Tufikirie namna gani tutazuia kuwa na viongozi legelege kama tulio nao sasa kwa siku za mbeleni

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
16,505
41,013
Sifa kubwa ya kiongozi anayeweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii yoyote ile ni kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika kuhakikisha dira, malengo na majukumu anayoamini yanateklezwa, tena kwa kwa namna, kiwango na mbinu anazoziamini. Kwa hiyo kiongozi kwanza ni lazima awe na imani fulani, kutokana na imani hiyo, ashiriki kwenye kuandaa mipango, malengo, majukumu na mbinu za kuifikia imani yake - lakini siyo tu ashiriki bali pia aamini kuwa mipango, malengo, mbinu na mikakati hiyo ndiyo njia sahihi za kutimiza imani yake.

Kuna imani kuwa serikali ni ya wananchi, na kwamba maamuzi yote hufanywa na wananchi kwa hiyo hata Taifa linaposhindwa kufanikisha mipango yake ni kwa sababu ya wananchi wenyewe LAKINI ukweli ni kwamba serikali ni ya kiongozi mkuu na wasaidizi wake wachache sana, na nchi inaposhindwa kutekeleza mipango yake hawa hawana haki hata ya 1% ya kukwepa hukumu ya wananchi kwa kushindwa kutekeleza yale ambayo kwa kiasi kikubwa ni wao walioyabuni.

Viongozi waliowahi kuleta mabadiliko makubwa katika mataifa yao ni wale ambao waliokuwa na uwezo mkubwa katika kujenga imani na fallsafa sahihi za kuyabadilisha mataifa yao, kisha wakaenda kwa watu wao kuwashawishi watu wakubaliane na yale wanayoamini kuwa ndiyo njia sahihi za kuyaondoa mataifa yao katika hali duni; wanaweka mipango na mikakati kisha huipeleka kwa wananchi na kuwashawishi waikubali, na baadaye mipango hiyo hugeuzwa kuwa ndiyo mipango ya wananchi. Baada ya hapo watawala wanakuwa wamepaa mandate ya umma ya kuisimamia bila ya kuonekana kuwa madikteta. Kiongozi kuandaa mipango mbalimbali, halafu ikapelekwa kwa wananchi, nao wakaikataa huwa ni dalili moja kubwa ya kiongozi huyo kutokuwa na uwezo au wananchi kutokuwa na imani naye.

Kwa uchambuzi sahihi, viongozi wa aina ya JK na Pinda, siyo viongozi wa kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka katika jamii, bali ni viongozi ambao wanaweza kufaa katika kuendeleza mfumo uliopo. Viongozi wa kuleta mabadiliko katika jamii, kwa vile hupingana na mfumo ambao umezoeleka ni lazima kwanza wawe wenye mtizamo/dira tofauti na ya mfumo uliopo, wawe na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi magumu na ya kijasiri ya kuuondoa mfumo wa uongozi na usimamizi katika mazoea, wawe na ushawishi mkubwa katika Taifa kiasi cha kila aliyepo katika mamlaka na wananchi wote kuamini kuwa falsafa mpya, mipango na mbinu mpya ndiyo njia sahihi ya kuleta mabadiliko. Lakini pia lililo muhimu zaidi ni jamii kuamini kuwa kiongozi ana uwezo wa kusimamia anachoamini na kutamka. Ukiwatazama hawa viongozi wetu wakuu hawana sifa hizo:

JK
  • Yeye ni kiongozi ambaye hapendi kuonekana ni mbaya kwa mtu yeyote, na kama angekuwa anaweza angependa apendwe na watu wote Duniani. Ni kiongozi ambaye hapendi kumwudhi mtu yeyote, japo kwa kufanya hivyo ameweza kuwaudhi na kuwasikitisha watu wengi zaidi
  • Si kiongozi mwenye msimamo wa wazi kiitikadi na kivitendo. Ni vigumu sana kufahamu kwa undani JK anataka nini. Anataka Tanzania liwe Taifa la namna gani kiuchumi na kiitikadi. Amekuwa ni kiongozi ambaye anaegemea kwenye matamanio badala ya mipango ya mabadiliko
  • Ni kiongozi asiyependa confrontation, na kwa sababu hiyo mara nyingi amekuwa naye akilalamika kama mwananchi wa kawaida. Watu walitegemea kuwa wanapolalamika Rais achukue hatua, lakini naye analalamika huku akiwajua anaowalalamikia. Hata pale alipostahili kuchukua hatua, yeye amekuwa akiongea na wanahabari ili wahalifu wasikie na wananchi wasikie kuwa Rais yupo upande wetu, lakini na kwa ule upande wa wahalifu isionekane amewatendea jambo lolote baya katika uovu wake
  • Mbaya zaidi amependelea kila mara kuwa na wasaidizi wake wa namna hiyo hiyo. Kwenye kundi hilo yumo Pinda, Kawambwa, Ngeleja, Malima, Mwandosya, n.k. Viongozi wale wa kutenda kama Magufuli, wasiopenda siasa za kujipendekeza, si watu ambao wanaonekana kumfurahisha Rais katika utendaji wao
Pinda
  • Huyu kama alivyo boss wake ni kiongozi mwoga
  • Kiongozi mnafiki mwenye nia ya kutaka kuwafurahisha watu wote, kama alivyo boss wake. Ndiyo maana kwaajili ya kutaka kuwafurahisha wananchi aliamua kukataa kutumia gari la kifahari lakini hakuweza kuzuia ununuzi wala matumizi ya magari hayo kwa viongozi wengine, maana hapendi confrontation wala kuwaudhi watu wengine
  • Ni kiongozi wa nadharia - kiongozi wa kusimlia aliyoyaona lakini siyo wa kujifunza kutokana na anayoyaona. Ndiyo maana kila mara kwenye mikutano amekuwa akielezea alivyoona South Korea, India, n.k. jinsi wanavyobana matumizi na kukazania uzalishaji lakini hajawahi kueleza kutokana na hayo aliyoyaona anatoa maagizo gani
  • Ni kiongozi ambaye hana footprints. Haonekane kuwa na dhamira ya kuweka kumbukumbu ya uongozi wake kwa kufanya mambo ambayo kwayo atakumbukwa. Kiongozi mzuri ni yule anayepigania kutenda mambo makubwa ya kimaendeleo ili akumbukwe daima.
  • Naye, kama alivyo boss wake hapendi viongozi wanaosimamia maagizo bila kupindisha. Ni tabia hiyo ndiyo iliyomfanya amzuie Magufuli kuvunja nyumba zilizopo kwenye hifadhi ya barabara kwa sababu tu kuna watu walimlalamikia, naye alitaka kuonesha anawajali
Ndani ya nchi ambayo mfumo wake wa uongozi na usimamizi umevurugika kama Tanzania, tunatakiwa kuwa na viongozi wa kubadilisha mifumo yote ya kiutawala na uongozi, na hasa zaidi katika usimamizi. Na ili hayo yaweze kutendeka tunahitaji viongozi wenye falsafa sahihi na ya dhahiri, viongozi jasiri wanaosimama katika kauli zao mstari kwa mstari, wenye dhamira na walio jasiri katika kufanya maamuzi magumu kwaajili ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kiutawala na kijamii. Viongozi wasio na falsafa sahihi, wasio na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu kwaajili ya manufaa ya Taifa, viongozi ambao matendo yao hayafuati kauli zao, kama hawa tulio nao, ni wa kuwaogopa sana siku za usoni kama tunataka vizazi vijavyo katika Taifa hili viishi katika Taifa lenye ustawi na matumaini. Katika mataifa yote Duniani mabadiliko makubwa ya kiuchumi yalihusiana na mtawala fulani. Ili kuleta mabadiliko huhitaji kundi la watu, ni mtu mmoja tu - Kiongozi Mkuu wa nchi. Mkimpata huyo tu, treni ya maendeleo iliyosimama kwa miaka mingi inaweza kuanza kukimbia kwa mwendo kasi ambao kila mmoja hakuutegemea, maana yeye ndiye anayeamua awatafute wasaidizi wa namna gani. Mara nyingi kiongozi goigoi huchagua wasaidizi goigoi.
 
Back
Top Bottom