule hata kama mtu huyo ni mfalme wa mbinguni.

Ni lazima waandishi wajifunze kuuliza maswali ya kubana ambayo msingi wake unaanzia na “lakini”. “Lakini, mzee Malecela (mfano) hayo malumbano ni yapi na kina nani wanaolumbana?” anaulizwa.

Zaidi ya yote maswali hayo ya kubana yanaendana na mtu kujua anachozungumzia. Kama mwandishi usiende kwenye mkutano wa waandishi wa habari kama hujajiandaa kuuliza maswali ya kupekua!

Zaidi ya yote mwandishi makini asikubali majibu ya jumla ambayo yanaacha maswali yakielea. Wakati wowote unapopewa jibu ambalo liko la jumla tu kama la “ndiyo au hapana” ni lazima utafute namna ya kuuliza swali la nyongeza lenye kuhitaji maelezo zaidi, na ushahidi zaidi. Tusije kugeuka kuwa vipaza sauti vya watawala nakurudia kama kasuku kile kinachosemwa hata kama hakina ukweli.

Chukulia kwa mfano suala hili la DECI. Hivi serikali ilikuwa wapi muda wote huu? Sasa tunapompata mtu wa Benki au Polisi kuelezea kuhusu DECI badala ya kusikiliza anachosema kuhusu taasisi hiyo ni jukumu la mwandishi kuwauliza maswali ya ndani wao wenyewe na uhusika wao katika DECI na kutaka majibu ya kuridhisha.

Inakuwaje Polisi kutoa ulinzi kwa kampuni inayovunja sheria wakati wanajua inavunja sheria? Kama watu hawa watapoteza fedha zao kama Serikali inavyohofia kwanini uongozi wa Jeshi la Polisi usiwajibike kwa kutoa ulinzi kwa wezi?

Hivyo, ni muhimu kujifunza kuuliza maswali kwa kufyatuka na kuyarusha pasipo kuangalia sura ya muulizwa, cheo chake au jicho analoweza kukurushia.

Changamoto ya tatu ni kuwa waandishi ni lazima wawe huru

Mojawapo ya changamoto ninazoziona ni kuwa bila waandishi kuwa huru ni vigumu sana kwa wao kuandika habari kwa uhuru wote. Uhuru ninaozungumzia mimi hasa ni kuwa waandishi wasikubali kutumiwa kama wasaidizi wa Serikali.

Katika sekta binafsi sijali sana lakini linapokuja suala la fedha za umma na Serikali itakuwa ni makosa makubwa kwa waandishi kuwa kama sehemu ya Serikali.

Kati ya vitu vinavyonitatiza sana ni pale ambapo Serikali au kiongozi fulani wa Serikali anapoamua kusafiri na waandishi wa vyombo huru vya habari halafu akawalipia usafiri, malazi na posho.

Hili lilitokea mwaka jana katika safari za kiongozi mmoja wa kitaifa wakati waandishi kadhaa ambao wamekuwa wakiiandika kwa uzuri Serikali walipopewa nafasi ya kupeperuka naye kwenda majuu kitu ambacho kilichukuliwa kama shukrani ya aina fulani.

Kama vyombo vya habari haviwezi kuwagharimia waandishi wake ni bora wasishiriki kuliko kujiweka kwenye mazingira ya kuonekana kuwa wana ukuwadi wa aina fulani.

Inapotokea, kwa mfano, ni lazima mwandishi asafiri na kiongozi fulani basi chombo cha habari husika ndicho kinatakiwa kubeba gharama ya mwandishi huyo ili kuhakikisha uhuru wake.

Uhuru huu wa waandishi wa habari utatuhakikishia waandishi hata wakiwa kwenye msafara mmoja na kiongozi fulani bado wanakuwa huru kuandika wanachokiona pasipo woga wa kukosa nafasi nyingine huko mbele.

Katika hili wakati umefika kwa sera au makubaliano ya kimaadili ya kazi kuandikwa kati ya Serikali na waandishi wa habari. Serikali iweke utaratibu ulio wazi wa jinsi ambavyo waandishi wa habari wanatakiwa kusafiri na viongozi, au kushiriki na mikutano ya viongozi.

Kwa mfano, kiongozi wa umma asiruhusiwe kabisa kuchagua mwandishi gani au wa chombo gani aende kwenye mkutano wake! Wakati huo huo vyombo vya habari vihakikishe waandishi wake wanatia sahihi makubaliano ya kuheshimu miiko ya kazi ambayo inaeleweka.

Pasipokuwa na vyombo huru vya habari na waandishi huru matokeo yake ni huu mwelekeo wa kisiasa ambao tunauona siku hizi katika vyombo vyetu vya habari hadi kufikia mahali tunajua kabisa gazeti fulani au steheni ya radio fulani imefungamana na mwanasiasa fulani na hivyo habari tukizisoma zinakuwa na mwelekeo huo.

Ni kwa sababu hiyo naamini uandishi wa magazeti kadhaa (kwa sababu za wazi sitayataja) licha ya kuwa na habari nyingi muhimu, yamefikia mahali kuwa yana mwelekeo wa kufuata fuata watu fulani fulani kiasi kwamba ukilishika gazeti mojawapo utajua kabisa wiki hii linamlenga nani!

Mwisho utagundua kuwa katika magazeti hayo kuna watu kama wanane tu ambao ndio wanazungushwa kila toleo! Huu siyo uhuru wa habari!

Inapofikia gazeti fulani haliwezi kuandika habari nzuri za mtu fulani basi ujue kuwa gazeti hilo limepoteza uhuru wake! Katika hili kwa kweli lawama kubwa inawaendea wamiliki wa vyombo hivyo vya habari kwani kwa kiasi kikubwa wao ndiyo wenye kupiga filimbi nani acheze. Wamiliki hawa hawawezi kuona magazeti yao yakiandika jambo jema la mtu fulani kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanampa ujiko. Matokeo yake waandishi wa magazeti hayo kwa kweli wanabakia kuwa vikaragosi vya wamiliki wake!

Lakini lawama kubwa zaidi ambazo zimechangia kupoteza uhuru huu ni usimamizi mbovu wa Serikali ambapo wamevumilia uchafu mwingi kwenye magazeti yetu na hadi sasa hawajui nani achukuliwe hatua bila kuonekana ameonewa na mwingine ameogopwa. Ni Serikali kama ilivyolea uchafu mwingine wa ufisadi, sasa imekaa pembeni ikiruhusu ufisadi katika uandishi wa habari kushamiri.

Kama tunataka kuwa kweli vyombo huru vya mabadiliko kuelekea 2010 na katika ujenzi wa taifa ni lazima vyombo vyetu vya habari viwe huru, viwe vyenye kuthubutu na waandishi wake wawe na ujuzi wa mambo mengi wanayoyafanyia kazi au kuyaandikia.

Ni lazima turudi na kuhakikisha kuwa uhuru wa habari si sawasawa na wingi wa vyombo vya habari. Tunaweza kuwa na vyombo vingi vya habari ambavyo si huru wakati miaka michache iliyopita tulikuwa na vyombo vichache vya habari lakini huru sana.

Vinginevyo, ufisadi ambao tunaamini umeingia kwenye utendaji wa Serikali na vyama vya siasa, nina hofu umekwisha kuingia kwenye vyombo vyetu vya habari na sasa vimegeuka kuwa nakala tu za mafisadi hao. NI lazima tujiokoe kabla hatujazama.
 
Back
Top Bottom