Elections 2010 Tusikubali kugeuzwa punda

Munkya

Member
Apr 29, 2010
23
0
Huu ni wakati mwingine wa kutafakari umuhimu wa uongozi bora na viongozi wenye ubora unaotakiwa kutupeleka mbele. Hiki ni kipindi kingine cha kujiuliza maswali mengi kuhusu mustakabali wa Taifa letu na kuamua kuchagua watu ambao wanaweza kutuongoza katika kujenga mustakabali huo.
Iwapo tutakitumia kipindi hiki kuuza kura zetu kwa sababu tumepewa bakshish tutakuwa tumeuuza utu wetu na tumejiweka utumwani. Wale wanaotulipa ili tuwachague hawana sababu ya kutuheshimu, kwani tutakuwa tumewasabilia uhuru wetu. Hawana sababu ya kutuchelea kwa sababu tutakuwa tumejiuza kama bidhaa yo yote nyingine inayouzwa sokoni.
Mchapo mmoja uliwahi kuenezwa mitaani Dar es Salaam kubainisha hiki ninachokijadili hapa. Mheshimiwa mmoja alisimama kama mgombea wa kiti cha ubunge katika mojawapo ya majimbo jijini, na akatumia fedha nyingi kuwanunua wapiga kura katika jimbo lake. Ulipofanyika uchaguzi akapata kile wana-malevya wanachokiita “ushindi wa kishindo” na akaingia bungeni,
Baada ya miaka miwili akiwa bungeni, mbunge huyo, ambaye alikuwa mtu mzima na mzoefu katika masuala ya kisiasa, na kisha fedhuli kwa tabia na mwenendo, akatembelea eneo moja katika jimbo lake akiwa na nia ya kuwasalimia wananchi waliompigia kura.
Katika mkutano hupo mheshimiwa huyo alisomewa risala ambayo, pamoja na mambo mengine, ilimtaka mbunge huyo awasaidie wananchi wa sehemu hiyo kupata maji safi, salama na ya uhakika, na pia awasaidie kukarabati barabara yao iliyokuwa imeharibika vibaya. Aidha walimtaka awasaidie kuongeza madarasa mawili ya shule yao ya msingi ambayo ilikuwa haina uwezo wa kuchukua watoto wote waliohitaji shule.
Katikati ya risala, mheshimiwa alimwambia msoma risala akae chini, na kisha mbunge akasimama na kuwakemea wananchi waliokuwa pale kwa kuwaambia: Upuuzi gani huu mnanisomea mimi leo? Mimi nilikuja kwenu nikagawa fedha kila mahali. Mkala, mkanywa, mkapata na kanga na vitenge. Kwa msingi wa fedha zangu mkanichagua niwe mbunge wenu. Tulifanya biashara nzuri tu. Sasa hayo mnayodai niwafanyie mnayatoa wapi?
Ni dhahiri kwamba mtu huyu alikuwa fedhuli na mwenye dharau kubwa kwa wapiga kura. Lakini alichowaambia ni ukweli mtupu: Kwamba walifanya biashara ya kura zao na kwa hiyo hawakuwa tena na haki ya kumdai awafanyie cho chote,
Naamini ujumbe alioutoa mbunge huyu mkongwe ndio ujumbe unaotakiwa kusambazwa kote nchini, kuwaambia wananchi wanaopiga kura kwamba kura ni kitu adhimu kwa sababu kura ndiyo inayowapa uwezo wa kudhibiti maisha yao na kutengeneza mustakabali wao. Wakijiruhusu kurubuniwa na wakaiuza haki hiyo, basi wakubali kuwa bidhaa za huyo waliyejiuza kwake na wala wasitumai kwamba atawafanyia kazi yo yote.
Hapa ningependa tukumbushane mambo madogo yanayoendana na mantiki. Katika hali ya kawaida, ya binadamu wa kawaida kabisa, ukitekenywa unatarajiwa ucheke, na ukifinywa unatarajiwa ulie. Kutekenya na kufinya ni matendo mawili yanayofanana kwa sababu aghalabu yanafanywa kwa kutumia vidole juu ya mwili wa binadamu, lakini matokeo yake ni vitu viwili tofauti kabisa.
Ukitekenywa unatarajiwa ucheke na ukifinywa unatarajiwa ulie. Ukitekenywa kisha ukalia na ukafinywa nawe ukacheka hiyo ni dalili kwamba hisia zako za kimwili zimeingia ‘shoti’ na hazifanyi kazi kama zinavyotakiwa kufanya.
Vivyo hivyo tunatakiwa tujifunze kwamba mtu anayenunua bidhaa ndiye mwenye mali na ataitumia mali aliyoinunua kama anavyotaka, na wala mali hiyo haiwezi kumwambia mnunuzi aitumikie. Kwa hiyo anayekubali kuuuza haki yake ya kura ajue kwamba anauza uhuru wake kwa huyo mnunuzi na wala hawezi tena kudai lo lote kutoka kwa huyo aliyamnunua.
Tunaweza pia kufikiria mfano wa punda. Bwana Ali anakwenda sokoni kununua punda. Punda anayemnunua hawezi kutaraji kwamba Bwana Ali atamtumikia yeye, kwani punda ni mali ya Bwana Ali na ni Bwana Ali mwenye haki ya kumtumikisha huyo punda kama Bwana Ali anavyotaka.
Ikitokea kwamba huyo punda akataraji kwamba Bwana Ali atamfanyia kazi, huyo punda atakuwa amekosa akili kwa kiwango ambacho hata punda hatakiwi kukosa akili. Katika upunda wake, hata punda anajua nafasi yake katika mpangilio wa maisha.
Ni vyema, basi, wananchi waelezwe ukweli kwamba wanapokubali kuuza kura zao wanakuwa wamekubali kununuliwa, na kwamba wakiisha kukubali kununuliwa tofauti kati yao na punda ni ndogo sana. Hawana budi kukubali kumtumikia Bwana Ali aliyewanunua.
Sina shaka kwamba idadi ya wananchi wanaogundua kwamba wameingizwa katika biashara isiyokuwa na tija kwao inaongezeka kila kipindi cha uchaguzi kinapokaribia, na sina shaka kwamba siku itafika wananchi walio wengi watakataa kuwa punda. Lakini siku hiyo bado iko mbali, na jukumu la wazalendo ni kuiharakisha ifike mapema iwezekanavyo.
Hii inatokana na ukweli kwamba biashara ya siasa imewanufaisha watu wengi mno. Katika nchi yetu, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, siasa ndicho kiwanda kisichohitaji lo lote kukifanya kizalishe, alimradi mtu anajua “kupiga domo.” Hivi sasa inadhihirika zaidi na zaidi kwamba ukitaka utajiri wa haraka na nafasi katika jamii inayotokana na heshima-hewa unachotakiwa kufanya ni kuingia katika siasa.

Kwa kuwa siasa zetu ni za uongo, na kila anayeweza kusema uongo kuliko wengine ndiye mwanasiasa bora, waongo wamejazana katika siasa, wakichuana katika mashindano ya udanganyifu. Huu ndio msimu wa kuwaona kwa mara nyingine tena wakipita na kujinadi. Huu ni msimu mwingine wa uongo, ulaghai na ahadi zisizotekelezeka wanazotoa wanasiasa, bila haya wala kupepesa kope, huku wakijua kwamba wanachokiahidi hakitekelezeki.
Labda hatuwezi kuwazuia wanasiasa kutembeza uongo wao, kwani hiyo ndiyo silika yao. Inawezekana kwamba kutaka kuwazuia wanasiasa kusema uongo ni sawa na kujaribu kumzuia mbwa kubweka. Lakini tunaweza angalau kuwatanabahisha wananchi wetu kuhusu mibweko isiyokuwa na maana isipokuwa kuwadanganya wananchi ili wanaobweka waneemeke kupitia migongo ya wananchi waliokubali kurubuniwa. Hili tunaweza kulifanya. Wapo walioanza kulifanya kwa kutoa elimu ya uraia kwa wapiga kura na kwa kuendesha kampeni za makusudi kabisa kupambana na udanganyifu huu unaotuuumiza. Hatuna budi kuendelea, kwa sababu iwapo tutakata tamaa, iwapo tutajiruhusu kuamini kwamba hatuwezi kitu dhidi ya nguvu ya hawa wanunuzi na wauzaji wa kura, tutakuwa tumekubali kuwa punda, tena punda wa dobi.
 
Back
Top Bottom