Tunduru walia na madaraka ya Rais

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
Sunday, 02 September 2012 12:03

00000000000000000000000000aaatunduru.jpg
Wajumbe wa Tume ya Katiba, Fatuma Said Ally, Ally Saleh na Profesa mwesiga Baregu wakimsikiliza mwananchi anayetoa maoni katika kijiji cha Nandembo wilayani Tunduru jana. Picha na Elias Msuya.

Elias Msuya
TUME ya Mabadiliko ya Katiba iko katika awamu ya pili ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu wanataka nini kingie katika Katiba Mpya. Kwa sasa Tume hiyo imegawanyika katika makundi saba yakizunguka kote nchini kwa ajili ya kukutana na wananchi ili watoe maoni yao.
Moja ya kundi la Tume hiyo linaloongozwa na Profesa Mwesiga Baregu liko katika mkoa wa Ruvuma ambako linatarajia kufanya mikutano ipatayo 60.
Wakiwa wilayani Tunduru, wamekutana na wananchi katika vijiji vya Lukumbule, Mchesi, Mapinduzi, Muungano, Nyerere, Angalia na Mtina, ambako pamoja na mambo mengine, wananchi wamenyooshea kidole suala la ukubwa wa madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na kutaka yapunguzwe katika Katiba ijayo.
Awali Profesa Baregu alitoa mwelekeo wa maoni yanayotakiwa kutolewa kuwa ni pamoja na masuala ya amani na utulivu, demokrasia, mfumo wa Serikali, madaraka ya rais na mambo mengine katika mihimili ya utawala.
Vilevile Profesa Baregu aliwaambia wananchi kuwa wanayo nafasi ya kuujadili Muungano na hata suala la mgombea binafsi.
Kadhalika wanaweza kuelezea maoni yao kuhusu Tume ya Uchaguzi, masuala ya umiliki wa ardhi, maliasili, ulinzi na usalama sambamba na suala zima la haki za binadamu.
Akitoa maoni yake mwananchi kutoka kijiji cha Mchesi, Bakari Naliwila yeye anaguswa na mamlaka ya Rais ya uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya na kwamba wengi wao huwa pia wana majukumu mengine kama vile ubunge, hivyo kushindwa kufanya kazi za maendeleo katika wilaya/mikoa yao kwa sababu kwa muda mrefu huwa hawaonekani katika maeneo yao ya kazi.
“Rais apunguziwe madaraka ya kuteua wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Rais anateua, lakini unapita muda mrefu hatuwaoni, labda kuwe na chombo kingine kitakachosimamia shughuli za wananchi,” anasema Naliwila na kuongeza;
“Mawaziri wasitokane na wabunge, suala la kulindana litakwisha, kwa sababu akitokea nje hataweza kulindwa na mfumo uliopo.”
Naye Malaje Daudi licha ya kutaka madaraka ya Rais yapunguzwe, ametaka Katiba Mpya iseme wazi kuwa huduma za afya na elimu zitolewe bure.
Mwananchi mwengine, Zuberi Mtojima licha ya kutaka Katiba imtambue mkulima, anataka Katiba Mpya impe Rais kipindi kimoja cha miaka 10 bila kuwa na chaguzi za miaka mitano kwani zina gharama kubwa kwa taifa.,
“Kama Rais anakaa miaka 10 madarakani, baada ya miaka mitano tunachagua tena, sijawahi kuona Rais anashindwa uchaguzi huo. Tunapoteza bure fedha za umma, bora Rais aendelee tu, amalize muhula wa mika kumi. Katiba mpya iseme kama rais akishindwa kazi kati kati ya madaraka yake wananchi wamtoe na iweke njia za kumuondosha Rais madarakani,” anasema Mtojima.
Msaka Mohamed yeye anasema kuwa Katiba Mpya itamke wazi kuwa Rais akiugua atibiwe hapa nchini kwani siku zote amekuwa akidai kuwa hali ya afya imeimarika nchini.
Vilevile ametaka Katiba Mpya itamke kiwango cha mshahara na posho za Rais.
“Katiba imbane Rais kwamba, kama ataahidi kuleta maendeleo kama vile kujenga barabara na asifanye basi ashitakiwe. Tunataka pia katiba itaje mshahara na posho zake ili wananchi waelewe Rais analipwa,” anasema Mohamed.
Kwa upande wake Hussein Said wa kijiji cha Mchesi anasema Rais amepewa madaraka makubwa ya kuteua viongozi wasio chaguo la wananchi kama vile wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na mawaziri ambao hulipwa mishahara minono huku viongozi wa ngazi za chini kama vile wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanaowajibika moja kwa moja kwa wananchi wakiwa hawalipwi mishahara.
“Wateule hao wa Rais hawana kazi kubwa kama wakurugenzi, wenyeviti wa vijiji na wenyeviti wa vitongoji, lakini wanalipwa vizuri,” anasema.
Naye Rajab Sinzi anataka viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wasiteuliwe na Rais, badala yake wateuliwe na Bunge.
Suala la dini
Wakazi wengi wa wilaya ya Tunduru ni waumini wa dini ya Kiislamu, katika maoni yao wametaka Katiba itamke kuwa Serikali ina dini na kwamba siku ya Ijumaa iwe siku ya mapunziko kwa Waislamu kama zilivyo siku za Jumamosi na Jumapili kwa Wakristo.
“Mimi, nataka Katiba itambue siku ya Ijumaa iwe ni siku rasmi ya Waislamu kupumzika, mbona Wakristo wao wanapumzika siku zao,” anahoji Khalifa Issa Yasin kutoka kijiji cha Lukumbule.
Naye Abdallah Chombo kutoka kijiji cha Mchesi ametaka Katiba iunde Serikali yenye dini na kuepuka kuingilia imani za watu.
“Tunataka Katiba Mpya itambue uwepo wa Mwenyezi Mungu na pia iItambue sheria zake. Serikali isilazimishe mtu kufuata sheriaambazo zinakwenda kinyume na imani…,” anasema Chombo.
Kwa upande wake Jawad Omar ametaka Katiba iruhusu kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi na Tanzania ijiunge na OIC ili ipate misaada kutoka katika umoja huo.
Hamza Hassan ametaka Katiba itamke i-kuwa ina dini; “Serikali inasema haina dini, lakini Bunge linasema Mungu ibariki Tanzania, Mungu gani huyo?
Hata hivyo Crispin Swalehe Mkaitana anapinga suala la Serikali kuwa na dini kwani litaleta michanganyo.
“Serikali isiwe na dini, kwani kama ikiruhusiwa kuwa na dini itakuwa ya dini ipi?” anahoji Swalehe.
Anazungumzia pia suala la ardhi akisema kuwa inapaswa kumilikiwa na Serikali lakini itengwe pia ardhi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, michezo ili kupunguza migogoro ya ardhi.
Ameshauri pia kuwapo kwa dira ya taifa, ili kila chama kinachoingia madarakani kifuate dira hiyo, tofauti na sasa ambapo kila chama kinafuata ilani yake.
Kuhusu suala la mgombea binafsi analiunga mkono huku akishauri kuwa endapo kiongozi wa siasa aliyechaguliwa na wananchi akifukuzwa na chama chake asipoteze nafasi yake.
Kuhusu Muungano anasema kuna haja ya kuurekebisha ili upande wa bara uwe na Bunge lake kama lilivyo Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Mbali na hoja hizo, wananchi hao pia wamejadili masuala mengine ya kitaifa ambapo Hassan Rajab amegusia suala la mgombea binafsi akisema halifai kwani kama ataruhusiwa itakuwa vurugu.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi ametaka viongozi wake watokane na vyama vya siasa ili kuepusha migogoro inayovihusisha vyama hivyo na Tume.
Akizungumzia suala la Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, Rajab anasema haoni umuhimu wa Muungano huo kwa kuwa haueleweki,
“Muungano huu ufutwe, tangu nimezaliwa sioni umuhimu wake. Tunasena kuna muungano wakati kule kuna baraza la mapinduzi, marais wa wawili wa nini. Kama muungano upo basi kuwe na Serikali moja na Rais mmoja,” anasema.
 
hii nimeipenda,
"Tunataka Katiba Mpya itambue uwepo wa Mwenyezi Mungu na pia itambue sheria zake. Serikali isilazimishe mtu kufuata sheria ambazo zinakwenda kinyume na imani…,".

walivyo wanafiki, eti wakiwa wanaanza kile kikao chao cha mazingaombwe "BUNGE" huwa wanajifanya kumuomba Mwenyezi Mungu, halafu hapo hapo hawataki kutumia sheria zake alizoziteremsha kwenye vitabu vyake vitakatifu kama vile TAURATI, ZABURI, INJILI na QUR'AN. wanamuomba Mwenyezi Mungu, halafu hapo hapo hawataki kutii sheria zake, sijui huwa wanatumia aya gani za BIBLIA au QUR'AN ambazo zinaruhusu tu kumuomba, na sio kutumia SHERIA ZAKE kuhukumu, WATU WAZIMA LAKINI FULL MAIGIZO, sijui wana matatizo ya akili hawa wanaojiita wenye mamlaka.



Tuendeleeni kuwaelimisha watanzania, ili waelimike waling'oe madarakani hili li serikali la ccm MAONGO/MAFISADI/MAJAMBAZI/WAUAJI.
 
Back
Top Bottom