This is what is happening...!

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
This is what is happening to my life now - nimechoka kabisa kuamka asubuhi
sana only to find out that my salary ends kwenye michango ya watu!

MICHANGO! Ah Mungu wangu weee... Nchi gani hii kila ukiamka, kila ukiwa
njiani, ofisini au ukilala ni kusakamwa na michango tu?

Michangooo, michangooo, michangoo tu! Twatolewa weeeee mpaka tumepata
pancha.

Hapana jamani. Hakikyanani tena sasa mmezidi.
Amka asubuhi utasikia hodi, ukifungua kuna mtoto wa jirani na kikadi
kilichoburuzwa kwenye kompyuta kikiomba mchango wa "kitchen party." Toba!
Unamwambia utawasiliana na baba yake anaondoka.
Upo kwenye daladala unawahi Pugu rodi kazini, unaombwa samahani na mtu
akidai alikuwa na barua yako na anakupatia bila hiana. Mtumeee! Unafungua
unakuta ni kakadi kengine ka mchango. Safari hii ni ka "chicken party na
kameonyesha kiwango kabisaa. Kwa fasheni ya sasa ni 7,000/-.
Huyu ni wa aibu, hivyo unampa dala ukidai mbili utamtuma mtoto.

Unatoka kazini hujala chochote kwa vile 5,OOO/= ulitoa kwenye"chicken party"
ambayo hata maana ya neno lenyewe hujui. Unakuta kengine nyumbani. Hako ni
ka mchango wa "send off'. Jamani mwanitakani lakiniiii?

Unaoga, ghafla aja mtu na kadi, tena safari hii ni mchango wa harusi ya
shemejiyo. unajikamuakamua ili usiadhirike ukweni. Unampatia kiasi
kilichokuwa ada ya Sikujua shuleni.

Hapo bado kuhudhuria vikao vya shemejio vya harusi. Nako kuna ka mchango ka
kila mkutanapo kanaitwa uchache au chakaza.Shemeji mtu tena si ni lazima
wakukamue kamasi mwanangu?

Haiishii hapo. Unakuja ujumbe kuwa dada yake dada wa mama yako mzazi kafia
Muhimbii yuko mochwari. Hapo achilia mbali bakuli la mchango utakalokuta
linakungoja. Patakuwepo pia kitabu cha kujiorodhesha wanandugu na kiasi
mtakachotoa.

Yallah! Michango haitoshi. sasa yabidi wale wa karibu yake mjazie ili
iwezekane kukodisha "Fuso" ya kumpleka kwao Mbagala. Na huko nako ni lazima
mkamuliwe tena hela ya kununulia mboga.

Unasema walau sasa napumua. Mara inatoka barua kwa wajomba zako kuwa ile
arobaini ya babu ni mwezi ujao. Na unatakiwa mchango wa kununulia nyama na
mchele kwa ulaji wa siku hiyo.
Kwani utakimbia jamii yenu kwa vile imekuwa ya michango?
Haya tena. Kazini nako wameanza kukukata mshahara kwa madeni uliyo nayo
SACCOS. Mtoto wa jirani ambaye umemdhamini ubatizo naye aja akidai mchango
wa kununulia gauni la "birthday".

Ebo! Sasa mwanangu? Utasahau mdogo wenu wa mwisho aliepigwa ritrenchi na
sasa ana mtoto mchanga wa kubatiza... Utakwepa vipi usimchangie kitu kidogo
atakapowahi kwako majogoo?

Afadhali usingezaliwa Kipatimo mwanangu. Mwezi huu ni wa kuwacheza watoto.
Utawaambla nini huko kwenu wakuelewe kama hukutuma mchango wa hilo tamasha
ambapo mwezi uliopita mtaa wa pili alipochezwa Sikuzani watu walikula
wakasaza?

Bado wana wewe kaka!
Mtoto wa kaka yako anapata komunio utamkwepaje mbele ya jamii
iliyokuzunguka? Na asavali tajiri yako asingekuwa na mtoto Chuo Kikuu
anayegradueti mwisho wa mwezi na keshakuletea kadi ya mchango.
Utachangia sana graduesheni ya sekondari, chekechea hata na darasa la
saba, nini VETA...
Mtajiju ! Kwani nani aliyewatuma kuzaliwa Bongo? Asavali wanajeshi hawana
sherehe hata wapatapo usaameja.

Utadhani sasa utapumua uendapo nyumba za ibada. Toba yaillahi! Huko
Utakutana na michango ya ofisi ya paroko, mchango wa jengo na pikipiki ya
shemasi - kama sio mchango wa madrasa, mchango wa majamvi msikitini ama
mchango wa kofia ya imamu. Upo hapo?

Huko kijijini ndo usiseme. Kuna barabara, shule, maji, zahanati, ugeni wa
DC, vyote vyadai mchango na mara nyingi hakuna risiti. Si ni jamaa zako una
wasiwasi gani weye?

Umesahau mfereji wa kijiji, trekta la mshikamano, shamba la kijiji na
kadhalika - vyote navyo vyataka michango; achilia mbali mchango wa damu
Muhimbili! Ila asavali huu wa damu kwa vile hauhusu fedha.

Unafikia mahali unasema utapanchi hiyo michango. Ukiwaza hayo, mara anapita
Katibu kata mwenyewe. Huyu anadai mchango wa mapokezi ya Waziri Mkuu au ya
Mwenge utasemaje?

Unaambiwa hakuna cha huruma na mtu wala hakuna wa kutaka kujua kipato
chako kabla hajakupa kadi ya mchango.
Shuleni watatuma barua kuhusu mchango wa kumuaga mwalimu mkuu. Bado
michango ya tuisheni, uji wa saa nne, safari ya Serengeti na T-shirt za siku
ya michezo shuleni.
Hapo usisahau redio ya shule ikikosa betri wazazi shurti mchangishwe.
Mwashangaa nini, kwani hospitalini hamchangii?

Michango hii!
Sasa mtatukamua mpaka damu. Ipo ya kwaya, Saidia Simba Ishinde, usafi wa
makaburi, basi la kijiji. Bado sijasema michango ya SACCOS na upatu kazini
kwenu.
Enheee, halafu mama watoto anacheza mchezo. wiki hii zamu yake kutoa na
mama nanihino kaja jana kukumbushia asicheleweshewe kama safari ileee...
Hujakaa sawa hodi! Wakala wa wazoa taka yuko mlangoni na kitabu chake cha
risiti mkononi. Anang'aka kwamba safari hii usipotoa atakuripoti kwa
mwenyekiti wa mtaa kwamba huna ushirikiano katika mambo ya kutunza
mazingara.
We haya weee... kufa hatufi, lakini cha moto twakiona
 
Back
Top Bottom