Tuendelee kuvumiliana – Balozi Seif

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
[h=1][/h]Posted on February 14, 2012 by zanzibaryetu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akifunga semina ya siku mbili ya kujadili hali ya kisiasa Zanzibar

Lakini hata hivyo, ni vyema pia tukaelewa kuwa hatuwezi kujenga nyumba imara ya jiwe kwa siku moja na tukaishi humo. Utamaduni ule ule wa kustahamiliana utahitajika kufikia hatua nyengine tunayoitaka. Utamaduni tulioutumia wa kuleta mabadiliko bila ya kujali maslahi ya mtu au kikundi fulani bado unahitajika kwani gharama ya kufanya mabadiliko kwa lengo la kutaka mtu au watu, kikundi au vikundi fulani vinufaike ni kubwa inayoweza kuturejesha tunakotoka.
HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI SEIF ALI IDDI, MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR ALIYOITOA KWENYE UFUNGAJI WA MKUTANO WA PILI WA HALI YA SIASA VISIWANI ZANZIBAR, HOTELI YA BWAWANI ZANZIBAR, TAREHE 14 FEBRUARI, 2012
Ndugu Mwenyekiti,
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala,
Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi,
Viongozi wa Serikali,
Wageni Waalikwa
Mabibi na Mabwana
Assalamu Aleykum,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa leo chini ya mwamvuli wa baraka ya hali nzuri ya kisiasa Zanzibar ambayo wengi wetu tunajivunia na tuko tayari kuimarisha ili kuwa bora leo na kesho pia. Kujitokeza kwenu kwa wingi ni ushahidi tosha kuwa kila mmoja wetu anataka kuwa ndani ya mwamvuli huu wa baraka.
Nawashukuru kwa dhati waandaaji wa mkutano huu kwa kunialika kuja kuufunga, na kwa heshima kubwa nawakaribisha wageni wetu waliotoka nje ya Visiwa vyetu. Karibuni sana na mjisikie mko nyumbani.
Ndugu Mwenyekiti,
Mkutano huu wa pili wa hali ya siasa Visiwani mwetu, wenye mada zilizojikita kwenye lengo la kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni muhimu kwa maendeleo yetu ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Mada zilizojadiliwa hapa ni za msingi katika kuendeleza na kuifanya Serikali yetu kuwa bora zaidi itakayoweza kuwatumikia watu wake kwa uzuri zaidi. Hapa sina budi kuipongeza REDET kwa maandalizi mazuri ya mkutano huu uliojadili mada zifuatazo:-
1. misingi ya kikatiba ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa;
2. ushirikishwaji wa Wazanzibari;
3. kujenga imani ya wananchi katika Sserikali ya Umoja wa Kitaifa;
4. Namna Baraza la Wawakilishi na Serikali (yaani mhimili wa utendaji) vinavyofanya kazi katika mpangilio wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na
5. nini kifanyike kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa;
Tukiangalia hayo yote tunaona wazi kuwa ili Serikali ya Umoja wa Kitaifa ifanye kazi vizuri ni lazima hayo yawe wamewekwa sawa. Kwa kweli zilikuwa mada nzuri sana na zitatoa mchango mkubwa katika kuimarisha Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifa, hasa tukizingatia kwamba Serikali hii imeletwa na Wazanzibari wenyewe kwa hiari zao.
Ndugu Mwenyekiti,
Mada hizi nzuri zilizotayarishwa na wataalamu wetu mahiri na kujadiliwa kwa kina na hadhira makini ni hatua moja muhimu ya kwenda mbele. Rafiki zetu Wachina wanao usemi usemao: “safari ya maili mia moja huanza na hatua moja”. Nasi safari yetu ya kwenda kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyo imara imeshaanza na naamini kasoro mlizozigundua wataalamu wakati wa utekelezaji tukizirekebisha tutapiga hatua nyengine muhimu ya kuelekea katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyo imara zaidi.
Lakini hata hivyo, ni vyema pia tukaelewa kuwa hatuwezi kujenga nyumba imara ya jiwe kwa siku moja na tukaishi humo. Utamaduni ule ule wa kustahamiliana utahitajika kufikia hatua nyengine tunayoitaka. Utamaduni tulioutumia wa kuleta mabadiliko bila ya kujali maslahi ya mtu au kikundi fulani bado unahitajika kwani gharama ya kufanya mabadiliko kwa lengo la kutaka mtu au watu, kikundi au vikundi fulani vinufaike ni kubwa inayoweza kuturejesha tunakotoka.
Mabadiliko kwa mwanadamu ni jambo lisilozuilika na kama hatupendi mabadiliko hatuwezi kupata maendeleo. Lakini nadhani mabadiliko ya mwendo wa haraka haraka yanaweza yasitusifikishe tunakotaka kwenda. Uzoefu wa mataifa yaliyofanya mabadiliko ya haraka haraka kama Urusi kwa mfano tunaujua.
Jambo moja la msingi ni kwamba kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuliamuliwa kwa kura ya maoni. Sio kila mtu basi alikubaliana na hilo, ndiyo maana matokeo ya kura za maoni kuhusu jambo hili yalionyesha asilimia 62 ndiyo waliokubali. Bila shaka wapo waliokataa. Kwa hivyo, wale waliokataa ni vyema wakaona uzuri wa Serikali hii ili nao sasa iwe rahisi kushawishika na kuiunga mkono na kuitetea kwa nguvu zao zote. Kwa Mzanzibari yeyote aliyoifahamu hali ya kisiasa nchini mwetu atakubaliana na watu wengi kuwa mabadiliko yametokea tangu kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Katika kusisitiza hilo labda nitoe mfano wa hivi karibuni tu. Mwezi mmoja uliopita tulisherehekea miaka 48 ya Mapinduzi, na kila mmoja wetu aliona kuwa ushiriki wa wananchi ulikuwa wa hali ya juu. Wazanzibari kwa pamoja bila ya kujali itikadi za kisiasa, tulishirikiana na kufanikisha sherehe hizo, tofauti na miaka ya nyuma, jambo ambalo linaashiria kuwepo kwa mshikamano baina ya Wazanzibari kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.
Nina imani kubwa kuwa imani sasa inajengeka kwa wale waliokuwa na mashaka hapa na pale kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaweza kufanya kazi nzuri na inahitaji kuungwa mkono kwa hali zote. Kwa wanasiasa jambo hili lilionesha ukomavu mkubwa. Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa imeazimia kufanya kazi kwa kuweka maslahi ya wananchi mbele kwanza kuliko maslahi binafsi. Ndiyo maana hakuna jambo linaloamuliwa na mtu mmoja peke yake bali Serikali nzima chini ya Uongozi wa Baraza la Mapinduzi. Tukisema huu ni uamuzi wa Serikali, uamuzi huo umefikiwa katika misingi hiyo.
Ndugu Mwenyekiti,
Hakuna kitu duniani hapa kinachotengenezwa na mwanadamu ambacho hakiwezi kuboreshwa zaidi na zaidi. Hata nyumba huwezi kuijenga mara moja ikaisha. Marekebisho ya hapa na pale hufanyika. Uboreshaji waweza kutokana na changamoto zinazojitokeza siku hadi siku. Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifa ina changamoto nyingi, zile za kawaida za Serikali yoyote, na zile za Serikali za namna hiyo. Sisi tulio Serikalini tuko tayari kusikiliza mawazo ya kujenga kuhusu changamoto hizo yanayotoka kwa wadau mbali mbali na kuyafanyia kazi. Tunategemea kupata mchango wa kuifanya Serikali yetu kuwa bora zaidi na imara zaidi, kutokana na maoni, mapendekezo na maazimio yaliyotokana na mkutano huu. Serikali itakuwa makini kuangalia mapendekezo hayo ili yaweze kuboresha si Serikali tu bali hata Taasisi nyinginezo zinazohusiana na utendaji kazi wa Serikali yenyewe.
Tumesema na tutaendelea kusema na kuhimiza kuwa watendaji wetu wabadilike, wasifanye kazi katika utaratibu wa “business as usual”. Hatutowatendea haki wananchi na hiyo siyo azma ya Serikali hii.
Ndugu Mwenyekiti,
Napenda kuwashukuru watoa mada wote na wale waliojadili mada hizo hadi kufikia mapendekezo yaliyotokana na majadiliano hayo na ambayo naamini yatafanyiwa kazi na vyombo mbali mbali kutegemeana na yalikoelekezwa.
Zaidi ya hapo niseme kuwa nategemea REDET itaendelea kutoa nafasi kwa Zanzibar katika programu zake kama ilivyofanya sasa ili nasi tuweze kujadili mambo yetu kwa manufaa ya nchi yetu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.
Niseme tu kuwa Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifa ni tofauti na Serikali za Umoja wa Kitaifa za Kenya na Zimbabwe, kwa sababu Serikali hizo ziliundwa baada ya kutokea migogoro iliyotokana na uchaguzi. Serikali hizo ni za muda. Yetu ni ya kudumu na imo ndani ya Katiba ya Zanzibar.
Baada ya kusema hayo, naomba niseme kuwa mkutano wa pili wa “Hali ya Siasa Zanzibar” umefunguliwa rasmi. Nawatakia wote safari njema wale mtakaosafiri mbali na tunawakaribisha tena katika Visiwa vyetu vya Zanzibar, Visiwa vya marashi ya karafuu kama wengi wanavyopenda kuviita, kwa ajili ya shughuli za kikazi au za kiutalii.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom