Tunashindwa kuwaelewa viongozi na ngonjera za ufisadi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Date::9/1/2008
Tunashindwa kuwaelewa viongozi na ngonjera za ufisadi
Elias Msuya
Mwananchi

KWA mara nyingine tena Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amerudia kosa lile lile alilolifanya bosi wake, Rais Jakaya Kikwete kwa kushindwa kuwawajibisha watuhumiwa wa ufisadi wa kashfa ya zabuni ya umeme wa dharura wa kampuni ya Richmond.

Katika taarifa yake aliyoitoa Bungeni kuhusu utekelezaji wa Serikali wa mapendekezo 23 ya kamati ya Richmond, Pinda alibainisha mambo kadhaa ambayo Serikali imeyachukulia hatua na mengine ikayaachia kwa ajili ya mamlaka nyingine zinazohusika.

Katika mapendekezo yote yaliyotolewa, watu wengi tulikuwa na shahuku hasa ya kutaka kuona kama kweli Serikali ina ubavu wa kuwawajibisha watuhumiwa wa ufisadi?

Lakini taarifa ile ya Waziri Mkuu, Pinda ilipiga chenga suala hilo na kulirushia kwa wengine. Watuhumiwa hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, waliokuwa mawaziri wa Nishati na madini, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha ambao walijiuzulu mara tu baada ya kamati ya Richmond iliyokuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe kuwabainisha kama watuhumiwa.


Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Pinda, Mawaziri hao, (Karamagi na Msabaha) sasa watachunguzwa na vyombo vya dola ili kubaini kama walikula rushwa katika mchakato wa kupitisha zabuni ya mkataba wa Richmond.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, Dk Edward Hosea, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Arthur Mwakapugi na Kamishna wa Nishati, Bashir Mrindoko. Hawa walikataa kujiuzulu licha ya kutajwa kwenye kamati ya Mwakyembe.

Waziri Mkuu Pinda alisema kwamba hao wameshaandikiwa barua wakajieleze kwa Rais Kikwete kwa kuwa ndiye aliyewateua na ndiye mwenye mamlaka ya kikatiba ya kuwaondoa.

Pinda aliendelea kufafanua kwamba, Hosea na Mwakapugi wametakiwa kwenda kuijieleza kwa Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, ambaye atatoa maelekezo kwa Serikali namna ya kutekeleza maamuzi hayo.

Baada ya taarifa hiyo ndefu ya Waziri Mkuu, Watanzania tumebaki tumeduwaa. Tunashindwa kuwaelewa hawa viongozi wetu na ngonjera zao dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Pinda amerudia kosa lile lile alilolifanya Rais Kikwete alipokuwa akilihutubia Bunge hivi karibuni, aliushangaza umma pale aliposhindwa kutaja majina ya mafisadi wa EPA.

Yaani Rais Kikwete alionyesha wazi wazi namna alivyowakingia kifua watuhumiwa wa ufisadi wa EPA. Ndiyo maana hata baada ya hotuba yake, Spika wa Bunge, Samuel Sitta alimshangaa Rais Kikwete kwa kuwa na huruma na mafisadi eti kwa kisingizio cha haki za binadamu.

Kisingizio hicho hicho ndicho alichokuja nacho Waziri Mkuu Pinda. Eti Serikali haikurupuki, inafanya kazi kwa kufuata sheria. Sheria gani hizo? Mbona Serikali inajali sana sheria pale vigogo wake wanapotuhumiwa? Wanapotuhumiwa walalahoi hakuna cha sheria wala taratibu zinazozingatiwa.

Taarifa hii ya utekelezaji wa mapendekezo ya kamati ya Richmond, imechukuwa muda wa miezi sita hadi kukamilika. Lakini tunacholetewa leo ni ahadi tu kwamba serikali inaendelea kuwachunguza, mara hatua zitachukuliwa na mamlaka husika. Hivi kwa mwendo huu wa konodkono ufisadi utakwisha katika nchi hii?

Alichokifanya Pinda ni sawa na mshambuliaji wa mpira wa miguu ambaye amewapita wapinzani wake wote akabaki na golikipa, halafu badala ya kufunga goli, anaurudisha mpira nyuma kwa beki, eti anamtaka beki ndiyo afunge. Ukiwauliza wataalamu wa michezo watakwambia kwamba mchezaji kama huyu lazima tu atakuwa amehongwa na timu pinzani.

Haiwezekani mchezaji akamwonea huruma mpinzani wake huku anajua fika kwamba kwa kufanya hivyo atajihatarishia ushindi wake. Kwa hali hii inawezekana kuna namna inayochezwa kati ya mafisadi na viongozi wetu. Haiwezekani viongozi wetu wa Serikali walio na mamlaka yote na vitendea kazi vyote washindwe vita dhidi ya ufisadi. Ni lazima kuna namna!

Kama kamati ya Mwakyembe iliweza kufanya kazi kwa muda mfupi tu kwa ufanisi, inawezekana kuumaliza ufisadi katika nchi hii kwa kipindi kifupi tu. Inawezekana kuwawajibisha mafisadi ndani ya kipindi kifupi tu kwa sababu ushahidi wote upo.

Tangu sakata la Richmond lilipoanza kuvuma na kuwabainisha watuhumiwa waliohusika, Rais Kikwete hakuchukua hatua yoyote. Tena kibaya zaidi ndiyo aliwachukuwa watuhumiwa, akina Mwanyika na Hosea akawapa kazi ya kuchunguza ufisadi wa EPA. Jamani, Watuhumiwa wa ufisadi tena wachunguze tuhuma za ufisadi? Haya wamechunguza, kilichopatikana ndiyo hayo mauzauza yaliyotangazwa na Rais Kikwete hivi karibuni.

Huyu Hosea ndiye aliyeisafisha kashfa ya Richmond, akadhani yamekwisha. Kumbe moto ndiyo kwanza unaanza kuwaka.

Bila shaka nchi hii itaendelea kuandamwa na kashfa za ufisadi daima. Ni mpaka viongozi watakapoamua kubadilika. Ufisadi huu wanaulea kwa makusudi kabisa.

Tatizo ni kwamba hata viongozi wenyewe wameingia madarakani kwa misingi ya kifisadi. Mafisadi hao ndiyo waliofadhili mikutano ya kampeni, wakatoa fedha, magari, vipeperushi, fulana na kofia. Sasa viongozi hao waliposhinda kwa kishindo ndipo nao wakaanza kurudisha fadhila walizokopwa na mafisadi.

Ndiyo maana leo viongozi wetu wanaona haya kuwashughulikia mafisadi, wanaishia kurushiana mpira tu, mara litashughulikiwa na Rais mwenyewe, mara Katibu Mkuu Kiongozi, mradi tu siku zinakwenda na watu wanaendelea kudunda mitaani.

Hotuba ya Waziri Mkuu Pinda kama ilivyokuwa ya Rais Kikwete zimewekwa kiporo kujadiliwa hadi kwenye kikao kijacho cha mwezi Novemba. Wamefanya hivyo kwa makusudi ya kuzima mijadala kuhusu maamuzi hayo ya Serikali.

Yawezekana viongozi wetu hawana dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi.

Simu:0754 897 287
 
Back
Top Bottom