Tendwa anatumika ili kubariki gulio haramu

Zak Malang

JF-Expert Member
Dec 30, 2008
5,404
233
(Uchambuzi)

Na Mbasha Asenga

WAKATI Msajili wa Kwanza wa Vyama vya Siasa nchini, George Liundi, alipomaliza utumishi wake kwenye ofisi hiyo na ghafla akatangaza na kuanza harakati za kusaka ubunge wa Afrika Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), watu wengi walijiuliza hivi kiongozi huyo alikuwa CCM tangu lini?

Wapo walitoa majibu mepesi kabisa juu ya swali hili gumu na zito, wakisema alikuwa mwanachama wa CCM kabla ya kuteuliwa kuwa msajili wa vyama, na kwa sababu sheria hairuhusu msajili kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa, aliacha uanachama wake kwa muda, lakini baada ya utumishi wake eti akaufufua!

Hayo yalikuwa majibu mepesi kwa swali gumu linalogusa uadilifu wa kiongozi anayekalia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

Ugumu wa swali hili unatokana na unyeti wa ofisi hiyo, kwamba kiongozi wake ambaye analindwa na sheria na ambaye maamuzi yake kuhusu vyama ni amri inayoweza kuathiri kwa kiwango kikubwa mno ustawi wa chama chochote cha siasa.

Ndiyo maana sheria ikataka mwenye kukalia kiti hicho kamwe asishabike chama chochote kwa kuwa huyu ni kama refa. Hadi leo kitendo cha Jaji Liundi cha kujitokeza punde na kuanza kusaka ubunge kupitia CCM bila kwanza kuwa ametimiza sharti la lazima la CCM la kuwa mwanachama kwa miaka mitano kabla ya kujitosa kwenye nafasi ya kuchaguliwa, kimeacha doa kwamba huenda katika utendaji wake kiongozi huyo alikuwa akisaidia CCM miaka yote hiyo.

Wakati ya Jaji Liundi yakiwa ni historia, juzi Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, naye ameonyesha dalili mbaya kwamba huenda naye ni kama mtangulizi wake, kwamba ingawa haruhusiwi kushabikia chama chochote kati ya vilivyopo na akiwa hana uhuru wowote wa kujiamuliwa mambo atakavyo nje ya kanuni sheria na taratibu, ametoa kauli inayoonyesha wazi kuibeba CCM.

Wawakilishi wa vyama vya siasa na wadau mbalimbali walikutana na Tendwa kwa nia ya kupitia mapandekezo ya rasimu ya kanuni ya sheria ya fedha za uchaguzi ya mwaka 2010, kwa mujibu wa waliohudhuria kikao hicho taarifa ambazo na Tendwa mwenyewe amethibitisha, mapendekezo ya vyama yaliyokuwa yemetolewa tangu mkutano wa kwanza, yalitupwa na hivyo kutumbukizwa mapya ambayo yanafanana na harakati, nia na kampeni za CCM za kusaka Sh. 40 bilioni za uchaguzi.

Kwa njia ambayo dhahiri inaonyesha kwamba waamuzi juu ya kima cha fedha za uchaguzi si vyama vya siasa na wadau wengine ambao wamekwisha kukutana na masajili mara mbili katika mikutano ya kuandaa rasimu ya kanuni ya utekelezaji wa sheria hiyo, Tendwa aliwataka wasiokubaliana na kiasi cha Sh. 40 bilioni wawasilishe mapendekezo yao kwa maandishi naye atawasiliana na serikali kufanya maamuzi ya mwisho.

Ni kweli, msajili wa vyama vya siasa ametajwa kama masimamizi mkuu wa sheria ya uchaguzi, na ameonyesha dalili za kutaka kuhusisha wadau wengi zaidi katika kupatikana kwa kanuni hizo.

Lakini tatizo kubwa linaibuka pale watu wanapoona sasa njia inapindishwa kusaidia kufanikisha matakwa ya CCM, huku Tendwa mwenyewe akijidhihirishwa wazi kuwa wakala wa chama tawala.

Mwenendo huu mpya wa Tendwa umenikumbusha ule wa mtangulizi wake mara baada ya kumaliza utumishi wake, kwamba kumbe ijapokuwa sheria inafunga kiti hicho kutokufungamana na chama chochote, ukweli ni kwamba kila akikaliae anawakilisha CCM. Ni fedheha na aibu kwa mfumo wa utawala wa sheria kuwa na aina ya watu wanaoshindwa kutawala matamanio yao dhidi ya matakwa ya kisheria.

Kwa walio wengi walidhani nia ya sheria ya fedha za kugharimia uchaguzi pamoja na mambo mengine ni kuepusha matumizi ya fedha chafu katika uchaguzi, lakini pia kuratibu matumizi yanayokubalika kisheria katika uchaguzi; kubwa zaidi kuliokoa taifa na kansa ya matumizi yaliyopindukia ya fedha katika uchaguzi kwa sababu kwa kumwaga fedha kiasi hicho ni sawa kabisa na kununua kura.

Ununuaji wa wapigakura ni moja ya mapokeo mapya ya siasa za vyama vingi, lakini ambayo yamesababisha fedha kuwa kigezo cha kushinda uchaguzi na si sifa za mgombea au ilani ya chama chake. Kwa ilivyo, uchaguzi umegeuzwa kuwa gulio kubwa la kitaifa, kwamba wenye fedha wanakuja na fedha zao na wenye kura wanakuja na kura zao wanakutana gulioni, mwisho tunapata wenyeviti wa mitaa, madiwani, wabunge na hata rais wanaotokana na nguvu ya fedha.

Kama nia ya Rais Jakaya Kikwete tangu 30 Desemba 2005 alipotangaza nia ya kuweka utaratibu unaokubalika wa matumizi ya fedha katika uchaguzi ilikuwa ndiyo hiyo iliyotupa sheria hii mpya ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010, basi kuwaza kutumia Sh. 40 bilioni kwa ajili ya uchaguzi si kufuru na uhalalishaji wa gulio la uchaguzi tu, bali ni kufungua milango zaidi kwa fedha kuwa kigezo namba moja cha mtu kupata uongozi kwa njia ya kura.

Ni kwa hali hii hisia za baadhi ya wanasiasa kwamba ofisi ya msajili wa vyama vya siasa haikuwa taasisi sahihi ya usimamizi wa sheria hii, inaaza kupata nguvu kadri siku zinavyokwenda katika utekelezaji wa sheria husika.

Ni vigumu mno kushawishi wananchi hadi waelewe kwamba matumizi ya Sh. 40 bilioni ni halali katika kusaka nafasi za kuchaguliwa. Huu ni ufujaji mkubwa wa fedha ambao unatafutiwa baraka kwa kupitia mgongo wa Tendwa.

Haukubaliki na kwa kweli ni njia nyingine ya kuminya demokrasia na maana nzima ya mchakato wa uchaguzi kwa ujumla. Kama fedha hizi zitapitishwa, basi tuseme tu uchaguzi wetu ni gulio la kitaifa.

Source: Mwanahalisi toleo na. 184
 
Tatizo tunaloliona tulio wengi ni jinsi gani sheria hii itatekelezwa ili kutimiza matarajio ya walio wengi maana chaguzi zetu kwa muda mrefu zimekuwa zikitawaliwa na matumizi makubwa ya pesa.

Hili ni dhahiri maana hata Rais mwenyewe alikiri kipindi fulani na ndipo kuahidi kuletwa sheria hii.lakini kama ambavyo tumeshaona manung'uniko ya walio wengi tangu kupitishwa kwake na kauli za msajili,tunapata picha ya kwamba utekelezaji wake utakuwa wa ubabaishaji.

Matokeo yake badala ya kuwa tiba kwa matumizi ya fedha kwenye chaguzi itakuwa chanzo cha utengenezaji wa kesi nyingi za uchaguzi.

Hivyo msajili kwa kushirikiana na Takukuru ni wakati wao sasa kuturidhisha kuwa watatimiza wajibu wao wa msingi kwa utekelezaji wa sheria hii,la sivyo chaguzi zitaendelea kuwa gulio la kutafutia madaraka na utajiri haramu kama alivyowahi kusema Fred Mpendazoe alipoamua kujitoa C.C.M.
 
Hivyo msajili kwa kushirikiana na Takukuru ni wakati wao sasa kuturidhisha kuwa watatimiza wajibu wao wa msingi kwa utekelezaji wa sheria hii,la sivyo chaguzi zitaendelea kuwa gulio la kutafutia madaraka na utajiri haramu kama alivyowahi kusema Fred Mpendazoe alipoamua kujitoa C.C.M.

Tusitegemee lolote kutoka kwa Msajili Tendwa wala hao Takukuru maana wote ni 'watumwa' wa Serikali ya CCM. Mpaka hapo CCM watakapokuwa tayari kuheshimu misingi halisi ya demokrasia ndipo tunapoweza kupata viongozi wa kweli wenye nia ya kuwatumikia wananchi na si wale wanaotaka madaraka kwa manufaa yao binafsi.
 
Back
Top Bottom