Udhibiti wa ubora wa bidhaa utathminiwe upya

Edwin Mtei

Senior Member
Dec 13, 2008
181
342
Tanzania Bureau of Standards (Taasisi ya Ubora wa Bidhaa Tanzania) ina jukumu la kukagua na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazozalishwa viwandani hapa nchini na hutoa vyeti (Certificates) kwa wazalishaji na kupiga mihuri zile bidhaa inazoridhika na ubora wake kabla ya kusambazwa kwa walaji au watumiaji. Naamini pia ni jukumu la TBS kuona kwamba bidhaa zinazoingizwa kutoka nje zinadhibitiwa.

Majukumu haya muhimu ya TBS yanapaswa kutekelezwa kabla bidhaa hazijaanza kusambazwa au kuuzwa reja reja kwa wananchi. Hata hivyo kumezuka mtindo wa wafanya biashara wengi kuuza bidhaa feki au bidhaa zenye ubora wa hali ya chini sana.

Huenda hali hii inatokana na maafisa wa TBS kutokuwa makini pale bidhaa zinazalishwa humu nchini. Kwa bidhaa zinazoingia toka nje, Idara ya Forodha na TBS wanatakiwa kuhakikisha ubora wa bidhaa hizo. Inakuwa ni fedhedha kwa Idara ya Serikali kutoza ushuru na kodi na TBS kuruhusu bidhaa ziingie, halafu zikifika dukani, Polisi wanazikamata na kuziteketeza eti kwa vile ni bidhaa feki.

Hali hii huenda ikatokana na tamaa ya wafanya biashara wenyewe kutaka kutajirika haraka haraka kwa kuuza bidhaa rahisi, au kutokuwa makini katika kuamua ni bidhaa zipi bora. Wenye tamaa hata kuagiza bidhaa mbovu au hafifu kwa bei ya chini maksudi ili waweze kuziuza kwa urahisi kwa vile wanajua wanunuzi wengi nchini kwetu wana uwezo mdogo kutokana na umaskini. Idara ya Forodha na TBS wahusishwe kikamilifu. Waagizaji wa bidhaa hafifu wasije wakatoa rushwa kwa maafisa wa TBS kupitishabidhaa zisizokidhi mahitaji na nyingine kuweza kuathiri afya na maisha ya wananchi.

Kumezuka mtindo wa viongozi wa Serikali katika ngazi za chini kuvamia maduka vijijini au hata mijini na kukamata bidhaa feki au bidhaa zenye ubora wa hali ya chini na kuamuru ziteketezwe. Wananchi kadhaa hushangilia wanapoona wafanya biashara wakitiwa mbaroni au bidhaa zao zikiteketezwa, wakiwalaumu kwamba ni wanyonyaji na mabepari.

Maoni yangu ni kwamba mtindo huu unaweza kutupeleka pabaya. Wafanya biashara vijijini ni watu muhimu wanaotoa huduma ambayo wanavijiji wanahitaji kwa karibu. Duka la kijijini ni mahala wanajamii wanapopata kwa karibu bidhaa au vifaa ambavyo wangelazimika kwenda mbali kuvipata. Hata katika miji, bidhaa au vifaa muhimu hupatikana toka maduka haya yanayotoa huduma za reja reja.

Kama bidhaa ni feki au zina ubora wa hali ya chini, ni kutokana na udhibiti usiokidhi mahitaji katika viwanda au bandarini wakati wa kuingiza bidhaa hizo. Kwa hiyo TBS na wakala wake wana wajibu wa kufanya kazi zaidi. Sina hakika Sheria inayohusu TBS inatumiwaje kudhibiti bidhaa hafifu au feki ambazo tayari zimekwishaingia katika maduka ya reja reja.

Hata hivyo, ili kuondoa uwezekano wa wafanya biashara kuonewa, nashauri TBS itoe maelekezo na utaratibu wa kufuata katika kushughulikia tatizo hili. Itambulike kwamba wenye maduka mijini na vijijini ni watu wanaotoa huduma muhimu, wengi wao wakiwa ni waadilifu. Ijulikane pia kunaweza kuwa na maafisa wenye choyo au wenye kutaka kulipa kisasi ambao wanaweza kuvamia maduka na kuteketeza mali kwa kisingizio kwamba ni feki.

Ijulikane pia kwamba bidhaa au vifaa vyote hata kama vina ubora wa chini vinanunuliwa wa wenye maduka, na kama vimetoka nje ya nchi, ni fedha zetu za kigeni zimetumika. Kabla ya kuviteketeza ni lazima turidhike kwamba ni kwa manufaa ya umma au la.

Ningependekeza kwamba bidhaa ambazo zinatumika kama chakula au dawa za binadamu au mifugo ambazo ni feki ziteketezwe bila kusita pale inapodhihirika hazifai. Hata bidhaa ambazo ni dawa za mimea au mbolea ambazo ni feki ziteketezwe. Lakini bidhaa ambazo ni vyombo vya matumizi yasioathiri afya mara moja, kama redio, TV sets, samani, mavazi n.k., waagizaji walazimishwe kuvirejesha kwa waliowauzia na kuwarudishia fedha zao.

Hapo awali, wakati nikiwa Gavana wa Benki Kuu, waagizaji wa bidhaa toka ng’ambo walikuwa wanatakiwa wafungue Letters of Credit katika benki yao ya biashara, na hiyo benki ilikuwa inaruhusiwa kupeleka fedha kwa muuzaji wa hizo bidhaa tu, pale zilipofika katika bandari yetu na kuruhusiwa na Idara ya Forodha kuingia nchini. Kama utaratibu huu ukizingatiwa, na kuhusisha TBS katika kukagua na kuthibitisha ubora wa bidhaa zinazoingia, basi tungelipia mali inayokidhi ubora tunaotaka tu. La sivyo bidhaa mbovu zingerudishwa zilikotoka, kwa vile hazitalipiwa.

Kuhusu ubora wa bidhaa tunazozalisha hapa nchini, bila shaka kama TBS na wenye kuzinunua toka viwandani au mahala popote zinapotengenezwa watakuwa makini, tutaepuka tatizo hili. Hasara kwa wafanya biashara pia itaepukwa.
 
Hii ni kweli sana; nimeona juzi walipokamata bidhaa huko Tabora na wale wafanyabiashara walijikuta wanailalamikia serikali kuwa wao wanafunga safari kwenda Dar kununua bidhaa kwenye maduka makubwa na yenye hadhi; hawana utaalamu wa kujua ipi ni bidhaa halisi au feki. Wanauziwa na wafanyabiashara wakubwa wanaoagiza vitu hivyo nje.

Lakini cha kushangaza ni kuwa ni hawa wafanyabiashara wa mwisho ndio wananyang'anywa bidhaa zao. Hadi hivi sasa sijui kama kuna waagizaji wa bidhaa hizo wametiwa mbaroni au kufikishwa mahakamani kwa kuagiza na kuingiza bidhaa feki nchini. Lakini vile vile watu wa customs ambako bidhaa hizo hupita hawajui jinsi ya kugundua tofauti ya bidhaa hizo?
 
Mzee Mtei,
Times change. Hii ndio nchi tuliyoamua kuijenga. Kila kitu ni feki feki tu.
 
Mzee Mtei,

we acha tu, anyway hebu kwanza tufikirie nani mgombea wetu
 
Ktk nchi yetu tatizo kubwa ni siasa aka maneno matupu. Hawa tbs sidhani kama wanafanya kazi kwa manufaa ya watu wa hali ya chini. Nadhani na nilishapendekeza kuwa takukuru, tbs, wizara ya fedha viwe chini ya usalama wa taifa wakisaidiana na JWTZ manake hawa kidogo wanaonekana kuwa na moyo wa uzalendo ndo mambo yatakwenda vizuri vinginevyo maumivu ni palepale tu!
 
Solution ni mabadiliko.....USA kulikuwa na issue ya toys za watoto zinazotengenezwa China kuwa na sumu ya led,wauzaji hawakulaumiwa bali manufacturers this time makampuni ya China pamoja na kitengo cha marekani kinachoshughulikia ubora wa bidhaa,nchi yetu ni bora liende na maslahi ya wananchi is nothing....na rais anadai anaweza kuamua chochote bila kujali haki za binadamu,sasa mnategemea nani aamue nini na kwa maslahi ya nani?Wanaoagiza bidhaa hizo kwa jumla ndo wenye kuchangia ccm.
Msitegemee haki chini ya utawala usiojali haki.
 
Kumezuka mtindo wa viongozi wa Serikali katika ngazi za chini kuvamia maduka vijijini au hata mijini na kukamata bidhaa feki au bidhaa zenye ubora wa hali ya chini na kuamuru ziteketezwe. Wananchi kadhaa hushangilia wanapoona wafanya biashara wakitiwa mbaroni au bidhaa zao zikiteketezwa, wakiwalaumu kwamba ni wanyonyaji na mabepari.

Ningependekeza kwamba bidhaa ambazo zinatumika kama chakula au dawa za binadamu au mifugo ambazo ni feki ziteketezwe bila kusita pale inapodhihirika hazifai. Hata bidhaa ambazo ni dawa za mimea au mbolea ambazo ni feki ziteketezwe. Lakini bidhaa ambazo ni vyombo vya matumizi yasioathiri afya mara moja, kama redio, TV sets, samani, mavazi n.k., waagizaji walazimishwe kuvirejesha kwa waliowauzia na kuwarudishia fedha zao

Mzee Mtei unachosema ni kizuri sana.

Lakini inauma sana unapoteketeza bidhaa za mfanyabashara zenye thamani ya shilingi milioni 50. Hapo unakuwa umemuua kabisa kibiashara, kwanza kabisa ni lazima tujiulize ni kwanini bidhaa feki zinaingia kwenye soko letu? zinapitia wapi? kwa nini tusianze kushughulika na zinapopita? Hatuwezi kushughulika na zinakotoka, na kusema tuziteketeze hapa nyumbani ndio lengo la wanaoataka zitupwe, yaani tunakuwa tumewasaidia kutimiza lengo la kutafuta dumping place tena kwa kumtia hasara mfanyabiashara mtanzania. Kwa hiyo best way ni kuhakikisha kuwa haziingii au hazipiti bandarini, lakini kutokana na ufisadi pale bandari ndio maana tunalalamika kuwa tuna tatizo la bidhaa feki. Tunajua kabisa zinapopita why don't we deal with them from there.

TBS hatuwezi kuiamini sana, bado haina uwezo wa kukagua ubora wa bidhaa kama huamini chukua bidhaa yoyote yenye nembo ya TBS ipeleke UK au South Africa usikie matokeo yake, ina uwezo kidogo sana na hakuna anayejali kuiwezesha iwe na uwezo mkubwa. NI much better ikifa, tutumie maabara za Afrika kusini au Uingereza kwa gharama za chini na kwa ufanisi zaidi kuliko kuwa na TBS ambayo ni impotent. Lakini muhimu zaidi ni ku-deal na bandari.
 
Kwa hili la bidhaa feki na zenye ubora hafifu, everyone must play their part.

Waziri wa Viwanda na Biashara: aelimishe umma juu ya athari za kutumia bidhaa feki na zenye ubora hafifu. Pia waweke mikakati madhubuti ya kupambana na waagizaji wa hizi bidhaa za ubora mdogo.

Maofisa wa vyombo husika (TBS, TFDA, Bandari, TRA): Kuweni makini. Mpeleke mapendekezo wizarani ya jinsi mnavyoweza kuwezeshwa kukabiliana na hili tatizo.

Wananchi wa kawaida: Hawa ndo muhimu zaidi kuliko wote hapo juu. Tujielimishe na kutambua kwamba rahisi ya bidhaa hafifu leo ni ghali kesho kiafya na kimaendeleo kwa ujumla. Tutambue kwamba kwa mtazamo mrefu, bidhaa bora ni nafuu zaidi kwa gharama. Tuangalie mbali. Wananchi wa kawaida wakizikataa bidhaa hafifu, hakuna atakayeziagiza. Tuondokane na hulka ya kupenda vya dezo na rahisi bila tafakuri ya kina.
 
tunaendelea kutumia bidhaa feki sijui kwa nini tunajiua wenyewe ..tunashindwa kulitumi box la kura vema
 
Back
Top Bottom