Tulipoacha kulijenga Taifa ndipo.. (Hoja)

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
NI mambo gani yametufanya tufikie mahali tunakoromeana na mafisadi na kupigana vijembe na wezi?


Ni nini kimetupata Watanzania hadi tujikute tunakasirikia 'vijisenti' na kudharau vibangusilo?

Sijui kama mwenzangu umewahi kujiuliza nchi yetu ya Tanzania ilipotea njia wapi hadi wajanja wakaiteka nyara mchana kweupe?

Kama kuna mahali tulipotea na kuchukua njia isiyo sahihi, ni wapi hapo ili tukumbushane ili tuweze kurudia njia sahihi? Kuibuka kwa madai ya ufisadi ambayo matokeo yake ni kujiuzulu kwa mawaziri wanne pamoja na kufukuzwa kazi kwa Gavana wa Benki Kuu ni ishara wazi kuwa kuna mahali sisi kama taifa tulienda kombo.

Mahali ambapo tulipotea njia. Ni ishara kuwa kuna kitu ambacho hatukukifanya sawasawa kiasi kwamba leo hii tunavuna matunda yake.

Wizi wa mabilioni ya shilingi katika maeneo mbalimbali ya serikali yetu na matukio yote ya mambo ya mikataba ambayo tunaweza kuikariri kama ngonjera hayakutokea hewani na si njama toka kuzimu. Kwa haya yanayotukuta leo hii hatuwezi kumlaumu shetani na majeshi yake kwani hata yeye anaweza kutuambia “mnanionea”.

Na shetani akilia “mnanionea” basi ujue kweli tumeharibu!Baada ya kutafakari kwa kina nimetambua jambo moja ambalo naamini ni kiini cha matatizo yetu mengi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ndugu zangu, pale tulipoacha kulijenga taifa, hapo ndipo tulipoanza kulibomoa.

Tulipoona kuwa hakuna umuhimu tena wa kujenga misingi ya taifa letu na kuiimarisha , tukavunja vunja kwa makusudi ile iliyokuwapo na tukatupilia mbali na ramani za ujenzi wa taifa hilo ndipo hapo tulipoanza taratibu kulibomoa taifa letu.

Lakini kulibomoa huko kunaonekana zaidi katika athari zake lakini si katika vitendo vilivyo dhahiri.

Kama watoto wachezao “kula mbakishie baba” ndivyo na sisi kila mtu akawa anakula upande wake; wengine kwa pupa zaidi lakini wengine kwa pole pole, lakini kila mtu kivyake tulianza kulitafuna taifa. Tulianza kulibomoa.

Na wale waliopiga kelele “msilibomoe taifa” na wao tukawakaribisha mezani. Tulichokifanya kwa miaka hii ya ufisadi ni kulibomoa taifa badala ya kulijenga.

Mfano mzuri ni wa mtu aliyeamua kujenga jumba lake la kisasa; akatumia gharama kubwa kuchora ramani, akapata kiwanja kwenye eneo zuri na lenye mandhari nzuri kabisa. Akakodi mafundi walio bora kabisa na wengine akaita kutoka nje. Msingi ukachimbwa na zege likamwagwa.Na pole pole kingo za kuta za jumba hilo zikaanza kupanda taratibu.

Ndani wakaanza kugawa vyumba na nafasi mbalimbali kwa mujibu wa ile ramani. Waliopita pembeni wakaona na ingawa hawakuwa na ramani, lakini waliweza kuona kuwa hilo jumba linalojengwa hapo si dogo ni bab kubwa. Walio na ujasiri wakawauliza mafundi ambao waliowaonesha ramani na picha ya nyumba ikikamilika.

Watu wakapigwa na mshangao. Lakini kama vile maajabu kuta zilipofikia maeneo ya madirisha na vyumba kuanza kuonekana wazi; mwenye nyumba akawaambia waanze kupiga lipu na kuweka sakafu ya marumaru; akaanza kuagiza mazulia kutoka Uchina na samani kutoka Uhispania. Akawaambia mafundi “inatosha ujenzi; nimeshajua chumba changu kitakuwa wapi, na cha watoto kitakuwa wapi; ninajua jiko na sebule, veranda na msalani, inatosha”. Mafundi wakaambiwa waache mambo ya ujenzi waanze kusaidia kuipamba hiyo nyumba.

Makochi yakaletwa, ma TV makubwa makubwa (kumbuka nyumba haina umeme inategemea jenereta! meza nzuri na madirisha mazuri yakaning’inizwa kwenye nyumba hiyo ambayo iliwekwa paa la nyasi.

Wapita njia wakaanza kumcheka mwenye nyumba; lakini wajanja wakajitokeza na kuomba kazi ya kuipamba nyumba. Wakaajiriwa watunza bustani, wakaajiriwa wapishi na watunza bustani wakawaambia ndugu zao “njooni kuna ulaji hapa”. Mabinamu, mashangazi, wajomba na wakaza wajomba wakajipanga foleni kupata kazi katika nyumba isiyo malizika.

Jamaa mwenye nyumba ni tajiri hakujali fedha kwani alikuwa nazo. Akaajiri kila aina ya watu kuanza kuitumikia hiyo nyumba na kusafisha vitu vyenye vumbi; Akaishi kwa furaha kwenye jumba lake la thamani linalovuja na ambalo halijamalizika.

Tatizo likatokea mvua za masika zilipoanza. Tajiri wetu hakuwa amemaliza nyumba kuweza kuzuia upepo na maji; mvua ikaipiga nyumba ile, maji yakafurika, choo kikafurika; vitu vyote vya thamani vikaaribiwa na maji na kitanda chake cha thamani kikasombwa. Mara baada ya mvua kupita na jua kuanza kutoka na maji kukauka tajiri wetu badala ya kuamua kumalizia nyumba akaajiri watu kuja kumpa ushauri wa kusafisha jumba lake lililochafuliwa kwa maji na matope. Akaomba na wataalamu kutoka Sweden kwani walioko alidai “hawajui kusoma ramani”.

Wataalamu wote kwa sababu wanazozijua wao waka mwambia anahitaji mapambo bora zaidi kwani yale ya zamani yameharibiwa kwa sababu ni duni. Basi akaagiza na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ambao wote walikuja na lengo moja tu kufanya magofu yake yapendeze na yeye aweze kujivunia uzuri wa magofu hayo huku wakidai malipu makubwa kwa “ushauri wao” huo.

Jambo pekee ambalo hakuwa tayari kulifanya ni kujenga nyumba yake ikamalizika. Hakutaka kumalizia ujenzi wa jengo hilo na hasa angalau kuweka paa zuri na madirisha!

Hivyo ndivyo tulivyoifanyia nchi yetu. Tulipopata uhuru na hatimaye kuungana tulitaka kujenga taifa.

Tulitengeneza ramani ya taifa letu na tukaonyeshana na wenyewe tukaipenda. Tukasema tunataka kujenga taifa la “watu walio huru na sawa”; tukasema tunataka kujenga taifa ambalo “kila mtu ana haki ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”.

Hivyo ndivyo tulivyotaka. Hiyo ndiyo ilikuwa njozi yetu.

Baba wa Taifa katika ujumbe wake kwa TANU siku chache kabla ya Uhuru wa Tanganyika, aliwaandikia wananchi kwenye gazeti la 'Uhuru' na kusema hivi kuhusu huo ujenzi wa nyumba: (tafsiri kutoka Kiingereza ya kwangu).

“Nina uhakika kuwa kila mmoja wetu atasherehekea Siku ya Uhuru kwa furaha kubwa. Tunasherehekea ushindi. Hata hivyo, tunachopaswa kukumbuka ni kuwa tulichoshinda ni haki yetu ya kufanya kazi kwa ajili yetu sisi wenyewe, hari ya kubuni na kujenga hatima yetu wenyewe.

Ni sawa na kupata ardhi ya kujenga nyumba. Kupata kiwanja cha kujenga baada ya kupingwa sana, ni ushindi na inastahili kusherehekea, lakini nyumba haitokei ghafla tu wakati wa sherehe; bali inataka kufanya kazi zaidi tena kwa ujuzi, jasho, na uvumilivu. Ni hivi vitatufanya tuone fahari sisi wamiliki wake”. Akaendelea kusema:

“Tumekuwa tukizungumza kwa muda mrefu ni nyumba gani tunataka kuijenga kwenye ardhi hii. Sasa tunayo nafasi ya kufanya hivyo.” Hayo ni maneno ya hekima. Lakini tunachokiona leo hii ndugu zangu ni kuwa tumeacha kulijenga taifa na badala yake tumeanza kulibomoa. Tumekuwa tukifanya jitihada ya kuendeleza vitu ili kuipamba nyumba tusiyoimalizia.

Tunafurahia kujenga majengo marefu ya vioo vioo huku mitaro wa kupitishia maji machafu hapo chini haipo au imeziba wangu 'mwaka 47! Tunajitahidi kujenga mahoteli makubwa kwa ajili ya watalii na wageni wanaokuja kututembelea kwenye nyumba yetu lakini mtaa wa pili kama pale Uwanja wa Fisi kuko duni!

Juzi nimeona picha kwa ndugu yangu Mpoki kutuonyesha mwanafunzi akijisadia porini huko Kasulu kwa sababu shule haina choo! Wenyewe tunafurahia kuweka samani kutoka Uchina! Tumeacha kulijenga taifa.

Tumeacha kufanya mambo ya msingi ambayo ni muhimu kwa taifa lolote na leo tunajikuta kwenye matatizo kadhaa. Tulipopata nafasi ya kuandika sheria ya maadili tulifanya nini?

Tuliandika mojawapo ya sheria za vituko kabisa nchini mwetu. Sheria inayotoa haki ya kuangalia mali za viongozi lakini kutozitangaza! Sasa kama hamtaki watu wajue kwanini kuruhusu.

Hivi watanzania wote milioni karibu 40 wajipange msururu kwenye kwenye tume ili waone mali za viongozi wao? Si ndiyo maana tuna vyombo vya habari ambavyo vinatumika kutoa habari kwa watu wengi?

Tulipoacha kulijenga taifa, ndipo tulipolibomoa.Tukaandika sheria ya Usalama wa Taifa ya 1996 ambayo nayo ni kituko. Ni sheria gani inayowafanya Usalama wa Taifa wawe ni watoa ushauri tu na kukusanya habari lakini wanakatazwa kusimamia usalama? Ni nani huyo aliyesimamia sheria hiyo (Chenge???) ambayo haiwezi hata kulinda usalama wa vifaranga vya kuku? Je, yawezekana sheria hiyo iliandikwa ili kuuminya usalama wa taifa wakati wajanja wakapoanza kuchota toka Benki Kuu na taasisi nyingine?

Je, ilikuwa na lengo la kuweka vikwavyo vya 'kisheria' kwa Usalama wa Taifa kufanya kazi zao? Tuliacha kulijenga taifa.

Tukaacha kuweka kipaumbele kwenye mambo ya msingi kweli na badala yake tukajiingiza kichwa kichwa kwenye madini huku sheria nyingine mbovu ya madini ya 1998 nayo ikatengenezwa kama vile na nchi ya vichaa!

Baadaye watu wanaanza kukomba madini yetu na rasilimali zetu tunashtuka na kujiuliza kulikoni. Tunataka thamani lakini hatutaki kutengeneza paa! Tuliacha kulijenga taifa.

Kwa sababu tunazozijua sisi (wao ) tukaanzisha Bodi ya Mikopo kwa sheria nyingine mbovu ambayo ikachochea ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma. Leo tunajikuta na matatizo pale chuo kikuu tunashangaa imekuwaje?

Tunatilia umuhimu kuwa na wahitimu wengi lakini tumesahau kutoa wasomi! Tumeamua kuchanganya mtu kupata shahada na mtu kupata elimu. Matokeo yake baadhi ya wale waliohitimu na ambao hawakuelimika licha ya kufaulu mitihani wamepewa nafasi ya kusimamia uletaji wa samani na mazuria ya nyumba inayovuja!

Hawaulizi mbona nyumba inavuja wanasema “sisi ni watumishi tu!" Tunashangaa mbona wanaleta mambo ya Richmond na wadogo zake na watu wana shahada za Uzamili na za Kuzamia katika ufisadi? Watanzania!! Tuliacha kulijenga taifa.

Leo hii tunashangaa tunapoona mawaziri wanaporomoka kama makuti makavu. Tumeamua kuwaita mafisadi lakini hatutaki kuangalia ni wapi tulipowafungulia mafisadi waingie ndani na kuchota fedha zetu kwa upole kama kumchomolea mlevi!

Kwanini wasiingie wakati hata milango tumeacha kuweka kwenye nyumba yetu? Leo hii Saidi Mwema na timu yake wameshindwa kupokea changamoto yangu ya kuanzisha mfuko wa “Donge Nono” la kushawishi watu watoe habari kuhusu mauaji ya maalbino.

Na siku hizi chache habari za maalbino kuuawa na wengine kujisalimisha kwa wakuu wa polisi zinaendelea kutokea. Tunasubiri wauawe wengine halafu mwisho wa mwezi Rais atoe wito kwa watu ‘kuacha ushirikina’.

Ndugu zangu tulipoacha kulijenga taifa ndipo tulipoanza kulibomoa. Hata kama hawataki kamchango kangu kadogo, basi niko tayari kushirikiana na Chama cha Maalbino kuanzisha mfuko huo.

Wako wapi wale watetezi wa haki za binadamu? Wale waliosimama kifua mbele kupinga ziara ya Rais Bush na kutoa matamko yao kulaani jinsi Marekani inavyovunja haki za watu wa Iraq na Palestina?

Walioandamana kwa jazba na mabango na kuchoma bendera ya Marekani kuonyesha kuwa wao ni watetezi wa haki za binadamu? Mbona hawajaandamana kuwatetea watoto wetu na ndugu zetu maalbino.

Au hadi wawe maalbino wa Kiiraq? Watatoa matamko watakaposikia kuwa ni Wamarekani ndio wanafanya mauaji ya Albino ndio watakuwa na uchungu? Ndugu zangu, tuliacha kulijenga taifa.Tusiogope kuangalia tulikotoka kwa kuogopa kuonekana mashabiki wa Nyerere au watetezi wa ujamaa na mapinduzi.

Leo hii taasisi ya mwasisi wa taifa letu inaenda kwa kusua sua na kuomba omba ufadhili huku wanaosema “wanamuenzi Nyerere” wakienda Butiama na kutumia mamilioni ya shilingi kwa shughuli hizo na kuacha taasisi aliyoianzisha Nyerere mwenyewe ikifanya “umatonya”. Inaweza kumshangaza yule malaika wa kifo kuwa viongozi ambao wanadai wanapenda kumuenzi Nyerere, wameshindwa kuiunda taasisi hiyo kwa mujibu wa Bunge na kuiwekea bajeti na kuifanya iwe na fedha yote inayohitaji kujisimika kama chombo muhimu cha kudumu na inayojitegemea cha kumbukumbu ya historia yetu na pia cha kutukumbusha ramani ya taifa letu.

Ndugu zangu, ni dalili ya wapi tulipopotea. Hatuwezi kuendelea kuleta samani na mapambo kutoka ng’ambo katika nyumba isiyokwisha.

Hatuwezi kuendelea kuimba sifa za nyumba nzuri na ya kuwa “maisha bora kwa kile mgeni yanawezekana” kwenye jumba bovu. Ndio, tunajitahidi kupaka rangi; ndiyo, tunajitahidi kuweka majenereta yenye nguvu zaidi; ndiyo, tunajitahidi kukaribisha wageni waje waione nyumba yetu na kuisifia.

Lakini kitu kimoja ambacho hatuko tayari kukifanya ni kujenga jumba letu tunavyotaka. Tunahitaji maamuzi ya makusudi na ya dhati. Maamuzi ya kutuambia kuwa huku tuliko siko tulikotaka kwenda.

Hapa tulipofikia sipo tulipotaka kufika. Turudi tulipopotea. Turudi kwenye nadharia nzima ya kulijenga taifa. Rafiki yangu mmoja daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama kwenye hospitali moja jijini alimsaidia mhandisi mmoja hivi wakati mke wake amepata matatizo wakati wa kujifungua. Rafiki yangu alijitahidi kwa kila alichoweza hadi kuhakikisha mama na mtoto wako salama baadaya ya kulazimika kufanya upasuaji.

Yule Mhandisi alishangazwa na jinsi daktari huyo alivyokuwa anafuatilia suala la mke wake na muda na yote aliyoyafanya kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa mazuri. Mhandisi huyo (ambaye ni raia wa Marekani) alishangazwa na kujituma kwa daktari huyo kijana.

Hata hivyo, rafiki yangu anasema hakufanya kitu chochote ambacho hakikuwa cha kawaida. Anadai alichofanya kingeweza kufanywa na daktari yeyote Tanzania au nje. Ilikuwa ni sehemu ya kazi yake.

Yule mhandisi akaanzisha urafiki na rafiki yangu na baada ya muda akamtembelea kuona mahali rafiki yangu ameanza kujenga nje kidogo ya Jiji la Dar.

Yule mhandisi aliona ujenzi ulivyokuwa unafanyika kwa kutumia mafundi wa “uswahilini” tu ili kukwepa gharama na akaona matatizo mengi sana katika ufundi mzima. Akaamua kumuomba rafiki yangu ruhusa ya kutoa maoni juu ya hicho “kibanda chake”.

Alipomaliza rafiki yangu alijikuta anatikisa kichwa na kuchanganyikiwa. Yule mhandisi akamuambia amruhusu aonyeshe shukrani yake kwa kumchorea jengo jipya na kusimamia ujenzi yeye na kampuni yake bure kabisa kama shukrani ya wema aliotendewa.

Rafiki yangu hakuamini lakini hakuweza kukataa. Siku chache baadaye misingi na kuta za nyumba ile zikafumuliwa na yule mhandisi na timu yake wakaanza moja.

Wiki chache baadaye misingi mipya na sura mpya ya jengo la kisasa likaanza kuinuka taratibu. Wiki chache zilipita, rafiki yangu na mke wake mpya ndio wamehamia katika nyumba yao.

Ndugu zangu, tuna uchaguzi wa kufanya. Tunaweza kuendelea na nyumba inayovuja na yenye paa la nyasi ambayo tayari ina misingi imara au tunaweza kuamua kutengeneza paa na kukamilisha kuta na kuziba nyufa zote. Napendekeza uamuzi huo wa pili kwani huo wa kwanza ni wa nchi ya ufalme wa wajinga.

Tutengeneze paa letu ili litulinde wakati wa hari na wakati wa mvua. Paa hilo ndugu zangu ni katiba yetu. Matatizo yetu mengi sana katika uongozi na utawala yanatokana na madhaifu makubwa katika katiba.

Kuendelea jinsi ilivyo kwa kudai kuwa “haina matatizo” ni sawa na mbuni kuficha kichwa mchangani akidhani haonekani. Hili la Katiba nitaliandika zaidi wiki chache zijazo na kulitolea mifano.

Lakini kwa vyovyote vile tukitaka utawala bora, uwazi na kuwajibika kwa viongozi hakuji kwa maandamano bali kwa kutengeneza paa imara; yaani katiba imara. Iliyopo imetutosha hadi sasa, lakini huko tunakokwenda haifai. Tukishatengeneza paa, tuanze kuziba matundu na mianya yote inayotishia uimara wa nyumba yetu.

Mianya ya sheria mbovu na ambazo zimepitwa na wakati kama sheria ya maadili, sheria ya fedha haramu, sheria ya usalama wa taifa, sheria ya TISS na sheria nyingine za adhabu n.k
Kabla kweli hatujaanza kuvuna matunda ya taifa tulilolijenga hatuna budi kuhakikisha kuwa tunajenga kwanza taifa hilo. Isijekuwa leo hii tunalalamikia mavuno kumbe tunachovuna leo ndio tulichopanda.

Tunajua cha kufanya; tusahihishe tulipokosea na tuache kukwepa kubeba lawama au kukubali wajibu wetu. Tusisubiri vizazi vijavyo vifanye kazi ambayo sisi tungeweza kuifanya leo hii. Kile ambacho tunaweza kukifanya leo kisingoje kesho.

Turudi kwenye ujenzi wa taifa na tuangalie ni vitu gani tufanye kwanza ili kuweka misingi. Vinginevyo, tutaendelea kuweka mapambo na kufurahia kupendeza kwa mandhari ya vitu na siyo hali ya watu.

Tutajikuta kama Kenya ambao baada ya uhuru wao waliamua kuendeleza vitu, tukawaonea wivu hawa kuchukua hatua za kujenga taifa hadi matukio ya hivi karibuni yalipowalazimisha kutambua kuwa la kwanza ni kujenga taifa.

Vivyo hivyo Rwanda, Uganda, na Congo, walipopata Uhuru hawakwenda kwenye kulijenga taifa bali wakaanza kulitumikia. Matokeo yake wakajikuta kwenye matatizo. Sasa hivi wenzetu wametambua umuhimu wa kujenga taifa kwanza na mambo mengine yanafuata. Uganda wameamua kujenga taifa kwa kuzungumzia na kushughulikia yanayowasumbua kama taifa; Wanyarwanda vivyo hivyo baada ya matukio ya 1994 wametambua hawawezi kwenda mbele bila kuangalia walikotoka na walikopotea; na vivyo hivyo Kongo.

Ni sisi ambao tulianza kwa kulijenga taifa lakini mahali fulani tukaamua kuacha tukiamini kuwa “tumefika”. Huko tunakokwenda tutajikuta kwenye matatizo na tutashangaa tumefikaje; jibu nimewapatia ndugu zangu, tulipoacha kulijenga taifa ndipo hapo tulipoanza kulibomoa. Kwanini tusirudi kulijenga tena?
 
Back
Top Bottom