TUCTA yaikamia CCM 2010

JoJiPoJi

JF-Expert Member
Aug 8, 2009
2,907
3,261
na Christopher Nyenyembe, Mbeya


TAMKO lililotolewa na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), huku wakitangaza kuunga mkono waraka wa Kanisa Katoliki, linahofiwa kuweza kukisambaratisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa uchaguzi mkuu mwakani, baada ya serikali kuongeza sh 4,410 kwenye mshahara wa kima cha chini.
Kutokana na kuongezwa kwa kima hicho cha chini, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA taifa, Nicolaus Mgaya, alisema wanatarajia kukutana jijini Dar es Salaam hivi karibuni, pamoja na mambo mengine, kuangalia namna ya kuandaa waraka kwa wafanyakazi wote ili kuwaandaa waweze kuwachagua viongozi bora watakaotetea masilahi ya wafanyakazi.
Akizungumza wakati wa kupokea maandamano ya wafanyakazi mkoani hapa kupinga ongezeko hilo la mshahara la sh 4,410 kwa kima cha chini, lililotolewa na serikali hivi karibuni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010, Mgaya alisema kiasi kilichoongezwa ni sawa na kumzika mtu angali hai.
“Kanisa Katoliki lilitoa waraka, baadaye walifuata Waislamu, madhumuni ni kuwaelimisha waumini wao jinsi ya kuchagua viongozi bora mwakani, sisi tunawaunga mkono na tukirudi Dar es Salaam, tutakutana kuangalia jinsi ya kuandaa waraka kuwatayarisha wafanyakazi kupiga kura katika uchaguzi mkuu mwakani ili wawachague viongozi bora watakaotetea masilahi ya wafanyakazi,” alisema Mgaya.
Naibu katibu mkuu huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa Bunge sasa limegeuzwa kuwa kijiwe cha wastaafu kwenda kulala bungeni badala ya kuwa sehemu ya kutetea masilahi ya taifa na watu wake, ambao wengi kipato chao ni kidogo na hakina uwiano na wale waliowachagua.
Huku akishangiliwa na wafanyakazi walioshiriki maandamano hayo, Mgaya alisema vyama vya wafanyakazi havikuhusishwa kuandaa ongezeko hilo kama yalivyo makubaliano ya TUCTA na serikali, bali limetolewa kinyemela, hatua aliyotahadharisha kuwa ni hatari, kwani inawagonganisha viongozi wa TUCTA na wafanyakazi.
Pamoja na udogo wa nyongeza, ambayo wameiita kuwa ni matusi kwa wafanyakazi wa chini na kati, naibu katibu mkuu huyo aliitahadharisha serikali dhidi ya utaratibu wake wa sasa wa mishahara aliodai unatoa upendeleo kwa baadhi ya taaluma.
Katika risala yao iliyosomwa na Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mbeya, Kibwana Njaa, wafanyakazi mkoani hapa wameionya serikali dhidi ya hatua yake ya kuwapuuza wafanyakazi na kuitaka ianze mara moja kulipa kima cha chini cha sh 315, 000 kwa mwezi.
Alisema TUCTA inaitaka serikali ilipe sh 315, 000 kama kima cha chini kwa mwezi, vinginevyo hawataiunga mkono katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tunapenda kuitahadharisha serikali kwamba kupuuza suala la mishahara ya wafanyakazi ni jambo la hatari sana na kwa vyovyote vile, litaigharimu kwenye uchaguzi mkuu mwakani,” alisema.
Alisema wafanyakazi hawawezi kuifumbia macho hali hiyo na maandamano haya ni mwanzo wa mchakato wa safari ndefu kuelekea ilipo haki yao.
Pengine hatujui siku wala saa ya kufika, lakini lazima tutafika,” alisema Njaa.
Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na Tanzania Daima baada ya maandamano hayo, walielezea hofu ya TUCTA kuweza kuisambaratisha CCM katika uchaguzi mkuu mwakani.
Wafanyakazi hao walipinga nyongeza za mishahara na makato ya kodi kwa madai kuwa hiyo ni aina nyingine ya ufisadi, unaofanywa na viongozi wachache wanaotaka kujinufaisha, huku kundi kubwa la wafanyakazi likiumia.
“Wafanyakazi wote tumeungana chini ya umoja wetu kudai haki kwa amani, hizo zote ni ishara za watu kuchoka, wanajua jinsi wakubwa wanavyoitafuna nchi kwa ufisadi, wananchi hao wakiungana na waraka wa Kanisa Katoliki, CCM imekwisha,” alisema mfanyakazi, Musa wa mkoani hapa. “Sisi wafanyakazi ni waelewa na ni wasomi, endapo tutaamua kwa nguvu kusimamia msimamo wetu kuungana na waraka huo, itakuwa hatari kwa CCM, kwani inaweza kusambaratika, maana laana ya kuwadharau wafanyakazi itawatafuna,” alisema.


Chanzo:
Tanzania Daima
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=8791
 
Last edited:
Hili suala linaweza kuipindua CCM mwakanai kama wafanyakazi wote watakuwa kitu kimoja na nia moja. Wangelivichukua hivyo vijisenti vya Mzee Chenga tu, basi wasingelikosa kuwaengezea watu mara mbili ya hizo walizotoa!
CCM kazi kwao, maanake wafanyakazi nao wakitoa muungozo wao, basi sura itabadilika nchini.
But the question is: Who is next? Serikali ya wafanyakazi, waislamu au wakatoliki? Hatari inatusogelea nchini!
 
Nao TUCTA wanatakiwa kufanya kweli sio yanakua maneno matupu. Na wakikosea hapo wakaishia kutishia mtu mzima nyau wajue wamekwisha ccm ikirudi.

Muungano wa vyama vya wafanyakazi umeleta mapinduzi sehemu nyingi duniani. Hapa Tz viongozi wao wanasambaratishwa kijasusi na kushia kupiga makelele tu.
 
Hizi kelele za ukombozi zilikuwa zinasikika kwa mbali sana na hata taswira yake tulikuwa hatuioni kabisa,lakini kwa hapa tulipofikia naanza kupata picha halisi,hii sio kazi ya TUCTA peke yake ni shughuli kubwa inayotakiwa ifanywe na kila mtanzania kwa lengo moja la kujitoa kwenye hii minyororo sugu tunayoendelea fungwa!!!
 
Back
Top Bottom