Tujenge utamaduni wa kuwajibika kwa wakati

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
KATUNI%28621%29.jpg

Maoni ya katuni


Kwa kipindi kirefu sasa taifa hili limekuwa linaruhusu kuimarika kwa utamaduni wa kutokuwajibika. Hali hii kwa bahati mbaya inaelekea kuchangiwa zaidi na hali ya kuamini kuwa mwenye madaraka hawajibiki kwa aliyeko chini yake.
Kwa takribani wiki mbili sasa kumekuwa na mvutano baina ya madaktari na serikali juu ya maamuzi ya kuwaondoa madaktari wanafunzi (interns) katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambao walikuwa wamegoma wakidai posho zao.
Kufuatia mgomo huo serikali ilitafuta posho zao na kuwalipa, lakini baada ya kulipwa tu wakapewa barua za kuwataka wakaripoti Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; kilichoelezwa kwenye barua hizo ni kwamba walikuwa wamevunja mkataba wa kuwako Muhimbili.


Kutokana na hali hiyo, uliibuka mvutano baina ya Chama cha Madaktari (MAT) na wizara juu ya hatua za kuwaondoa kinyemela madaktari wanafunzi Muhimbili kisha wakapangiwa vituo vingine vya kazi. Wapo waliokubaliwa moja kwa

moja kuanza kazi kwenye vituo vipya, lakini wengine ni kama walitoswa. Wamekutana na kile kinachoitwa njoo kesho, njoo kesho.
Katika kipindi chote hiki, MAT wameingilia kati na kutaka kuwakutanisha madaktari hao na uongozi wa wizara, lakini vimeibuka vikwazo vya kushangaza. Hivi ni pamoja na kila upande kuandaa eneo lake la mkutano hali iliyofanya madaktari kuwasubiri viongozi wa wizara ukumbi wa Don Bosco, huku madakrati wakisubiriwa ukumbi wa Anoutoglo. Kila upande umekuwa unamlaumu mwingine kwa hali hii.
Kimsingi hali hii ikiendelea kilichoathirika ni huduma kwa wagonjwa, ingawa juzi Muhimbili walisema huduma zake zinaendelea kama kawaida na kutaka taarifa za kuzorota kwa huduma zipuuzwe, bado kuna kila chembe ya ukweli kwamba katika mzozo kama huo ni muhali kuibuka na kudai kuwa hakuna madhara yaliyotokea kwa taasisi ambayo imehamisha au kuondoa madaktari zaidi ya 200 kwa mpigo.
Hata hivyo, hali katika Taasisi ya Mifupa (MOI) nako inaelezwa kuwa si nzuri, huduma zimedorora, huduma kwa wagonjwa wa nje zimesimama kabisa, kisa ni madai ya madaktari ambayo sasa yanaungana na yale ya interns. Kuzorota kwa huduma hizi kumejitokeza wakati madaktari kwa siku kadhaa sasa wamekuwa wakihudhuria mikutano yao katika ukumbi wa Don Bosco wakidai pamoja na mambo mengine kusikilizwa kwa interns lakini pia nyongeza ya posho zao za kazi na nyongeza ya mshahara kwa asilimia 30. Wanajenga hoja kuwa mara ya mwisho posho hizo zilirekebishwa mwaka 2004.
Ukifuatilia mivutano yote hii hadi kufikia kuanza kufanyika kwa mlolongo wa mikutano ambayo kwa hakika inaathiri utoaji wa huduma za afya katika hospitali za umma, utagudua kitu kimoja, hiki ni utamaduni wa kuacha kushughulikia madai au malalamiko ya watumishi wa umma kwa wakati. Malalamiko ya aina hii hayako kwa madaktari tu, walimu wamekuwa na malalamiko kama haya kwa miaka mingi kiasi cha kufikia hatua ya kutangaza mgomo.
Kila tunapotafakari hali hii tunajawa na hofu kwamba utaratibu wa kiserikali wa kuendesha mambo umepoteza dira kutoka kanuni na taratibu zilizokubalika hadi kuwa utashi wa kiongozi mmoja mmoja anayeongoza taasisi husika, hususan wizarani.
Ndiyo maana hata pale malalamiko yanapokuwako kwa muda mrefu hakuna hatua za haraka zinazochukuliwa kwa sababu watu hawaheshimu tena taratibu, hakuna majibu yanatolewa na mwisho wa hali hii ni milolongo ya mikutano kama ya madaktari kwa sasa na pengine migomo.
Hali hii inajenga picha ambayo haipendezi, kwamba wale wote walioteuliwa kusimamia taasisi za umma kama vile wizara, hispitali na asasi nyingine zinazojitegemea, wamekuwa hawajali sana kusumbuliwa na kero za wale walioko chini yao, matokeo yake taifa sasa linaelea kwenye malalamiko. Wananchi wanalalamika kila kona kwamba huduma zimezorota katika sehemu nyingi, malalamiko haya ni kielelezo cha kutokuridhika na hali ya mambo ilivyo.
Tunasema ni wajibu wa viongozi wa umma kushughulikia malalamiko na kila aina ya kero za wananchi, kuanzia za wale ambao hawana kibarua chochote serikalini hadi wale walioajiriwa kutoa huduma sehemu mbalimbali; kushindwa au kukataa au kupuuza kuwajibika kwa wakati ni sawa kabisa na kulelea utamaduni wa kutokuwajibika. Ni vema watawala wetu wakaamka na kuepusha nchi hii na mlolongo wa malalamiko na vitisho vya migomo.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom