Tucta wasalimu amri (MZEE J.K. AMESHINDA)

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
headline_bullet.jpg
Wasitisha mgomo uliopangwa kufanyika leo
headline_bullet.jpg
Wasema lengo kusubiri kikao cha Jumamosi
headline_bullet.jpg
Rais wake asema wanajipanga kujibu hoja



Ayoub%281%29.jpg

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, Omar Ayoub Juma, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuhusu kusitishwa kwa mgomo wa wafanyakazi uliotakiwa kuanza leo.



Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limetangaza kusitisha mgomo wa wafanyakazi uliopangwa kuanza nchini kote leo, huku likiwalaumu wasaidizi wa Rais Jakaya Kikwete kwa kumpotosha juu ya mwenendo wa majadiliano kati yao na serikali kuhusu nyongeza ya kima cha chini cha mshahara, hali iliyosababisha kuitwa waongo.
Uamuzi wa kuusitisha mgomo huo, ambao umechukuliwa na Tucta siku moja baada ya Rais Kikwete kuuelezea mgomo huo kuwa ni batili na kinyume cha sheria, ulitangazwa na Rais wa shirikisho hilo, Omari Ayoub, alipozungumza na waandishi habari, jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo na wanahabari uliitishwa kwa lengo la kueleza msimamo wa Tucta baada ya Kamati ya Utendaji Taifa ya Shirikisho hilo kumaliza kikao chake cha dharura, kilichojadili kuhusu hatima ya mgomo huo.
Ayoub alisema wamefikia uamuzi huo ili kusubiri kikao cha Jumamosi wiki hii kati yao na serikali, ambacho ndicho kitatoa mwelekeo kuhusu mgomo huo.
Alisema kauli ya Rais Kikwete kuwa wao ni waongo, imewasikitisha kwani inaonekana wasaidizi wake wamempotosha kuhusu mambo mengi waliyoyazungumza.
“Hatukutarajia kabisa Rais kuzungumzia lugha ya vitisho na kutumia silaha za moto kwa wafanyakazi kwa jambo la kudai haki zao kisheria. Tunasisitiza kuwa mamlaka yenye haki ya kubatilisha mgomo kwa mujibu wa Sheria namba 6 ya mwaka 2004 ni Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi,” alisema.
Ayoub alisema wanatarajia kujibu katika vyombo vya habari shutuma zilizotolewa na Rais Kikwete muda wowote kuanzia sasa ili kuweka mambo sawa.
“Tunawaomba wafanyakazi wote nchini wawe na subira, watuamini viongozi wao, wawe na mshikamano wakisubiri matokeo ya mazungumzo ya tarehe 8/5/2010 kuhusu masuala yote yanayolalamikiwa,” alisema.
Aliwataka wafanyakazi kutambua kuwa viongozi wa Tucta hawakuwa waongo wala wanafiki na Rais hakuwatendea haki kwa kuwahukumu bila kuwasikiliza.
“Rais Kikwete alitumia maelezo ya upande mmoja katika hotuba yake. Mfano barua ya Katibu Mkuu Hazina ya Aprili 23, mwaka huu, inaonyesha kuwa tulialikwa saa nane na nusu na wala siyo saa nne kama ilivyoelezwa,” alisema.
Alisema serikali iliwaita Machi, mwaka huu kwenye mazungumzo, ambayo yalikuwa tayari yameshapitwa na wakati kwa mujibu wa sheria ya majadiliano ya watumishi wa umma namba 19 ya 2003.
Alisema kwa heshima ya Rais, Tucta ilikubali kurudi meza ya mazungumzo, lakini hata baada ya kurudi, mazungumzo hayakwenda vizuri.
Kuhusu kima cha chini, Ayoub alisema pamoja na upande wa wafanyakazi wa sekta ya umma kukubali kushuka kiwango, wawakilishi wa serikali walizidi kukataa na waliishia kukubaliana kutokubaliana kama ilivyoonyesha kwenye tamko la mwenyekiti wa baraza hilo.
“Mheshimiwa Rais Kikwete katika hotuba yake anavyosema majadiliano yataendelea tarehe 8 mwezi huu si kweli kwa sababu mjadala ulishafungwa kwa kukubaliana na kutokukubaliana, hivyo inaonyesha ni dhahiri kuwa Rais hakupewa taarifa sahihi bali alipotoshwa kwani hata kwenye kikao kinachokuja hili halitazungumzwa kwani utaratibu wake ulishafikia mwisho,” alisema.
Juzi akihutubia taifa kupitia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema mgomo huo ni batili na yeyote atakayethubutu kugoma atachukuliwa hatua za kisheria na taratibu za kazi.
Alisema mgomo huo ni batili kwa vile umeitishwa katikati ya majadiliano kati ya serikali na Tucta kuhusu madai ya wafanyakazi.
Rais Kikwete alisema kiwango cha mishahara kinachoombwa na wafanyakazi kupitia Tucta, hakiwezi kutekelezeka hata kama mgomo huo utafanyika kwa miaka minane mfululizo.
Alienda mbali zaidi kwa kusema iwapo wafanyakazi wanafikiria kumnyima kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa serikali kushindwa kutekeleza madai yao, yuko tayari wamnyime, lakini serikali haiwezi kuwadhulumu Watanzania milioni 39 kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache.



CHANZO: NIPASHE

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) waogopa kufanya mgomo ama kweli waswahili husema (MIAFRIKA BWANA NDIVYO ILIVYO) Tutaendelea kweli jamani? wanaokufa njaa ni Wanyonge Mwenye nguvu mpishe apite. Mungu atusaidie walala hoi.
 
Back
Top Bottom