Tumevuka lengo la nafasi za uwakilishi wa wanawake

kalld

Member
Jun 14, 2007
87
0
jee hii kampeni ya kukataa ukatili dhidi ya wanawake itafikia malengo?
kuna unyanyasaji wa watoto na kina mama ,jee kina baba hawanyanyaswi?



Kikwete: Tumevuka lengo la nafasi za uwakilishi wa wanawake
Na Mwasu Sware


HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete alizindua kampeni ya kimataifa ya kukataa ukatili dhidi ya wanawake katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.


Wazo la kampeni hiyo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki-Moon na Naibu wake Dk Asha-Rose Migiro wakati wa kikao cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake kilichofanyika New York, Marekani Februari 25 mwaka huu.


Akizungumza na wananchi katika uzinduzi huo Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi kama njia mojawapo ya kupambana na ukatili dhidi yao na watoto.


Kikwete anasema Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa ukiwemo wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW), na kwamba imedhamiria kuitekeleza kwa kuongeza idadi ya viongozi wanawake hatua kwa hatua mpaka itakapofika asilimia 50.


?Nimeona mkipita na bango lisemalo asilimia 30.1 ya wanawake waliopo kwenye uwakilishi haitoshi. Hata hivyo, tumejitahidi kweli kuifikisha hapo ilipo tuliweka nia ya kufikia asilimia 30 lakini sasa tumevuka lengo. Tutaendelea kuongeza idadi ya wanawake hatua kwa hatua hadi itakapofikia asilimia 50,? anasema Kikwete.


Hata hivyo, Kikwete alikemea tabia ya wanawake kudharauliana na kuoneana wivu wenyewe kwa wenyewe badala ya kusaidiana na kuonya kuwa tabia hiyo inadhoofisha juhudi za Serikali katika kutekeleza malengo yake.


Badala yake aliwataka kushirikiana na kusaidiana hasa nyakati za uchaguzi ili kuhakikisha wanapata nafasi zinazotoa maamuzi.


?Serikali yangu imeweka mikakati maalum ya kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za uongozi kwenye ngazi mbalimbali zinazotoa maamuzi ili kushiriki kikamilifu katika kushughulikia maeneo yote yanayokiuka haki za wanawake na watoto,? anasema Kikwete


Anawataka wanawake kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na waume zao ili sheria zichukue mkondo huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuzifanyia mabadiliko sheria zote zinazoendeleza vitendo vya ukatili dhidi yao na watoto.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margaret Sitta anasema lengo la kuwepo kwa kampeni hizo ni kukusanya saini milioni moja za wananchi kwa kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono kampeni hiyo ya kutimiza lengo la kuchukua hatu zaidi za kutokomeza vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake katika nchi wanachama.


?Licha ya kuwa tunapinga ukatili dhidi ya wanawake, lakini katika nchini yetu tumeamua kuingiza na ukatili dhidi ya watoto katika kampeni hii kwa kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto navyo vimekithiri sambamba na vya wanawake,? anasema Sitta.


Anasema suala la ukatili dhidi ya wanawake ni changamoto kubwa duniani kote Tanzania, ikwemo. Utafiti pamoja na makala mbalimbali zinaelezea jinsi ukatili dhidi ya wanawake ulivyokithiri.


?Takwimu zinaonyesha kuwa mwanamke mmoja kati ya watatu anafanyiwa vitendo vya ukatili vinavyomwathiri kiuchumi, kisaikolojia na hata kimaumbile kwa kupigwa, kubakwa, au kufanyiwa ukatili mwingine katika maisha yake ikiwa ni pamoja na kuonewa kwa kunyimwa haki zake,? anasema sitta.


Anasema kuwa licha ya vitendo vya kikatili kufanywa dhidi ya wanawake na wanaume, wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto.


Anasema katika kutambua hilo, Serikali imefanya juhudi mbalimbali za kupinga ukatili huo ikiwa ni pamoja na kutia saini mkataba wa CEDAW, na kuridhia Azimio la Nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika kuhusu Jinsia na Maendeleo (SADC), na kuridhia Mkataba Kuhusu Haki za Watoto.


Sitta anasema pamoja na jitihada mbalimbali za kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, bado kuna changamoto nyingi zikiwemo mila na desturi zenye kuleta madhara kuenziwa katika jamii nyingi na imani za kishirikina na mfumo dume.


Anasema kuna sheria nyingi ambazo zinalinda haki za wanawake na watoto lakini hazieleweki katika jamii, pamoja na kukosekana kwa takwimu za matukio ya ukatili zilizochambuliwa kijinsia.


Changamoto nyingine ni pamoja na kumomonyoka kwa maadili kwa baadhi ya wananchi, ukimya wa kutotolewa kwa taarifa za walioathirika dhidi ya ukatili huo, kuendelezwa kwa sheria za kimila hasa katika masuala ya urithi na umilikishaji wa mali, usafirishaji na unyonyaji wa nguvu kazi ya wanawake na watoto na hata kuwaingiza katika biashara ya ngono.


Katika uzinduzi huo, baadhi ya wanawake waliotoa ushuhuda wa wao wa kudhalilishwa na waume zao. Miongoni mwao ni Asha Hassan Maguo (34) ambaye aliolewa mwaka 2001 na kupata mtoto mmoja ambaye sasa ana umri wa miaka mitano.


?Kisa changu ndugu zangu, mume huyu aliyenioa alinipa kipigo cha nguvu na kunipiga ngumi zisizohesabika sehemu zote za mwili wangu likiwemo jicho langu ambalo baada ya kipigo hicho lilipasuka na kutoa maji mengi.?


?Nilikwenda polisi na hospitali jicho langu likatolewa nikawa chongo mpaka hivi mnaponiona. Mume huyu ambaye ni mwalimu akanitelekeza na mtoto wangu mdogo na nimekwisha fanyiwa operesheni zaidi ya mara tatu lakini jicho langu bado linaendelea kunisumbua na bado linahitaji matibabu.?


Asha anasema kuwa mapambano ya kutokomeza unyanyasaji wa wanawake ni lazima yapigwe vita kwani unyama.


Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya anasema kuwa kampeni ya kukataa ukatili dhidi ya wanawake itafanikiwa endapo wananchi watakataa mila mbaya zinazoendeleza na Serikali kuchukua hatua za kubadilisha sheria zinazoendeleza ukatili dhidi yao.


Nkya anasema baadhi ya vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa wanawake vinatimizwa kwa kisingizio cha kuheshimu mila.


Anasema kushamiri kwa vitendo hivyo kunatokana na kuwepo kwa sheria zilizopitwa na wakati akitolea mfano wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, ambayo inaruhusu mtoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18 kuolewa.
 
vitendo hivi vya unanyanyasaji wa watoto na kina mama vimeshamiri sana ingawaje wengi wanaficha na vinaishia majumbani/vyumbani!
je sheria hizi kwa nini hadi sasa hazijabadilishwa ?
 
Back
Top Bottom