Tusijiliwaze: Utajiri wa mali asili umekwisha!

Kuhani

JF-Expert Member
Apr 2, 2008
2,944
64
%5Cmajitatizobado.jpg

Wakazi wa Tabata Sheli na maji ya dimbwi kwa matumizi ya nyumbani​


Tusisahau; vita ijayo ni ya kugombea ardhi na maji!



Raia Mwema
26-11 to 2-12, 2008


mbwambo.jpg



Na Johson Mwambo



LEO, hisia zangu zinanisukuma nizungumzie suala la uharibifu wa mazingira nchini mwetu.

Kwanza, ni kwa sababu najiandaa kwenda likizo kijijini, na kila ninapofikiria kijijini; suala la uharibifu wa mazingira vijijini hurejea katika fikra zangu na kunikosesha raha.

Jambo la pili lililonichochea kuandika leo kuhusu mazingira ni picha iliyochapishwa ukurasa wa nne wa gazeti la Mwananchi (toleo la Novemba 17, 2008) ya lori lililosheheni vipande vya magogo likivipeleka kwenye kiwanda cha nguo cha 21st Century Textiles Ltd kilichopo Kihonda, Manispaa ya Morogoro.

Maelezo ya picha hiyo yanasema kwamba kiwanda hicho hutumia nishati ya kuni ili kuzalisha umeme kwa ajili ya uzalishaji. Hebu fikiria ni miti (misitu) kiasi gani inateketezwa mkoani Morogoro ili kiwanda hicho kipate kuni za kuzalisha umeme!

Hebu fikiria; tupo karne ya sayansi na teknolojia, lakini bado tuna kiwanda cha nguo kinachotumia nishati ya kuni kuendesha mitambo ya kutengeneza nguo! Si nishati; angalau ya sola, kuni?! Kwa nini Serikali imeruhusu kiwanda kama hicho ambacho ni adui mkubwa wa mazingira?

Lakini tatu, ni kwa sababu zimebaki takriban wiki mbili kabla ya kufikia Desemba 19 - ile tarehe muhimu ambayo wanamazingira kote duniani hawataisahau.

Desemba 19, mwaka 1987, ni tarehe ambayo binadamu na viumbe vyote hai walianza rasmi kuishi kwa kutumia maliasili za dunia kwa "utaratibu wa kukopa".

Kwa maneno mengine, ni tarehe ambayo binadamu tulivuka rasmi uwiano wa utumiaji wa maliasili zilizopo duniani na urejeshwaji wake. Ni tarehe ambayo kiwango tunavyozitumia maliasili au kuzipora, kilipoacha kulingana na kiwango kinachorejeshwa na mfumo asilia.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba, kuanzia Desemba 19, 1987 (Miaka 21 iliyopita), tumekuwa tukichota zaidi maliasili kutoka katika dunia yetu kuliko uwezo wa mfumo asilia wa kuzirejesha.

Pengo hilo kati ya uchotwaji na urejeshwaji wa maliasili limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka, na kuleta balaa kubwa sehemu mbalimbali duniani. Ni dhahiri sababu kubwa ya kuongezeka kwa pengo hilo ni kuongezeka kwa idadi ya watu duniani.

Wataalamu wa mazingira na wanasayansi maarufu duniani wamekwisha bainisha wazi kwamba dunia yetu haiwezi tena kuhimili idadi ya watu, takriban bilioni sita waliopo hivi sasa duniani.

Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, binadamu wamepora kwa kasi mno maliasili alizotuwekea Mungu duniani – iwe ni maji, ardhi, miti au hewa – na sasa wakati wa kulipa makosa hayo umewadia!

Takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia mbili tu ya maji yote duniani ambayo kwa sasa ni salama kwa matumizi ya binadamu. Akiba ya mafuta ardhini nayo inakauka kwa kasi, samaki katika bahari wanazidi kupungua.

Isitoshe, maziwa, mito na mabwawa makubwa nayo yanapungua vina kwa kasi ya kutisha. Misitu inapotea, ardhi nayo inalimwa kupita kiasi (over-farming) na matumizi ya mbolea za kemikali yamedhoofisha mno ardhi ya dunia na kufanya mavuno yawe duni mwaka hadi mwaka.

Ni wazi kwamba mambo yote hayo huashiria balaa tupu kwa maisha ya binadamu hapa duniani; na chanzo ni matendo ya binadamu yanayotokana na ongezeko la watu na uharibifu wa mazingira.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka juzi za Jumuiya ya Madola, watu bilioni sita duniani watakosa kabisa huduma ya maji ifikapo mwaka 2,050 kutokana na kutoweka kabisa kwa vyanzo vya maji katika uso wa dunia.

Kwa hakika, wataalamu hao wanatabiri kwamba vita vijavyo duniani vitakuwa ni vya kugombea vyanzo vichache vya maji vitakavyokuwepo na ardhi kidogo yenye rutuba itakayobakia, na kwamba vita hizo zitakuwa na umwagaji damu mkubwa.

Hatari hii ya ongezeko kubwa la watu lisiloendana na maliasili chache zilizopo na pia uharibifu wa kasi wa hizo chache zilizopo, tayari imeshaanza kuonekana hapaTanzania.

Mapambano ya hivi karibuni kati ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wilayani Kilosa, yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa, ni mfano wa hivi karibuni tu wa hicho ninachokizungumzia.

Na haitakuwa wakulima dhidi ya wafugaji tu; bali hata wafugaji kwa wafugaji wenyewe na wakulima kwa wakulima wenyewe, na hata wavuvi kwa wavuvi wenyewe!

Katika wilaya ya Mwanga, kwa mfano, Ziwa Jipe linakauka kwa kasi na karibu wavuvi wote waliokuwepo hapo wamehamia katika bwawa la Nyumba ya Mungu na kusababisha shinikizo kubwa kwa bwawa hilo ambalo tayari limefurika wavuvi.

Tunasoma pia taarifa za mara kwa mara kwamba kina cha Ziwa Victoria – ziwa kubwa kushinda mengine yote barani Afrika, kinapungua kwa kasi na kwamba miaka si mingi, meli zitashindwa kabisa kutia nanga katika bandari za ziwa hilo.

Sambamba na kupungua kwa kina cha ziwa hilo, samaki nao wamepungua mno na aina fulani zimetoweka kabisa. Ni dhahiri muda si mrefu wavuvi katika ziwa hilo watalazimika kuhamishia uvuvi wao katika vyanzo vingine vya maji na kuongeza shinikizo ambalo tayari liko kwenye vyanzo hivyo.

Lakini si hayo tu. Sote tunajua vilevile, kwa mfano, kwamba ongezeko la watu mkoani Kilimanjaro limesababisha wenyeji wengi wa mkoa huo (Wachaga na Wapare) kuhamia mikoa mingine yenye ardhi na vyanzo vingi vya maji, na kusababisha shinikizo la matumizi ya maliasili katika maeneo hayo ambayo nayo tayari yameshaanza kujaa watu.

Sote tunajua vilevile kwamba baada ya wafugaji wa Kisukuma wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza kukata miti hovyo na kuharibu maliasili zao, sasa wamehamia maeneo mengine yakiwemo ya Morogoro, Mbeya na Ruvuma ambako pia wamesababisha shinikizo kubwa kwa vyanzo vya maji vilivyoko huko ambavyo vinawatosha watu wachache.

Kwa hiyo, wanamazingira na wanasayansi wanaposema kwamba dunia yetu sasa inashindwa kuhimili idadi ya watu waliopo, na kwamba sasa matumizi yetu ya maliasili zilizopo duniani ni ya "kukopa", mifano ipo hapa hapa Tanzania. Unahitaji tu kuutembelea mkoa wa Kilimanjaro au Mbeya kuelewa hicho wanachokisema wanamazingira na wanasayansi.

Swali la kujiuliza ni je: Tusubiri hadi maliasili zote zitoweke kabisa na kuanza kupigana wenyewe kwa wenyewe kugombea chache zilizopo ndipo tuchukue hatua? Maana tumeambiwa kuwa vita vijavyo vitakuwa vya kugombea maliasili chache zitakazopatikana kama vile maji na ardhi yenye rutuba.

Kwa mtazamo wangu, tunapaswa kuchukua hatua sasa kwa kufanya mambo mawili. La kwanza ni kuwa wakali kuhakikisha Sheria Mama ya Mazingira iliyopitishwa na Bunge mwaka 2004 inawang'ata kweli kweli waharibifu wa mazingira nchini. Mpaka sasa hatujayaona meno ya sheria hiyo kivitendo.

La pili (na hili ni muhimu na nyeti) ni kufanya tafiti kuona kama kweli maliasili zilizopo (hasa maji na ardhi yenye rutuba) zinalingana na idadi ya watu zaidi ya milioni 40 waliopo hivi sasa nchini.

Hisia za wanamazingira wengi nchini ni kwamba maliasili tulizonazo tunazikausha kwa kasi; kiasi kwamba zimeanza kushindwa kuhimili idadi ya watu zaidi ya milioni 40 waliopo sasa.

Tunahitaji kufanya tafiti kuthibitisha hilo. Na kama tafiti hizo zitathibitisha hivyo, basi, ni vyema tukaliangalia upya suala zima la ongezeko la idadi ya watu Tanzania, na pengine kufikiria kutunga sheria inayoweka ukomo idadi ya kuzaa watoto kwa kila familia.

Wenzetu China walijihami mapema kwa kutunga sheria ya namna hiyo, na nchi kama Nigeria imeathirika mno kwa kutokuwa na sheria ya namna hiyo ; kiasi kwamba nayo sasa imeanza kuifikiria!

Najua jambo hili ni gumu kukubalika kirahisi katika nchi kama ya kwetu yenye tamaduni na imani zinazotukuza suala la kuzaa watoto wengi, lakini hizi si nyakati za kawaida. Ni nyakati ngumu na zisizo za kawaida zinazohitaji hatua zisizo za kawaida!

Najua wapo watakaosema kuwa Tanzania ni nchi kubwa na yenye mapori mengi yaliyo matupu; hivyo tuzaliane na kuzaliana tu! Hoja, hata hivyo, si ukubwa wa nchi; bali ni wingi wa maliasili zilizopo. Hakuna maana yoyote kuwa na nchi kubwa kama Sudan yenye vyanzo vichache mno vya maji visivyotosheleza watu hata milioni mbili tu!

Kama wanasayansi wanasema kwamba ifikapo mwaka 2,050 watu bilioni sita duniani hawatakuwa kabisa na huduma ya maji, kwa nini sisi tujione tu salama?

Ni kwa muktadha huo huo naunga pia mkono msimamo wa Serikali ya Tanzania wa kutokubali masuala ya miliki ya ardhi, makazi ya kudumu na uraia, kuwa sehemu ya makubaliano ndani ya Muundo wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Tukiyakubali mapendekezo hayo ya EAC, ni dhahiri Wakenya ambao wana uhaba mkubwa wa ardhi yenye rutuba watakimbilia kuhemea kwetu, na hilo litakuwa balaa.

Maana, kama Wakenya wenyewe tayari wameshaanza kutoana damu kugombea ardhi ndogo yenye rutuba iliyosalia kwao (rejea mgogoro na skandali ya hivi karibuni ya Mt. Elgon), tukiwaruhusu waje Tanzania, si watatumaliza kabisa?

Ujumbe wangu ni kwamba tusisahau (lest we forget) kwamba vita ijayo itakuwa ya kugombea ardhi na vyanzo vya maji; hivyo natuzilinde na kuzithamini maliasili hizo ambazo bado tunazo.

Tafakari!
.........................................................................

Email: mbwambojohnson@yahoo.com

___________________
 
Ndo maana wakenya wamemind tunavyouweka usiku ktk kuunda shilikisho la EA
 
Back
Top Bottom