Tujiamini, vinginevyo maendeleo yatakuwa duni

MmasaiHalisi

Senior Member
Jan 15, 2009
192
23
Na Edwin I.M. Mtei


NI jambo la kusikitisha kwamba Tanzania kwa jumla, katika miaka ya hivi karibuni, tumeonyesha dalili za kutojiamini kadiri tunapoongezeka umri kama taifa.
Mara baada ya uhuru, iliwezekana kwa kutumia mkakati wa Africanization, kuwapatia mafunzo murua, (crash training programme) maofisa wa Kitanzania, na kuwapa mapema majukumu ya kuendesha na kuongoza wizara, idara na taasisi nyingi za umma.
Mwanzoni, mara nyingi kulikuwa na Advisors (washauri) kutoka ng’ambo ambao walisaidia kwa muda, lakini wengi waliondoka mapema na kuwaachia wazalendo kuendesha mambo.
Nyingi za hizi, wizara na taasisi za umma ziliendeshwa kwa ufanisi, na kutengeneza faida hata pale washauri walipoondoka.
Kama kulikuwa na udhaifu uliobainika, hatua zilichukuliwa mapema bila kusitasita, ama kwa kurekebisha miundo au kuondoa uongozi na kuwajaribu Watanzania wengine.
Tulipopata tatizo, hatukukata tamaa eti wananchi hawawezi kuongoza kitaalamu.
Hizo zilikuwa enzi za Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) kuendeshwa na kina Amon Nsekella; Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuendeshwa na George Kahama; Shirika la Biashara la Taifa (STC) kuendeshwa na Wena Kapinga akishirikiana na Bakari Mwapachu; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Geoffrey Mmari na baadaye Pius Msekwa; TANESCO ikiendeshwa na Jerry Kasambala na Salvatory Mosha, hata mie nikiendesha Benki Kuu ya Tanzania.
Taasisi nyingi zilizoshirikisha Kenya na Uganda, kama Reli, Posta na Simu, Shirika la Ndege na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, ziliendeshwa na wananchi wa Afrika Mashariki, wa Tanzania wakiwamo, bila wasiwasi.
Na iliwezekana kuwa na faida na kutoa gawio la ziada (dividends on surplus) mara nyingi mwisho wa mwaka. Kama kulitokea hasara, au udhaifu wowote, ilionekana ni jambo la kawaida katika uhai wa shirika lolote duniani na hatua za masahihisho zilichukuliwa.
Sasa inaonekana kuna kasumba iliyoenea miongoni mwa Watanzania kwamba hatuwezi kuendesha lolote. Hatujiamini tena. Hasa viongozi wetu wakuu hawana imani na wasomi wetu, licha ya miaka 45 ya uhuru ambayo imeshuhudia kuongezeka kwa wataalamu wa kikwetu kwa zaidi ya mara mia moja.
Kasumba inachochewa na wadhamini wetu na taasisi za kimataifa zinazotupa mikopo na misaada ya fedha.
Ni jambo ambalo haliingii akilini eti baada ya kuwa na reli ambayo ilijengwa enzi za Wajerumani miaka zaidi ya 100 iliyopita, na kuendeshwa na watu wetu kwa miaka zaidi ya 40, sasa tumeshindwa kuikarabati na kuiendesha.
Eti ni lazima tutafute Wahindi waikodishe na kuiendesha kwa miaka zaidi ya 20!
Wataalamu wetu wamekwenda wapi? Kama ni kukosa fedha kutokana na shirika kuendeshwa kwa hasara, kwa nini tusikope kidogo na kuongezea mchango wetu kwa kutumia hilo ongezeko la mapato ambalo rais wetu alitangaza kuwa limepatikana?
Kwa nini tusiwapeleke mameneja wetu wa Shirika la Reli, wakakaa na viongozi wa mashirika ya reli ya ng’ambo ambayo yanaendeshwa kwa ufanisi?
Ni mbinu gani hawa Wahindi wanaokodishiwa reli watatumia kufanikisha hili shirika, ambayo mameneja wetu hawataweza kujifunza kama wangepelekwa India kwa mafunzo ya kukaa nao (attachment)?
Kutokujiamini kwa Watanzania hakuhusiani na jinsi tunavyoshughulikia Shirika la Reli tu. Katika kila sekta inaonekana tumepoteza imani yetu kwa wataalamu wetu.
Uongozi wetu hauna imani kwamba tuna uwezo wa kujihudumia sisi wenyewe hata katika mambo tuliyo na mazoea nayo kwa miongo mingi.
Tunawapeleka vijana wetu kwa mafunzo ya elimu ya juu katika vyuo vikuu maarufu kama Harvard, Massachusetts Institute of Technology, Berkley California, Oxford na vingine vya Ujerumani, lakini wakirudi baada ya kufuzu hatuwapi majukumu.
Badala yake tunaomba consultants kutoka Marekani, Uingereza n.k kuja kuendesha miradi.
Wengi wa hawa consultants wanakuwa ni vijana ambao walikuwa masomoni pamoja na walewale vijana wetu tuliowagharimia kupelekwa ng’ambo. Huenda hata hawa consultants hawakufaulu vizuri kama hawa vijana wa kwetu. Kwa nini hatuwaamini?
Tumeshuhudia taasisi kama NBC, TANESCO, Shirika la Simu, Air Tanzania n.k. zikiuzwa au kupewa wageni kuendesha.
Wengi wa hawa mameneja wa ‘wawekezaji’ wanavurunda na wanategemea misaada kutoka kwa watu wetu waliokuwa wakiyaendesha mashirika hayo hapo awali.
Mengi ya haya mashirika yanafilisika au kuendeshwa kwa hasara.
Baya zaidi ni kwamba mikataba ya kuuza au kukodisha haya mashirika imeghubikwa na usiri.
Mingi ya hii mikataba inanuka rushwa. Matokeo ya yote haya ni wananchi kutoamini viongozi wao, aidha pia kuongezeka kwa hii kasumba au utamaduni wa Watanzania kutojiamini.
Kutokana na huu mtindo wa kutojiamini, mashirika tuliyokabidhi kwa wageni ama kwa kuuza au kwa mikataba ya kuendesha, uzalishaji wa bidhaa zake au huduma, umekuwa wa gharama za juu sana.
Matokeo ni kuchochea mfumuko wa bei na kuongezeka kwa shida kwa wananchi walaji. Lengo la maisha bora kwa Watanzania haliwezi kufikiwa kwa mtindo huu.
Maoni yangu ni kwamba kiini cha haya yote ni kukosa uzalendo. Hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu ya kuridhisha kama tutadumisha kutojiamini au kukosa imani na wataalamu wetu. Uzalendo wa dhati unampa mwananchi kujiamini na kupenda nchi yake na watu wake. Wanaopewa dhamana ya kutuongoza ni lazima wawe wazalendo wa kweli. Tujiamini; la sivyo maendeleo yatakuwa duni.
 
Back
Top Bottom