TRL kwenda likizo bila malipo!?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
TRL kwenda likizo ya bure

Imeandikwa na Na Shadrack Sagati; Tarehe: 26th February 2010 @ 23:59
Habari Leo

WASIWASI umetanda miongoni mwa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) baada ya kuambiwa na viongozi wao kuwa watapewa likizo ya lazima miezi sita bila malipo.

Hatua hiyo inatokana na kampuni hiyo kushindwa kuzalisha kutokana na miundombinu kuharibiwa na mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro.

Habari zinaeleza kuwa kwa vile hakuna uzalishaji ni vyema wafanyakazi wakabaki nyumbani kusubiri kutengemaa kwa miundombinu hiyo.

Jana Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Sylvester Rwegasira, aliwaambia wafanyakazi wa TRL, kuwa menejimenti ilimwita kumweleza jambo hilo, lakini akawajibu kuwa suala hilo haliwezekani.

"Nimemwambia Mkurugenzi, kwamba hilo jambo haliko kwenye mkataba wao, hivyo haiwezekani wafanyakazi kupewa likizo ya miezi sita bila malipo,” alisema Rwegasira wakati akizungumza na wafanyakazi hao.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo, alipoulizwa kama Serikali imetoa agizo hilo kwa menejimenti ya TRL alijibu: “Hayo masuala ya TRL waulizeni wenyewe, hiyo ni kampuni yao na wana mamlaka ya kuyazungumzia … mimi sina cha kusema.”

Meneja Uhusiano wa TRL, Midraj Maez, alipoulizwa juu ya suala hilo alisema: “Naomba hilo muulizeni Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, ndiye mwenye mamlaka ya kuzunguzia suala hilo, mimi sina cha kusema juu ya suala hilo.”

Lakini Rwegasira katika mkutano wake jana aliwambia wafanyakazi hao kuwa aliyetoa notisi hiyo ni vyema aende kwa wanasheria wakamshauri, kwani wao wafanyakazi hawatakubali kwenda likizo bila malipo kwa vile suala hilo halimo kwenye mkataba wao wa hiyari.

“Sisi tuna ajira za kudumu, haiwezekani mtu akaamka usingizini akaota kutupa likizo bila malipo, tena yawezekana mtu huyu hana huruma, kwani sisi tuna watoto na familia iweje twende likizo bila malipo?” Alihoji Katibu huyo.

Alisema wao hawakubaliani na hali hiyo kwa vile chanzo cha matatizo ndani ya TRL kimetokana na mkataba mbovu ambao Serikali imeingia na wawekezaji hao hadi kusababisha uzalishaji kusuasua.

Katibu Mkuu huyo alishauri Serikali kuwa badala ya kuwapa likizo wafanyakazi, ni vyema ikashughulikia utengenezaji wa mabehewa mabovu ili miundombinu itakapotengemaa, waweze kuyatumia.

“Sasa wanatuumiza sisi wafanyakazi, kwa kweli inatusikitisha,” alisema Rwegasira na kuwataka wanachama wake wahakikishe kuwa wanapata taarifa kutoka kwa chama chao juu ya suala hilo na wasiisikilize menejimenti.

Aliwahakikishia kuwa watafanya kila wanaloweza suala la kuwapeleka likizo bila malipo lisiwepo na badala yake wafanyakazi waendelee na kazi licha ya kuwa kwa sasa hakuna uzalishaji.

Kutokana na kampuni hiyo kutozalisha katika kiwango chake, Serikali imechukua jukumu la kuwalipa mishahara wafanyakazi hao. Imekuwa inatoa zaidi ya Sh milioni 800 kuwalipa.

 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom