Tuudumishe Muungano, lakini wananchi waachwe waukosoe

GHIBUU

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
4,432
3,006
LEO Watanzania tunaadhimisha miaka 47 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Mwaka 1964 waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume, walikaa pamoja na kukubaliana kuunganisha nchi zao za Tanganyika na Zanzibar ili kwa pamoja ziweze kukabili vishindo na mikikimikiki iliyokuwa inaziyumbisha nchi changa barani Afrika, kutokana na njama za mabeberu za kuzikwaza nchi hizo changa kisiasa na kiuchumi.

Ni vigumu kuelewa jinsi mstakabali wa Tanganyika na Zanzibar ungekuwa iwapo nchi hizo zisingeungana na kuwa nchi moja. Kama tulivyosema hapo juu, ubeberu ulikuwa umepamba moto na dunia ilikuwa imegawanywa katika makundi mawili kiitikadi, moja likiwa la Ukomunisti chini ya himaya ya Urusi na lingine la Ubepari chini ya himaya ya Marekani. Mgawano huo ulitokana na kumalizika kwa Vita ya Pili ya Dunia mwaka 1945 vilivyoanzishwa na aliyekuwa kiongozi wa Ujerumani, Adolf Hitler mwaka 1938.

Baada ya vita hiyo, himaya hizo mbili zilizua uadui mkubwa baina yao, huku kila moja ikitaka kuiangamiza nyingine ili itikadi yake itambe na kuiwezesha kuitawala dunia. Himaya moja iliinyatia Zanzibar na nyingine ilifanya hivyo kwa Tanganyika na kuzua hofu kubwa kwa nchi hizo mbili.

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa nchi hizo mbili walifanya makubaliano ya kuunganisha nchi zao ili kuushinda ubeberu uliokuwa unahaha huku na kule kupanua himaya zao katika nchi changa, hasa barani Afrika.

Ndipo viongozi hao kwa nia njema walisaini rasmi mkataba wa kuunganisha nchi hizo Aprili 26 mwaka huo, hivyo kuzaliwa kwa nchi inayojulikana kama Tanzania. Siku hiyo ambayo mwaka huu inasheherekewa leo nchini kote, huadhimishwa kila mwaka kwa vifijo, nderemo na bashasha.

Hapana shaka kuwa ingawa Muungano wetu unayumba, chombo hicho kimetoka mbali na sote tumesafiri nacho kwa umbali mrefu na kupita katika milima na mabonde. Hata hivyo, tungetegemea watawala wetu katika sehemu zote mbili za Muungano kuwataka wananchi wote kusaidia kutafuta suluhisho la kuyumba kwa chombo hicho.

Badala yake watawala hao wamefanya kila hila ili jambo hilo lisifanyike na kama tulivyoshuhudia wakati wa kujadili muswada wa marejeo ya Katiba ambao ulikataliwa na wananchi hivi karibuni, muswada huo ulikuwa na vipengele vya kuwatisha na kuwaziba midomo wananchi ili wasiujadili Muungano kwa kutamka kuwa ni kosa la jinai kufanya hivyo.

Hulka ya binadamu ni kupinga mambo yote hata kama ni mazuri ambayo hufanywa na watawala pasipo kuwashirikisha. Pamoja na umuhimu wa Muungano wetu, moja ya sababu za kupingwa kwake ni kuwa wananchi hawakushirikishwa.

Mwangwi tuliousikia na vurugu tulizoziona wakati wananchi wakijadili sheria ya marejeo ya Katiba havikutokana hasa na wananchi kuukataa Muungano, bali hasira zao kutokana na watawala kutowashirikisha katika kuunda na kuendesha Muungano huo.

Huko Zanzibar hasira za wananchi na viongozi wao kutosikilizwa kuhusu mambo ya Muungano zimejitokeza waziwazi. Kikundi cha G15 ambacho ni kati ya vikundi kadhaa vilivyojitokeza kuhoji uhalali wa Muungano kwa madai kuwa Zanzibar haikupewa hati ya mkataba uliohalalisha Muungano huo.

Na kama tulivyosema hapo juu, viongozi mashuhuri visiwani humo pia wamepaza sauti kuunga mkono madai hayo kwa kuitaka Serikali kuwaruhusu wananchi kujadili na kuhoji masuala ya Muungano ili waamue mustakabali wa nchi yao.

Mmoja wa viongozi hao ni aliyekuwa waziri katika Serikali ya Muungano, Hassan Nassoro Moyo, ambaye pia ni mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ambaye alisema mwishoni mwa wiki kuwa anaunga mkono vijana wanaohoji Muungano na kusema kuwa wananchi wana haki ya kuhoji uhalali wa Muungano na kwamba kiz Nyerere and Karume.jpg azi cha leo kiachwe kiseme nini kinataka.

Sisi tunasema kuwa ilikuwa makosa tangu kuanzishwa kwa Muungano huo kuwakataza wananchi kuujadili na hata kuukosoa kwa nia ya kuuboresha. Tunaishauri Serikali sasa itambue kuwa mhimili wa Muungano ni wananchi, sio watawala.
 
Back
Top Bottom