Tuungane Kuwasilisha Shinikizo letu Bungeni kwa kusaini petition ya Kilio cha Madaktari

HKBW

JF-Expert Member
Aug 4, 2009
468
342
Nchi yetu imekumbwa na matatizo mengi hivi karibuni na tegemeo letu kwa kiasi kikubwa limekuwa juu ya wawakilishi wetu tuliowachagua kutuongoza na kututekelezea yale yanayoweza kuijenga Tanzania yetu kwa manufaa ya watanzania wote.

Watanzania kwa kiasi kikubwa ni watu wa amani na uzalendo mkubwa kwa nchi yetu na jamii yetu na tumekuwa tukiwapenda, kuwaheshimu na kuwasikiliza viongozi wetu.
Wakati huu tunawarudia na kuwaomba waheshimiwa viongozi wetu kutenga mda huu kuwa maalum kusikiliza kilio chetu watanzania tulio wengi, tuishio katika dimbwi la umasikini na tunaokabiliwa na changamoto za kiafya bila kuwa na kimbilio la huduma rahisi za matibabu ya afya tulizozizoea kulingana na kipato chetu kidogo.

Tunatamani tungekuwa na uwezo wa kuwalazimisha madaktari kutushughulikia, lakini ni dhahiri kwamba wakiwa na vinyongo hawatatoa huduma iliyo bora na kusababisha ongezeko la rushwa kwenye hospitali zetu, kuongeza vifo vya watanzania wengi tusio jiweza kifedha na pia kutugawanya kwenye makundi ya huduma za afya.

Tunashukuru kwa demokrasia tuliyonayo ya kuwa na uhuru wa kuongea na kuwasilisha maoni yetu kwa uwazi, lakini tumesema sana na kujadili sana kila mahali na kwa hivi sasa mitandao ya kijamii nayo imesaidia kupaza sauti zetu na kuweza kuwasilisha njia mbali mbali za kutatua tatizo hili linalotukabili.Lakini muda umezidi kwenda, hali imezidi kuwa mbaya na bado hatujapata tumaini toka kwenu viongozi wetu wapendwa.

Maoni tuliyawasilisha kwa kuwa na tumaini la usikivu wenu, busara yenu na huruma yenu kwetu, lakini kutokana na mda mrefu mnaouchukua kutatua suala hili ukilinganisha na athari tunazozipata na matokeo ya kuwalazimisha madaktari kuwafanya kazi katika mazingira mabovu, hatunabudi kuandika petition (ombi la kutatutua tatizo la madaktari) na kusainiwa na sisi wananchi tunaotegemea huduma ya hospitali za serikali kwa asilimia 100, waathirika na yeyote mwenye kuona umuhimu.
Ombi hili tunalifanya kwa nia njema ya kuikumbusha serikali kuwa sisi wananchi kwa ujumla tunaona suala hili la madaktari ni nyeti na linahitaji utatuzi wa haraka usioweza kusubiri kesho.

Chama cha Madaktari tunakiomba kiandae ombi hili na kulisambaza kwa wananchi waliopo ndani na nje ya nchi kwa njia zote ziwezekanavyo na kuliwasilisha bungeni ndani ya wakati muafaka huku tukipendekeza iwe ndani ya kikao kijacho cha Bunge.
Kwa njia hii tutakuwa tumetumia haki yetu ya kidemokrasia, njia ya amani na utulivu kuwasilisha kilio chetu mbele ya wawakilishi wetu tukiwa na imani kuwa serikali yetu sikivu itatutatulia tatizo letu kwa wakati na kwa ubora zaidi.

Ni tumaini langu madaktari wanaweza kutusaidia fanikisha mchakato huu na kuweza kukusanya signature nyingi iwezekanavyo toka kwa wananchi na kushinikiza serikali kutatua mgomo huu kwa njia ya amani na utulivu.
Napenda kuwasilisha mawazo haya binafsi kwa Watanzania wanzangu
 
Back
Top Bottom