Uamsho kuwafichua waliochoma makanisa Zanzibar

GHIBUU

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
4,432
3,006
Na Mwinyi Sadallah
2nd June 2012

Kiongozi wa Jamhuri ya Maimamu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI), Sheikh Amir Ahmed akizungumza na waandishi wa habari, kwa mara ya kwanza tangu kutokea vurugu Zanzibar, katika msikiti wa Mchangani mjini Zanzibar janaWakati mali za mamilioni ya fedha zikiwa zimeharibiwa kufuatia vurugu zilizotokea Zanzibar, Kiongozi wa Kamati ya Muungano wa jumuiya za Kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed amesema wamefanikiwa kupata orodha ya watu waliofanya hujuma ya kuchoma makanisa moto na kuahidi kuifikisha katika vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Vurugu hizo zilizodumu kwa siku tatu, zilianza Mei 26, zimesababisha hasara kubwa ikiwemo uharibifu wa nyumba za Ibada, uporaji wa mali za watu, na wafanyabiashara katika soko kuu Darajani na Mwanakwerekwe kushindwa kufanya kazi kwa siku tatu mfululizo.

Miongoni mwa athari nyingine ni kuchomwa moto kwa magari likiwemo la Askofu wa Tanzania Assemblies of God (TAG), lenye namba za usajili Z 694 AX, uharibifu wa miundombinu ya barabara, uchomaji wa matairi ya magari na upangaji wa mawe katikati ya barabara.

Padri wa kanisa la Mtakatifu Mikaeli, Ambrose Mkenda, ambalo limechomwa moto alisema kwamba tukio hilo, limesababisha hasara kubwa kutokana na mabenchi yote yanayotumiwa na waumini katika ibada kuchomwa moto pamoja na mali mbalimbali zilizokuwemo ndani ya kanisa vikiwemo vinanda viwili navyo vilitekea kwa moto huo.

“Hasara kubwa karibu milioni 20 kwa vile mali zote zilizokuwemo kanisani zimeungua moto na walinzi wetu walikimbia baada ya kuvamiwa na watu waliokuwa na silaha kali,” alisema Padri huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fresh Enterprises Catherine Peter alisema kwamba wamepata hasara inayofikia kiasi cha sh milioni 200, kufuatia watu waliovamia baa ya daraja bovu, na kung’oa madirisha, mabati, milango, vyoo vya masinki na kupora vinywaji vya aina mbalimbali zikiwemo bia na pombe kali mbali na fedha taslimu za mauzo.

Alisema kwamba uharibifu huo wa mali ulifanywa na watu waliokuwa na silaha za kijadi, na kutaka Serikali kuangalia uwezekano wa kufidia hasara walizozipata.

“Wakati Serikali inahamasisha wananchi wake wajiajiri kama wajasiriamali, leo wanatokea watu, wanaharibu mali ya mtu wakati tunafanya biashara halali tukiwa na leseni na kufuata taratibu zote za ulipaji wa kodi, hati ya Muungano iko kwa Rais Jakaya Kikwete, Rais Dk.Ali Mohamed Shein na Umoja wa Mataifa, lakini haipo katika baa”, alisema Catherine.

Makundi mengine yaliathirika na vurugu hizo ni wafanyabiashara katika soko la Mikunguni, Darajani, Mwanakwerekwe, wamachinga ambao wamesema walishindwa kufanya kazi na kuitaka Serikali itoe elimu ya kutosha juu ya athari zinazotokana na vitendo vya vurugu.

Kwa upande wa Nishati ya Mafuta, taarifa kutoka kwa baadhi ya makampuni ikiwemo United Petroleum, wamesema vurugu hizo zilisababisha mauzo yao kushuka kwa asilimia 25, katika kipindi cha siku tatu za vurugu.

Taarifa kutoka kitengo cha hesabu ndani ya kampuni hiyo iliyotolewa na Hady Bensulmah, alisema wateja wao wakubwa ni makampuni ya utembezaji wa watalii, mahoteli ya kitalii ambao hawakuweza kununua mafuta katika kipindi chote cha vurugu hizo mbali na wananchi wa kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari, Amiri mkuu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar na Msemaji wa Muungano wa Jumuiya za Dini ya kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed alisema kwamba wamefanikiwa kupata orodha ya watu waliohujumu makanisa Zanzibar na wataifikisha katika vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema kwamba Jumuiya ya Uamsho haihusiki na hujuma zilizotokea na uporaji wa mali, kwa vile mafundisho ya dini ya Kiislamu yanakataza vitendo vya vurugu na wamesikitishwa sana na kulaani vitendo vyote vya uchomaji moto wa makanisa.

Alisema kwamba wataendelea kudai haki yao, ya kuitaka Serikali ianzishe mchakato wa kura ya maoni, ili Wazanzibari waulizwe kama wanautaka Muungano au hawautaki, hadi hapo lengo lao litakapofanikiwa.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom