Tunaomba Polisi wachukue hadhari zaidi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
maoni%20ya%20katuni%2030.jpg

Maoni ya Katuni


Jumatatu wiki hii tuliripoti habari ya kusikitisha ya kuuawa askari polisi kanzu mwenye cheo cha sajini wa kituo cha Polisi Sirari wilayani Tarime, mkoani Mara.

Askari huyu kwa mujibu wa habari za kipolisi aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kulia na mtu aliyekuwa anatuhumiwa kutishia kuua.

Mbali na mauaji hayo mtuhumiwa ambaye alitenda uhalifu huo pia anadaiwa kuwajeruhi askari wengine wawili ambao walikuwa na marehemu wakimsaka, wote wamelazwa hospitalini wakipatiwa matibabu huku mtuhumiwa akidaiwa kuwatoroka baada ya kufanya mauaji hayo.

Tunasikitika kuwa taifa kimepoteza askari wake akiwa kazini. Tunawapa pole wote walioguswa na msiba huu, tunawaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu; tunawatakia kila la heri majeruhi ili wapone haraka na kurejea katika wajibu wao adhimu wa kulinda maisha na mali za raia.

Hili siyo tukio la kwanza kuuawa kwa askari polisi akiwa kazini, wapo waliokufa wakipambana na majambazi kwa kurushiana risasi, wapo waliokufa wakifukuzana na wahalifu, kwa ujumla matukio ya kufa kwa askari akiwa kazini yameripotiwa mara nyingi nchini. Mara zote tumesema na tunasisitiza leo kwamba kupoteza askari kwa sababu zozote zile ni hasara kwa taifa.

Askari huyu anauawa alipokuwa amekwenda na wenzake kumkamata mtuhumiwa ambaye alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kutishia kuua kwa panga, askari hao walipomfuata na kumwamuru waende naye kituo cha polisi aligoma na kuchomoa kisu na kuanza kuwashambulia.

Kumbukumbu zetu zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji dhidi ya askari polisi ni la tatu kutokea katika Mji Mdogo wa Sirari katika kipindi cha mwaka mmoja; mwaka jana, askari polisi mwingine aliuawa pia kwa kuchomwa kisu tumboni wakati wa msako katika ofisi ya Sungusungu polisi walipokwenda kuwakamata watuhumiwa wa wizi katika ofisi ya Kitongoji cha Sokoni ambako mtuhumiwa ambaye anadaiwa kuwa raia wa Kenya aliwachoma visu na kuwaua watu wawili, akiwemo askari huo. Mwingine aliyeuawa katika tukio hilo la mwaka jana alikuwa mpakia mizigo katika soko hilo.

Matukio mengine ni majambazi kuvamia baa ya China na kuwaua watu wawili, akiwemo askari polisi, ambaye alipigwa risasi kifuani, aliuawa pamoja na mhudumu wa baa hiyo.

Matukio haya yanaonyesha kuwa Mji wa Sirari ni moja ya maeneo hatari siyo kwa raia tu, bali hata kwa walinda usalama wenyewe, ndiyo maana matukio ya mauaji dhidi ya raia na hata askari polisi yemekuwa yakitokea mara kwa mara.

Tunajua askari wetu wamefuzu mafunzo yao, wanajua jinsi ya kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa; ndiyo maana hapana shaka waliamua mwenda watatu kumkamata mtuhumiwa ambaye ni dhahiri kuwa ni mtu hatari katika jamii. Walikuwa watatu ili wamdhibiti mtuhumiwa kirahisi na kumfikisha kituoni kwa hatua zaidi za kisheria dhidi yake.

Ingawa wahenga walituasa kuwa ukijikwaa usijisumbue na ulipoangukia bali ulipojikwaa, nasi tunachukua wasaa huu kulitaka Jeshi la Polisi kuzingatia msemo wa wahenga, lakini pia tungependa kuona wakipiga hatua moja mbele zaidi kutafakari hata walipoangukia.

Ni kweli polisi wamekuwa wakilaumiwa sana kuwa wanatumia nguvu kupita kiasi wakati wa kukamata watuhumiwa, kwa maana hiyo kwa sasa wanaweza kuwa wanasukumwa na mkakati wa utii wa sheria bila shuruti na polisi jamii katika kutimiza wajibu wao, kwa hakika pamoja na uzuri na haja ya polisi kubadilika katika kutimiza wajibu wake kwa kuwa na mwelekeo wa mahusiano chanya zaidi kwa jamii, bado hadhari ya hali ya juu inapachwa kuweko kati ya tukio na tukio.

Tumesema hapo juu kwamba tunaamini polisi wana weledi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao, na tunaamini pia kuwa wamefuzu vizuri katika kutekeleza wajibu wao, lakini pia ni vizuri wakakumbuka kwamba kujipeleka kumkamata mtuhumiwa anayeripotiwa kuwa alikusudia kuua kwa panga bila nao kujihami sawasawa ni hatari pia.

Tunasema kuwa polisi wajue wakati wote kuwa wanapokwenda kumkamata mtuhumiwa yeyote ni vizuri sana wakaongozwa na mbinu za kiaskari wakati wote kwamba siyo kila mtuhumiwa anakuwa radhi kuonyesha ushirikiano, mara nyingi tumeona jinsi mataifa yaliyopiga hatua za maendeleo yanapokabiliana na watuhumiwa wenye tuhuma nzito kama za mauaji, kutishia kuua au kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Tunaomba askari wetu wasizoee sana kuamini kwamba mtuhumiwa ni mtu wa kufuatwa bila hadhari za kiusalama. Tunasikitika kumpoteza askari huyu, lakini yaliyotokea yafungue macho na masikio ya askari wetu jinsi ya kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu nchini.





CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom