Tume ya Warioba isije ikawa kama Tume ya Warioba

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
Makala
jenerali.jpg


Rai ya Jenerali

Tume ya Warioba isije ikawa kama Tume ya Warioba










Jenerali Ulimwengu

Toleo la 237
2 May 2012
















KATIKA makala ya wiki jana, pamoja na mambo mengine, nilitoa pole kwa tume ya Jaji Warioba iliyopewa majukumu mazito yanayohusiana na ukusanyaji na uratibu wa maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya. Nilisema kwamba ningeieleza hiyo pole yangu. Napenda kuirejea.
‘Pole’ yangu kwa Warioba na tume yake inatokana na ukweli wa mambo ninayoyaona na ninayoyakumbuka, ambayo nina uhakika kwamba na watu wengine pia wanayaona na wanayakumbuka. La kwanza ni kwamba, pamoja na kwamba sipendi kuwapamba wanasiasa, Joseph Sinde Warioba, pasi na shaka, ni Mtanzania wa kipekee, mtu makini wa aina yake, muadilifu na mkweli. Ni mtu ambaye kila utawala ulioingia madarakani tangu tupate Uhuru umeona umuhimu wa kumtumia katika nafasi mbalimbali.
Amekuwa Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Sheria na Waziri Mkuu, tukiacha nafasi nyingine alizokuwa nazo nchini na nje ya nchi. Anaheshimika sana kote duniani kwa kazi zake, lakini, muhimu zaidi, ni kwamba anaheshimika nchini mwake kwa sababu anaonekana kama kisiwa cha uadilifu katika jangwa lililokaukiwa na uadilifu, kipande cha almasi katikati ya vipande vya mbao vilivyojaza utawala wetu.
Hivi sasa amekuwa ni “mzee wa kijiji”, ambaye mara kwa mara anajitokeza kutoa matamko ya kuonya, kuasa, kutanabahisha na kukemea inapobidi kufanya hivyo. Anasikilizwa kwa sababu anaaminika. Ndiyo maana haishangazi kwamba, mkabala na madai ya Katiba mpya, Rais Jakaya Kikwete alimwona kwamba yeye ndiye mtu anayeweza kujenga imani miongoni mwa wananchi kwamba zoezi hili litafanyika kwa umakini na matarajio ya wengi yatapata kukidhiwa kwa sababu anayelisimamia ni mtu makini.
Wajumbe wengine wa tume hiyo, angalau wachache miongoni mwao ninaowajua binafsi, wanazo sifa za kutosha za kuwawezesha kulitumikia taifa hili katika shughuli kubwa inayokusudiwa kuleta manufaa kwa nchi yetu. Kwa hiyo ninayoyasema hapa, leo na katika siku zijazo, hayahusiani hata chembe na sifa za wajumbe wa tume hiyo, mmoja mmoja au kwa ujumla wao, bali ninachojaribu kufanya ni kutafakari hali halisi ambamo tume hiyo itafanya kazi yake.
Kwanza tukumbushane kwamba hii si tume ya kwanza kuitwa Tume ya Warioba. Angalau binafsi naikumbuka nyingine, ambayo iliundwa na Rais Benjamin Mkapa mwaka 1996 ambayo Rais aliikabidhi jukumu zito la kuchunguza kwa undani janga la rushwa nchini. Hiyo pia iliitwa Tume ya Warioba, na ilifanya kazi kubwa na nzuri ya kuainisha mapana na marefu ya saratani ya rushwa iliyokuwa inaitafuna nchi, na mwisho wake ikatoa mapendekezo kwa Rais aliyeiteua.
Taarifa ya Tume ya Warioba I ilipowekwa hadharani kwa muhtasari tu, hamasa ilikuwa kubwa nchini kote, nami nilihamasika kiasi cha kupanda ndege kwenda Mtwara ambako kulikuwa na maandamano makubwa yaliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa, Nsa Kaisi kumpongeza Rais Mkapa kwa ubora wa taarifa ya Tume ya Warioba I. Wananchi wakaamini kwamba sasa saratani ya rushwa, ufisadi na uozo ilikuwa imepatiwa dawa mujarrab. Iliyobaki, kama wasemavyo wenzetu, ni historia.
Taarifa ya Tume ya Warioba I hadi sasa inanukuliwa na wasomi katika mataifa mbalimbali duniani na serikali kadhaa zimeifanyia kazi, lakini si Serikali ya Tanzania. Taarifa imeachwa inakusanya vumbi makabatini wakati wakuu serikalini wakiendeleza ufisadi wa kuchefua, hususan katika taratibu za ununuzi (procurement), ambao ndio msingi mkuu wa taarifa hiyo. Hivi majuzi tumeshuhudia tena, bungeni Dodoma jinsi ambavyo ununuzi unafanyika, na kandarasi zinatolewa kama vile hatujawahi kuwa na kitu kama Tume ya Warioba wala taarifa yake.
Majumuisho ya uzoefu tunaoupata kutokana na Tume ya Warioba I ni kwamba ilikuwa ni kazi bure, halafu kazi bure ghali. Tuliingia gharama kubwa, tukawahangaisha watu waliojitokeza kutoa ushuhuda, maoni na mapendekezo, lakini mwisho wake ni makaratasi makabatini, utekelezaji sufuri. Leo najiuliza, hivi mle ndani ya Baraza la Mawaziri kuna mtu anaikumbuka Tume ya Warioba I?
Sasa, wasiwasi wangu ni kwamba, kama vile watawala walivyotaka kumtumia Warioba kujenga imani mwaka 1996 – ili Mr Clean aonekane Mr Clean kweli -- wanataka kufanya vivyo hivyo safari hii tena, kwa kuukamua uadilifu wa Warioba kwa maslahi yao, huku wakijua kwamba kitakachofanywa na tume hiyo hakitakuwa na uwezo wa kubadilisha jambo lolote la msingi. Itagongagonga debe huku na huku, itaondoa aya na kuingiza aya, itafanya mapendekezo ya kiutawala, lakini haitaweza kuweka misingi ya mabadiliko ya kimaendeleo katika muda iliyopewa.
Hofu yangu ni kwamba kwa mara nyingine tena tunaingia katika ubadhirifu wa mapesa chungu nzima kufanya kazi isiyokuwa na tija ya msingi. Mwisho wa siku tutakuwa tumeshuhudia hekaheka na mshikemshike wa mikutano, semina, makongamano, warsha, malumbano, majibizano na mapandishiano, lakini kitakochotoka hatimaye kitakuwa kiduchu. Walatini wa kale walisema, parituriunt montes, nacsetur ridiculus mus. Milima ina uchungu, kitazaliwa kijipanya kiduchu.
Nasema haya kutokana na ushahidi ninaouona, kwamba, pamoja na umuhimu wa kuwa na Katiba mpya, hatuna budi kwanza kupata mwafaka kuhusu masuala ya msingi kabisa, ambayo ni ya kisiasa kuliko jambo jingine lolote. Hatuna budi kuwa na mwafaka wa kisiasa, ambao kwa hivi sasa siuoni.
Nitoe mfano. Kuandika Katiba mpya (kama kweli ndicho tunachotaka kufanya, na si kutia viraka vipya juu ya viraka vya awali) ni sawa sawa na kujenga nyumba mpya (tofauti na kurekebisha au kukarabati nyumba iliyopo). Hii ina maana ya kuanza upya, kukidhi mahitaji mapya na kuangalia pia mahitaji ya ki-mustakabali.
Wanandoa vijana wanaoishi katika nyumba ya chumba kimoja na sebule watataka kuhamia nyumba yenye nafasi kubwa zaidi wanapoanza kupata watoto wawili, watatu, na watajadiliana pamoja aina ya nyumba wanayoitaka kabla ya kumuita msanifu majengo (architect). Watakubaliana juu ya ukubwa wa nyumba hiyo kutokana na watoto wanaokusudia kuwa nao.
Pia watakubaliana juu ya kuweka nafasi ya kutosha kwa watoto kucheza bila kuhatarisha maisha yao, na kadhalika. Nyumba hiyo itabuniwa kwa msingi wa watoto na mahitaji yao. Kama wamekwisha kupata mtoto mwenye ulemavu wa aina fulani, watakubaliana jinsi nyumba yao itakavyomsitiri.
Iwapo wanatarajia kuishi na mmoja au zaidi ya wazazi wao waliozeeka, watakubaliana ni wapi wazee hao wataishi, na jinsi maslahi ya wakongwe hao hayatavuruga maslahi ya wanandoa hao vijana kwa maana ya faragha yao na ukaribu wa kimapenzi. Mzazi aliyetoka shamba anaweza kuwa na tatizo la “kwenda haja” ndani ya nyumba, kwa hiyo hili litawekewa utaratibu ili choo chake kiwe nje kidogo ya nyumba.
Kama wanandoa wamedhamiria kuishi maisha ya ‘Kiswahili,’ wataamua kwamba nyumba yao lazima iwe na uwa, mahali pa akina mama kufanya shughuli zao za upishi, ususi, ufumaji wa vitambaa, na michapo. Watakubaliana juu ya utaratibu usioruhusu baba na binti zake kukutana wakiwa hawajajiweka ‘sawa’. Hii yote ni kusema kwamba nyumba inajengwa vichwani mwa wanandoa kwa maridhiano yao wawili (wakati mwingine na watoto pia, kama wamekua kiasi cha kutosha), kabla ya msanifu kuitwa na kupewa maagizo ya kuwachorea nyumba itakayokidhi mahitaji mahsusi ya familia yao.
Katiba haina tofauti kubwa na nyumba ya familia. Humo ndimo tunataraji kuishi kama taifa, pamoja na watoto wetu wenye mahitaji yanayotofautiana (jinsia, rika, ulemavu); pamoja na wazazi wetu wakongwe (faragha yetu na yao, maliwato waliyoyazoea wakiwa shamba), na kadhalika. Tungekuwa tunatafuta hoteli, tungeweza kupata hoteli yoyote, kwani hoteli moja ni kama nyingine; zinatofautiana ufahari na bei. Nyumba ya familia ni mahsusi kwa familia, mahsusi kwa mahitaji ya familia husika.
Napenda kurejea kile nilichokisema mara kadhaa. Yapo mambo yanayowasumbua wanasiasa, ndani ya chama tawala na ndani ya vyama vya upinzani. Haya ni yale ya kiutawala niliyoyataja hapo juu: tume huru ya uchaguzi; utaratibu wa uchaguzi; viwango vya asilimia katika uchaguzi; utaratibu wa uchaguzi; madaraka ya Rais; madaraka ya Bunge; kuwapo kwa waziri mkuu au la, na madaraka yake; uwakilishi wa uwiano (PR); ukomo wa mihula ya uongozi, na mambo mengine madogo madogo kama hayo.
Haya yote ni muhimu lakini hayana uzito kama ule ninaouona katika maeneo mengine: Kuwapo kwa Muungano na mgawanyo wa mamlaka na rasilimali baina ya Tanganyika na Zanzibar; mamlaka juu ya rasilimali za nchi kwa ujumla (ardhi, madini, maji, misitu); ugatuzi na mamlaka ya serikali za mitaa na mgawanyo wa madaraka baina ya serikali hizi na serikali kuu; mgawanyo wa rasilimali baina ya wakulima na wafugaji; utamaduni na lugha za asili mkabala na Kiswahili na Kiingereza; mfumo wa elimu utakaojenga Utanzania, na kadhalika.
Baadhi ya masuala haya mazito nilikwisha kuyatolea tafakuri, lakini sijachoka kuyarejea. Nitayajadili upya kadri tunavyokwenda.
Narudia kusema kwamba tusifanye mambo kwa haraka kwani hatuna tunakoenda. Tupo hapa, na tunataraji kuwa hapa kwa miaka milioni ijayo, kama si zaidi. Kwa nini tunafanya mambo kama vile tuko mapitoni (transit) tukienda mahali pengine?








[h=2]Soma zaidi kuhusu:[/h]Katiba
Warioba





[h=2]Tufuatilie mtandaoni:[/h]
 
Ndio lile swala langu la "ya". Unapoibinafisha nafasi ya uongozi kwa jina la mtu inakuwa tatizo. Serikali ya time ya - ni matatizo ya kiutendaji, umiliki, hata kuwajibisha
 
Hata mchele uwe mzuri vipi, kama wapishi wabovu, yatoka madida tu! Na wapishi wa fikra pevu za watutakiao mema kama Warioba, ni sisi wenyewe! Sasa tunategemea nini, kama tumeamini katika uwakilishi wa mtu mmoja, kwa majukumu ya watu?
Tume imependekeza mema, mtumishi wetu amekiuka kutekeleza, nani wa kuyatekeleza kama sio sisi wenye? Tunayaacha tu na kulaumu. Fikra mbovu kufikiri ni wale wanaojiita wanaharakati ndio wa kutekeleza, baada ya ukiukaji wa wawakilishi wetu. Kwani harakati ni nini? Kwani wewe na mimi sio wanaharakati? Mpishi mzuri wa mchele mzuri ni mimi na wewe tu!
Tutapata katiba mpya, inaweza kuwa nzuri, lakini kama mimi na wewe hatutokuwa wasimamizi na watekelezaji wa hayo mema ya katiba, basi ni upuuzi. Ni heri kumwambia mzee wetu asiumize kichwa juu ya kutuzawadia yaliyo mema, atuache tu, kwakuwa tumezoea kushabikia mpira wa nje, asitake kutupotezea muda!
Mimi najua kwa sababu naamini, "DEMOKRASIA SIO MFUMO SAHIHI KWA NCHI ZA KIAFRIKA, KWA MAENDELEO YA KWELI" Hatutotoka milele kama tutaendelea kung'ang'ania. Tukae chini tuumize vichwa, tubuni kimantiki, mfumo upi wa uongozi utakubalika kulingana na Nyakati na Mazingira yetu! Na sio lazima uwe umeshawai kutumika mahali fulani, hapana, unaweza kuanzia kwetu! Ni upuuzi kujifananisha na magharibi, ambao hata kikongwe wa miaka 90 anajua kuichambua siasa ya nchi yake. Njoo umuulize mtu wa miaka 40 kwetu uone majibu yake!
Mungu wetu anaita!
 
Back
Top Bottom